Michezo

Shujaa yajikwaa ikianza kampeni ya Raga ya Dunia mjini Dubai

December 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa imefungua kampeni yake ya Raga za Dunia za msimu 2019-2020 kwa kichapo cha alama 17-12 dhidi ya Afrika Kusini kwenye duru ya Dubai Sevens, Alhamisi.

Shujaa iliongoza 12-5 wakati wa mapumziko kupitia miguso Alvin Otieno na Vincent Onyala, huku Daniel Taabu akaongeza mkwaju wa mguso wa Otieno.

Afrika Kusini ilitangulia kuona lango kupitia kwa Ryan Oosthuizen aliyefunga mguso bila mkwaju kabla ya Kenya kujibu na miguso hiyo miwili. Hata hivyo, moto wa Shujaa ulizimwa kabisa na Afrika Kusini iliyorejea kipindi cha pili katili.

Katika kipindi hiki, Kenya, ambayo inanolewa na kocha Paul Feeney kutoka New Zealand, haikufunga alama, huku Afrika Kusini ikipachika alama za ushindi kupitia miguso ya Rosko Specman na Seabelo Senatla na mkwaju kutoka kwa Justin Geduld.

Katika mechi ya ufunguzi ya Kundi D, Uingereza ilitoka nyuma alama 0-7 na kulipua Uhispania 36-7. Francisco Hernandez aliweka Uhispania mbele kupitia mguso na mkwaju dakika ya kwanza. Hata hivyo, Uingereza ilijibu na miguso kutoka kwa Daniel Bibby, Dan Norton na Tom Emery. Bibby pia alichangia mkwaju katika kipindi cha kwanza. Uingereza ilipata alama zaidi katika kipindi cha pili kupitia kwa Norton, Phil Burgess na Oliver Lindsay-Hague. Bibby aliongeza mikwaju miwili katika kipindi cha pili.

Vijana wa Feeney watalimana na Uingereza katika mechi ya pili mnamo Ijumaa saa sita na dakika 26 adhuhuri kabla ya kukamilisha siku hiyo ya pili dhidi ya Uhispania saa kumi na mbili na nusu. Timu mbili za kwanza kutoka kundi hili zitaingia robo-fainali kuu, huku mbili za mwisho zikiteremka kushiriki mashindano ya Challenge Trophy.

Ikielekea Dubai, Shujaa ilisema inalenga kufika robo-fainali kuu mjini humo kwa hivyo ili kutumiza ndoto hiyo italazimika kupiga Uingereza na Uhispania siku ya Ijumaa.