• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
KILIMO CHA MBOGA: Shule inavyojitosheleza kwa aina zote za vyakula kupitia kwa kilimo

KILIMO CHA MBOGA: Shule inavyojitosheleza kwa aina zote za vyakula kupitia kwa kilimo

Na PETER CHANGTOEK

TAKRIBANI mita 700 kutoka mjini Chuka, ndipo ilipo Shule ya Upili ya Wavulana ya Chuka.

Shule hii imejengwa katika shamba la ekari 53, ambapo sehemu kubwa ya shamba hilo hutumiwa kuziendesha shughuli za zaraa.

Shule hii hutegemea shughuli za kilimo kuwalisha wanafunzi wapatao 1,200 na zaidi ya walimu na wafanyakazi 100 ambao huhudumu shuleni humu.

Kutokana na mauzo ya mazao mbalimbali ya shambani, shule hii ilijinunulia gari mnamo mwaka 2015, na kuyajenga majengo mawili makubwa yenye orofa tatu na mbili mtawalia, mnamo mwaka 2017.

Shamba hili lina mimea tofauti tofauti; mathalani miche 2,213 ya mikahawa katika ekari 3 na migomba katika ekari 2.5.

Aidha, lina mabwawa manne ya kuwafugia samaki, ambapo kila moja lina urefu wa mita 30 kwa mita 70 na kila bwawa lina samaki zaidi ya elfu moja, ambao huvuliwa kila baada ya miezi sita.

Shule hii ina nguruwe 58 ambao hulishwa kwa lishe zinazopatikana shuleni, na hivyo lishe zao huwa hazinunuliwi kutoka kwa maduka.

Pia, ina ng’ombe kumi na wanne amapo wanne hukamwa. Huku wengine wakiwa ndama na mafahali. Ng’ombe hao hulishwa mara mbili kwa siku- asubuhi na jioni.

Miongoni mwa lishe ambazo ng’ombe hao hupewa ni pamoja na nyasi aina ya mabingobingo, nyasi za kawaida, nyasi aina ya ‘Boma Rhodes’, na lishe aina ya ‘silage’.

Shule hii hupata maziwa kati ya lita 43 na lita 60 kwa siku, na maziwa yayo hayo hutumiwa kuwatengenezea wanafunzi, walimu na wahudumu chai.

Isitoshe, ina sungura 12 na mbuzi saba ambao hutumiwa kuwafunza wanafunzi.

Hata hivyo, wanafunzi wanaofanya vyema zaidi darasani, angaa hupata fursa ya kuonja nyama ya mbuzi wakati fulani, hususan mwishoni mwa muhula.

Vilevile, shule hii ya wavulana, ina kuku zaidi ya 150, ambao hutumiwa kuwapa mafunzo wanafunzi, ilhali mayai yanayotagwa na kuku hao hao, hulishwa kwa wanafunzi.

Pia, mimea ya kabeji imepandwa katika shamba robo tatu ya ekari katika shule hiyo ya upili, na mimea mingineyo ya mboga imekuzwa katika shamba ekari moja.

Hata hivyo, licha ya kufanikiwa kwa shule hiyo katika masuala ya kilimo, nusra ifungwe kwa wakati fulani, kwani ilishindwa kudumisha usafi baada ya tanki la kupitisha kinyesi kupata mipasuko, na hivyo kuuchafua mto Naka.

“Kwa miaka kadhaa tulipitia changamoto kadhaa. Tulijaribu mbinu kama vile kuchimba mashimo na mitaro, lakini kuvuja kwa maji taka kukaendelea, na tukapewa onyo na NEMA, na tukawa na hatari ya shule kufungwa, endapo tusingezingatia usafi,’’ asema Richard Mwenda, mwalimu anayehusika na masuala ya chakula, malazi na afya, katika shule hii.

Ufadhili

Ili kuikabili changamoto hiyo kuu, shule hiyo ilituma barua ya kuuomba ufadhili kwa shirika la Upper Tana ili kuiwezesha kuzalisha nishati kupitia kwa biogesi.

Ilipokea ufadhili wa Sh5 milioni kutoka kwa shirika lilo hilo la Upper Tana nayo shule yenyewe ikachangia asiliamia 10 kwa mradi huo.

Biogesi hiyo mhutoa nishati inayotumiwa shuleni kuwapikia chakula wanafunzi, walimu na wafanyakazi.

Pia, Mwenda anasema kuwa kupitia kwa mradi huo wa biogesi, shule hiyo hupata mbolea ambazo ni salama na zenye virutubisho vya nitrojeni, zinazotumiwa kuikuza mikahawa, migomba na mimea mingingeyo shuleni.

Mwenda anasema kuwa, kwa sasa, wao wana uwezo wa kudumisha usafi shuleni, kwa sababu ya kuwapo kwa mradi huo wa kuzalisha nishati kwa biogesi. Pia, huyasafisha maji taka ambayo hunyunyizwa kwa nyasi.

Kwa uhakika shule hiyo imefaidika kwa hali na mali kutokana na shughuli za zaraa, na hivyo kupunguza fedha ambazo zingetumika kuvinunua vyakula kutoka sehemu nyinginezo.

You can share this post!

AKILIMALI: Utapata faida tele ukijitosa katika kilimo cha...

KILIMO CHA MBOGA: Brokoli ni aina za mboga zenye faida tele...

adminleo