Eliud Kipchoge atuzwa shahada ya heshima ya udaktari

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge sasa atafahamika kwa jina Daktari Eliud Kipchoge baada ya kupata shahada ya juu kabisa kutoka Chuo Kikuu cha Laikipia, Ijumaa.

Kipchoge, ambaye anajivunia kukamilisha umbali huo kwa rekodi ya saa 2:01:39 kutoka ushindi wake wa Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2018, alikuwa miongoni mwa maelfu ya mahafali waliopokea vyeti vyao katika sherehe hizo za mwaka wa saba.

Kupitia mtandao wake wa kijamii, mshindi huyo wa tuzo ya mwanariadha bora duniani mwaka 2018 na 2019 alithibitisha kupokea shahada yake akisema, “Leo (Desemba 6, 2019) nimepokea digrii yangu ya masuala ya Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Laikipia. Nashukuru familia ya vyuo vikuu kwa tuzo hii muhimu.”

Katika tangazo lake kabla ya mahafali, Chuo Kikuu cha Laikipia kilikuwa kimesema kuwa kitampa Kipchoge shahada hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika nyanja za michezo.

“Seneti hasa inamtambua kwa ufanisi wake wa hivi majuzi wa kuwa binadamu wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa mbili,” Chuo hicho kilisema.

Bingwa wa Olimpiki Kipchoge alitimika mbio maalumu za kilomita 42 za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 jijini Vienna nchini Austria mnamo Oktoba 12 na kuwa mtu wa kwanza duniani kufanya hivyo.

Wiki moja baadaye, mnamo Oktoba 20, Kipchoge alipokea taji kubwa alipotambuliwa kama mmoja wa mashujaa nchini katika siku ambayo alipewa na Rais Uhuru Kenyatta alimpa tuzo ya Heshima ya Elder of the Order of the Golden Heart (E.G.H).