• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MBURU: Watu wachukue tahadhari kuepuka madhara ya mafuriko

MBURU: Watu wachukue tahadhari kuepuka madhara ya mafuriko

Na PETER MBURU

HUKU mvua iliyopitiliza ikiendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini, visa vya mafuriko kuathiri maeneo fulani kwa kuharibu mashamba, barabara, nyumba na hata kusababisha vifo vimekuwa vikiripotiwa kwa wingi.

Katika mengi ya matukio haya, wakazi wa maeneo husika wamelazimika kuhama makwao na kupiga kambi katika maeneo salama ama kuhangaika wanaposafiri.

Lawama kwa serikali kuhusu jinsi imezembea katika ujenzi wa barabara na kutoonya wananchi wanaoishi katika maeneo hatari ama kuwaokoa kunapotokea mafuriko nalo limekuwa jambo la kila siku, visa hivi vikiendelea kushuhudiwa.

Hata hivyo, nachukua mkondo tofauti katika kujadili suala hili leo, kwa kuzungumza na watu wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko ama majanga mengine, ama wenye mpango wa kuishi maeneo hayo.

Kwanza, ni vyema kwa wakazi wa maeneo haya kuchukua tahadhari wakati huu, kwa kuhakikisha kuwa maeneo wanakoishi ama kuenda ni salama, ili kuepuka majanga yanayoshuhudiwa.

Aidha, wakazi wanafaa kuwa makini kila wakati na kufuatilia habari kuhusu maeneo yaliyo kwenye hatari ya kukumbwa na mafuriko ama maporomoko ya ardhi, kupitia vyombo vya habari ama kutoka kwa mashirika yanayohusika na masuala hayo.

Wenye nia ya kununua mashamba pia wanafaa kuwa makini kuhusu mahali wanapoamua kupafanya nyumbani, kwa kufanya uchunguzi kuhusu jinsi maeneo husika huwa nyakati tofauti za mwaka, ili ikiwa ni mojawapo wa yanayokumbwa na mafuriko, kiangazi ama hata utovu wa usalama wawe tayari wanajua.

Hatua hii itasaidia kwa kuwa endapo janga kama hilo linaloshuhudiwa kwa sasa litatokea, mtu atakuwa amejitayarisha kwa njia fulani, badala ya kusubiri majanga kutokea kisha kuanza kulilia serikali.

Jambo kuu ambalo wananchi wanafaa kufahamu ni kuwa wakati mwingi, serikali itaingilia kati wakiwa tayari wameathiriwa kwa kupoteza mali, kuumia ama wapendwa wao kufa, na kuwa mara nyingi itakuja kuokoa tu, wala si kuzuia.

Hivyo basi, ni vyema kwetu sote kuchukulia usalama wetu kama jukumu letu wenyewe, wala si la serikali, kwani walio katika hatari ya kuathiriwa na majanga yanapotokea ni sisi, wala si serikali.

Ni watoto wetu wanaokatiziwa masomo wakiepuka vifo, mashamba yetu kuharibiwa ama wapendwa wetu kufariki.

You can share this post!

TAHARIRI: Majengo kuanguka ni tunda la ufisadi

MUTUA: Sekta ya afya nchini iige yafanywayo ughaibuni

adminleo