• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
PATASHIKA: Manchester City yaalika majirani Manchester United

PATASHIKA: Manchester City yaalika majirani Manchester United

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KIVUMBI kinatarajiwa katika gozi la 179 la Manchester wakati majirani City na United wataumiza nyasi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Etihad hii leo Jumamosi.

Kila mmoja ataingia katika mechi hii akiwa amejaa motisha wa kushinda mechi zao za katikati ya wiki.

Mabingwa watetezi City walizaba Burnley 4-1 siku chache baada ya kutoka 2-2 dhidi ya Newcastle. Nao United wakalima Tottenham Hotspur ya kocha wao wa zamani Jose Mourinho mabao 2-1, baada ya kukabwa na Sheffield United (3-3) na Aston Villa (2-2).

City ya kocha Pep Guardiola ilionyesha makali yaliyoifanya kutawala misimu miwili iliyopita huku Gabriel Jesus akijitwika majukumu ya kuongoza klabu yake kuzoa alama zote tatu dhidi ya Burnley, wakati Sergio Aguero yuko mkekani.

City itaanza mechi hii ikijivunia kuwa na rekodi nzuri. Imepoteza mara moja pekee katika mechi sita zilizopita za ligi dhidi ya United tangu Guradiola achukue usukani mnamo 2016.

Rekodi ya City uwanjani Etihad itawatia moyo vijana wa Guardiola. Imeshinda mechi 23 na kupoteza mara moja katika mechi 26 zilizopita za mashindano yote mwaka huu 2019. Katika Ligi Kuu pekee, City imetumia uwanja wake wa nyumbani vyema kwa kuzoa ushindi 24 katika mechi 27 zilizopita.

Hata hivyo, vijana wa Guardiola wataingia mchuano wa leo na presha kali ya kushinda ili kuweka hai ndoto ya kufikia viongozi Liverpool, katika vita vya kuwania taji la EPL.

Wasiwasi mwingine wa City ni kuwa tayari imedondosha alama nyingi mbele ya mashabiki wake kuliko msimu wote uliopita. Pia, City haijashinda mechi mbili zikifuatana tangu mwezi Novemba uanze. Vilevile, City haijafaulu kulinda nyavu zake zisichanwe katika mechi sita kati ya saba zilizopita.

Kwa upande wao, United ilihitaji sana ushindi dhidi ya Tottenham ili kumuondolea presha kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Katika mechi hiyo, “mashetani wekundu” United walimtegemea sana Marcus Rashford kupata magoli. Mwingereza huyo alipachika mabao yote mawili dhidi ya Tottenham na kufikisha idadi ya magoli ambayo amefungia klabu na nchi yake msimu huu, kuwa 12 katika mechi 13.

City, ambayo ilipiga United 3-1 uwanjani Etihad na 2-0 uwanjani Old Trafford msimu uliopita, inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 32. Iko alama 11 mbele ya nambari sita United.

Baadhi ya nyota wanaotarajiwa kunogesha mchuano huu ni David Silva, Kevin De Bruyne, Jesus, Raheem Sterling na Riyad Mahrez (City) na Rashford na Andreas Pereira. Paul Pogba na Anthony Martial wamekuwa wakiuguza majeraha, ingawa wanaweza kurejea ulingoni ikiwa watakuwa fiti. City itakuwa bila washambuliaji matata Aguero na Leroy Sane ambao wako mkekani.

Mabingwa City huenda wakajipata alama 14 nyuma ya Liverpool watakapoingia uwanjani ikiwa vijana wa Jurgen Klopp wataendeleza ukatili dhidi ya Bournemouth mapema leo Jumamosi.

  • Tags

You can share this post!

Drama Sonko akitiwa ndani

MAKALA MAALUM: Malipo duni ni miongoni mwa masaibu mengi...

adminleo