Makala

AKILIMALI: Umuhimu wa kujitengenezea chakula cha mifugo

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

UWEKEZAJI aliofanya Mhandisi Joseph O. Makolwal katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, anaokadiria kuwa unaweza kufikia Sh4 milioni si jambo rahisi.

Ikizingatiwa kuwa anafanya kazi ughaibuni, tegemeo lake kufanikisha shughuli hiyo li mikononi mwa wafanyakazi wake.

Hata hivyo, anasema amejifunza kuwa na imani na uaminifu nao, na kila wanachohitaji hasiti kuwatimizia.

Hufuatilia utendakazi wa mradi wake, Williberg Farm, kwa njia ya simu ambapo huzungumza na watumishi wake kila asubuhi, mchana na jioni. “Huwajulia hali kila siku, asubuhi kabla sijaingia kazini ili kujua kiwango cha maziwa walichopata, changamoto na anachofanya kila mfanyakazi. Mchana, hufuatilia kujua kiwango cha maziwa walichouza, yaliyosalia na waliyoafikia nusu ya siku,” afafanua.

Mfugaji huyo ana wafanyakazi wanne, akiwemo meneja na anasema jioni hutaka kujua walivyoshinda, changamoto ibuka na mipango ya siku inayofuata.

Ili kuwapa motisha, Mhandisi Makolwal hushughulikia maslahi yao kwa hali na mali.

“Uzalishaji wa maziwa, mauzo na afya bora ya ng’ombe, huamuliwa na wafanyakazi. Ukiwatunza vyema, hawatakuangusha katika jitihada zako,” aeleza, akisisitiza kuwa furaha ya mfanyakazi ni furaha kwa ng’ombe na matunda yake yatakuwa mapato ya kuridhisha kwa mkulima.

Alizamia shughuli ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa mwaka 2018 na ni shughuli anayoiendeshea Kaunti ya Homa Bay.

Mhandisi Joseph O. Makolwal ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Homa Bay ambaye ana mashine ya kusaga chakula cha mifugo, chaff cutter. Picha/ Sammy Waweru

Katika simulizi ya mfugaji huyo, alipoanza ni bayana kilichomhangaisha ni suala la chakula duni, ambacho hakijaafikia ubora wa bidhaa za mifugo. Watalaamu wanasema ili kufanikisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, sharti mifugo wapate mlo kamilifu; wenye virutubisho na madini faafu. “Virutubisho, madini na ratio ya chakula na kinavyochanganywa, ndicho kiini cha ng’ombe wenye afya bora. Kilele chake kitakuwa kukupa mazao ya kuridhisha,” ahimiza John Momanyi, kutoka Sigma Feeds.

Wakulima wengi wameasi ufugaji wa ng’ombe kwa sababu ya kuwepo kwa chakula ambacho hakijaafikia ubora. Mhandisi Makolwal anaiambia Taifa Leo Digitali kuwa kabla kugundua siri, aligharamika kununua chakula cha mifugo anachokitaja kilikuwa bandia tu. Ni muhimu mfugaji ajue kuwa kampuni nyingi za kutengeneza chakula, huandika kwenye mifuko virutubisho na madini ambayo hawajatia, kwa minajili ya matangazo pekee.

Baada ya kufanya uchambuzi na utafiti wa kina, mfugaji Makolwal alishauriwa kujikuzia nyasi na mahindi, ili aweze kujiundia lishe. “Chakula cha maduka hununua kiasi tu, cha kuchanganya na ninachojitengenezea,” asema.

Kwenye shamba lake, hulima nyasi maalum aina ya boma rhodes, brachiria na napier grass, ambazo ni muhimu katika uongezaji wa maziwa. Pia mfugaji huyo hukuza mahindi, na hutumia majani na matawi ya mahindi kuunda silage.

Nyasi anazokuza pia hutengeneza silage na hay. Vyakula viwapo tayari, huvichangananya na molasses na chumvi ya mifugo.

Ni hatua anayoipigia upatu, akihoji imempunguzia gharama kwa asilimia 70. Isitoshe, kiwango cha uzalishaji wa maziwa kimepanda kutoka lita 7 ng’ombe mmoja hadi zaidi ya 15, kwa siku.

“Chakula ninachowapa nina uhakika wacho, na utawazama ng’ombe wakikifurahia,” anasema.

Mtaalamu John Momanyi anasema chakula kamilifu hushawishi ng’ombe kuzalisha maziwa mengi ya hadhi na yenye ushindani mkali sokoni.