• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
MWANAMKE MWELEDI: Alikuwa malkia wa amani na mtatuzi mahiri wa migogoro

MWANAMKE MWELEDI: Alikuwa malkia wa amani na mtatuzi mahiri wa migogoro

Na KEYB

KWA miaka 15 alijulikana kutokana na jitihada zake za uanaharakati na vita dhidi ya ghasia za kiukoo.

Bi Dekha Ibrahim Abdi, mwanaharakati ambaye alifanya kazi kama mshauri wa serikali kadha wa kadha, vilevile mashirika ya kijamii.

Ni kazi ambayo ilimtambulisha kimataifa na kumshindia heshima.

Penzi lake hasa lilikuwa katika masuala ya elimu ya jamii ya wafugaji ambapo alifanya kazi kuimarisha elimu kwa jamii za kuhamahama. Lakini azma yake ya kujihusisha vilivyo na masuala ya kusuluhisha ghasia katika jamii za kuhamahama ilianza alipokumbana kwa mara ya kwanza na vita, suala lililounda msingi wa shughuli zake za kudumisha amani.

Ilikuwa miaka ya tisini ambapo wakati huo alikuwa mwalimu eneo la Wajir. Vita vya kimbari vilipochipuka huku vikichochewa na maji na mifugo. Ghasia hizi zilisababisha vifo vya watu 1,500.

Mwaka wa 1993 Bi Abdi aliungana na wanawake wengine watatu na kubuni mkakati wa upatanishi ili kusuluhisha tatizo hilo, licha ya kupata pingamizi kutoka kwa viongozi vijijini.

Kwa kawaida wangesikia masaibu ya wahusika, kisha kuyaangazia na kufikia maelewano. Ili kufuatilia suala hili walianzisha Kamati ya Wajir Peace and Development Committee ili kuthibitisha amani.

Mwaka wa 1998, Bi Abdi alijiunga na Responding to Conflict, shirika lisilo la kiserikali lililokuwa na makao yake katika chuo cha Woodbrooke College, Birmingham, nchini Uingereza.

Aidha, alikuwa mwanachama wa bodi ya Co-existence International, na mwanachama mwanzilishi wa Worldwide Peace Practitioners’ Network, Action for Conflict Transformation (ACTION).

Mwaka wa 2000, alijumuishwa katika warsha za kimaendeleo za Idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa, iliyonuiwa kusaidia serikali za mataifa yaliyo Kusini mwa jangwa la Sahara, katika jitihada zao za kutatua migogoro.

Pia alihudumu kama mdhamini wa mashirika ya Coalition for Peace in Africa (COPA), na Peace and Reconciliation Oasis (PRO). Pia, alikuwa mwanachama wa bodi ya Berghof Centre nchini Germany.

Mwaka wa 2002, Bi Abdi alikuwa mlinzi wa Peace Direct, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake jijini London, Uingereza. Baada ya shambulizi la mabomu jijini London mwaka wa 2005, alisaidia kuzindua mradi wa Young Muslims ili kutambua changamoto za kuwa Muislamu, na wakati huo huo raia wa Uingereza.

Aidha, Bi Abdi pia alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Centre for Peace and Conflict Studies nchini Cambodia, taasisi inayoimarisha amani barani Asia.

Mbali na hayo, alihudumu kama mkufunzi mshauri wa kudumisha amani miongoni mwa jamii za kuhamahama katika mataifa kadhaa.

Pia, aliandika kuhusu masuala ya amani na utatuzi wa migogoro na kuchangia uandishi wa vitabu na mawasilisho katika masuala hayo hayo.

Nchini Kenya, Bi Abdi alifanya kazi kama mshauri wa serikali katika masuala ya upatanishi, na mwaka wa 1999 alipewa tuzo ya Distinguished Medal of Service. Wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 na mapema 2008, machafuzi yaliyotetemesha Kenya, Bi Abdi aliitwa kusaidia kukomesha ghasia hizo.

Mbinu yake ya ukusanyaji data wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi, Ushahidi, ilitumika kama jukwaa la kukusanya habari wakati wa ghasia. Pamoja na wengine wanne, walianzisha Concerned Citizens for Peace (CCP), jukwaa lililojihusisha na shughuli za kukomesha ghasia wakati wa vita hivi.

Kikundi hiki kilifanya kazi na raia, machansela wa vyuo vikuu, mashirika ya mawasiliano na vikundi vya mashirika ya kijamii, miongoni mwa majukwaa mengine ili kutambua sehemu zilizokumbwa na ghasia ili kuingilia kati.

Kama mwanaharakati wa amani, Bi Abdi ametambuliwa na kupokea tuzo mbali mbali. Mwaka wa 2002, alikuwa mlinzi wa shirika lisilo la kiserikali la Peace Direct, lenye makao yake jijini London nchini Uingereza.

Mwaka wa 2005 alipewa tuzo ya mleta amani wa mwaka nchini, Kenya Peace Builder of the Year, mbali na kuteuliwa katika tuzo ya amani ya Nobel Peace Prize ambapo alijumuisha kikundi cha wanawake 1,000 waliojihusisha na shughuli za kuleta amani duniani kote.

Mwaka wa 2007 alipewa tuzo ya Right Livelihood Award, ambayo mara nyingi huchukuliwa kuwa tuzo mbadala ya ile ya amani ya Nobel. Alitumia pesa alizopokea kama zawadi kuanzisha chuo kikuu cha Peace University eneo la Wajir. Aidha mwaka wa 2009 alipewa tuzo ya German Hessian Peace Prize.

Kabla ya kifo chake mwaka wa 2011 katika ajali mbaya ya barabarani ambayo pia ilisababisha kifo cha mumewe, Bi Abdi alikuwa akiendesha shughuli zake mjini Mombasa, kuendesha miradi ya kuleta amani na hata kuanzisha kituo cha amani cha Oasis of Peace Centre.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Kisomo cha mpenzi wangu kinanitia kiwewe

AKILIMALI: Mkulima anavyofaidi kutokana na ukuzaji na...

adminleo