• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
JAMVI: Odinga na Ruto wanavyoyumbisha umoja wa Mulembe

JAMVI: Odinga na Ruto wanavyoyumbisha umoja wa Mulembe

Na BENSON MATHEKA

Umaarufu wa kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga eneo la Magharibi, na mikakati ya Naibu Rais William Ruto ya kupenya eneo hilo, huenda ikayumbisha juhudi za kuunganisha jamii ya Waluhya.

Tayari vigogo wa kisiasa katika jamii ya hiyo wanalaumu Bw Odinga na Bw Ruto kwa kutatiza juhudi za kuunganisha vyama vya kisiasa vya Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya ili kufanikisha umoja wa jamii ya Waluhya.

Wadadisi wanaonya kuwa juhudi hizo zinaelekea kugonga mwamba kufuatia upenyo wa Naibu Rais William Ruto eneo la Magharibi na umaarufu wa Bw Odinga.

Wiki jana, kiongozi wa chama cha Ford Kenya, Moses Wetangula alilaumu wanachama wa ODM eneo la Magharibi kwa kuvuruga umoja wa Waluhya.

Kulingana na Bw Wetangula, wafuasi wa ODM eneo hilo wamekuwa wakihakikisha jamii hiyo haiungani.

Wadadisi wanasema kwamba sio siri Bw Odinga ana wafuasi wengi eneo hilo kuliko Bw Wetangula na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na ameweka mikakati kuhakikisha kuwa litabaki ngome yake ya kisiasa.

“Madai ya Wetangula yanatokana na ukweli kuwa vigogo wa kisiasa wa jamii hiyo hawajaweza kuyeyusha umaarufu wa ODM katika eneo lao. Viongozi wengi waliochaguliwa wanatoka ODM na Bw Odinga amehakikisha limewakilishwa katika usimamizi wa chama ili kukinga maslahi yake,” asema Bw Eliud Sanga, mdadisi wa siasa.

Anasema Bw Odinga ana vibaraka wake katika jamii ya Waluhya akiwemo Naibu Kiongozi wa chama Wycliffe Oparanya na Katibu Mkuu

Edwin Sifuna.

“Bw Odinga amepenya katika chama cha Bw Mudavadi na kunyakua wanachama wenye ushawishi kama seneta wa Kakamega Cleopas Malala na mbunge wa kuteuliwa Godfrey Otsosi miongoni mwa mikakati mingine,” aeleza.

Anasema mikakati ya Bw Odinga na Bw Ruto na ukosefu wa nia njema miongoni mwa viongozi wa eneo la Magharibi kumesambaratisha mpango wa kuunganisha vyama hivyo vya kisiasa ili kuwa na mgombeaji mmoja wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mwaka jana, Bw Mudavadi alitofautiana na Bw Wetangula ambaye ilisemekana alinuia kuungana na Bw Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakati huo Bw Mudavadi alisema kumuunga Bw Ruto ni sawa na kuungana na mpinzani wao mkuu kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Mudavadi na Bw Wetangula wametangaza nia ya kuwania urais, sawa na gavana wa Kakamega Wycliff Oparanya na waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa.

Lengo la kuunganisha vyama vyao ilikuwa ni kuleta pamoja jamii ya Waluhya iliyo na zaidi ya kura 6 milioni ili iweze kuzungumza kwa sauti moja kisiasa.

“Lakini hali ilivyo sasa, ni wazi kwamba baadhi ya viongozi hao hawakuwa nia njema katika mpango wa kuunganisha vyama vya kisiasa. Hatua hiyo ingefanikisha umoja wa jamii ya Waluhya ambayo kwa miaka mingi imekuwa imegawanyika kisiasa.

“Wametangaza hadharani kwamba hawataki kuunga mmoja wao kuwa rais 2022 kwa kumuidhinisha Bw Ruto. Kutokana na hali hii itakuwa vigumu eneo hilo kutoa rais,” alisema mchanganuzi wa siasa David Ouma.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale alihamia kambi ya Dkt Ruto na kutangaza kuwa ndiye anayefaa kuwa rais huku Bw Mudavadi akisisitiza kuwa jina lake litakuwa kwenye debe.

Bw Sanga anasema ingawa mwanzoni mpango huo ulionekana kuendelea vyema, baadhi ya viongozi waliangukia mitengo ya Bw Ruto na Bw Odinga ya kugawanya eneo hilo wakilenga maslahi yao ya kibinafsi.

“Ndoano ya Bw Ruto eneo hilo na ujanja wa kisiasa wa Bw Odinga zimenasa wanasiasa kadhaa. Baadhi ya viongozi wameahidi kuwaunga mkono. Hii imekuwa pigo kwa juhudi za kuunganisha vyama vya ANC na Ford Kenya. Kwa ufupi juhudi zao zimekuwa sumu kwa muungano uliopangwa wa jamii ya Waluhya,” asema Bw Ouma.

Mwishoni mwa mwaka jana, Bw Khalwale alitangaza kubuniwa kwa chama kipya cha kisiasa cha All Kenyans Alliance (AKA) ambacho alisema watatumia kupigia debe mgombeaji wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Katika hatua ambayo ilikwaza Bw Mudavadi na wanachama wa ANC, Bw Khalwale alisema chama hicho sio cha Waluhya pekee.

“Utakuwa mzaha iwapo tutavunja vyama vyetu vya kisiasa kwa lengo la kuunganisha jamii ya Waluhya kisha tumuunge Bw Ruto ambaye tunashindana naye. Ninajua Bw Wetangula anafahamu vyema kwamba hatuwezi kujipanga kumuunga mtu tunayeshindana naye,” alisema Bw Mudavadi.

Lakini wiki jana, Bw Wetangula alisema ni wanachama wa ODM ambao wanakwaza juhudi za kuunganisha Waluhya. Seneta huyo wa Bungoma alisema ODM imekuwa ikitumia jamii ya Mulembe kisiasa na kuitupa.

Wadadisi wanasema kwamba kabla ya viongozi wa Ford Kenya kuengemea upande wa Bw Ruto na ODM kuzua uhasama wa ndani ya ANC, juhudi za kuunganisha vyama vya jamii ya Waluhya zilikuwa zikiendelea vyema.

Bw Sanga anasema Bw Odinga hawezi kukubali jamii hiyo kuungana kwa sababu itakuwa pigo kwake kisiasa. Anasema hata Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli ambaye amekuwa akipigania umoja wa jamii hiyo ni mwandani mkubwa wa Bw Odinga.

You can share this post!

Kalameni aoa wake wengi ili asifiwe

JAMVI: Ruto atakavyonufaika kwa BBI ikipitishwa

adminleo