• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
INDINDI: Rais atuonyeshe mfano bora katika kuthamini Kiswahili

INDINDI: Rais atuonyeshe mfano bora katika kuthamini Kiswahili

NA HENRY INDINDI 

TUNAPOKARIBIA kuufunga mwaka huu, ninatamani kutangaza matumaini yangu katika mwaka ujao. Ninatamani sana kuwa na matumaini kwamba mwaka huo ujao, tutaweza kuwa na Baraza la Kiswahili nchini.

Ninatumai pia kumwona Rais akijitokeza kama mfano bora kwenye usiku wa kuamkia mpya atakapoitoa hotuba yake.

Yaani akiitoa hotuba yake katika Kiswahili na atuahidi kwamba hotuba zake za tangu hapo katika hafla za kitaifa atazitoa katika Kiswahili basi nami pamoja na walezi wenzangu wa Kiswahili tutafurahi sana.

Lakini hayo ni matamanio na matumaini tu. Watekelezaji ni tofauti na sisi na huenda hawaishi katika ulimwengu wetu wakayaona mambo kwa jinsi tunavyoyaona sisi.

Inasikitisha kwamba katika siku zote hizi tulizojitahidi kulikumbusha taifa hili kuhusu utaifa na majukumu yanayotuhitaji kitaifa, bado viongozi wetu wanatumia lugha za kigeni katika hafla za kitaifa. Katika sikukuu ya majuzi ya Jamhuri, Rais aliamua kusiwe na hata harufu ya kisawasawa ya Kiswahili kwenye hotuba.

Yaani hata ile ya mbali iliyozoeleka baada ya kuisoma hotuba yake rasmi, haikuwa. Ilikuwa sikukuu ya taifa ambayo viongozi wa taifa walihiari kuifanya lugha ya kigeni kuwa na uwezo mkubwa sana wa kutekeleza majukumu ya kitaifa.

Sijui ni kwa nini viongozi wetu hawakujifunza chochote kutokana na uchangamfu wa wananchi waliohudhuria uzinduzi wa ripoti ya Hatua ya Kuwaunganisha Wakenya (BBI) kutokana na Waziri Palamagamba wa Tanzania kutumia Kiswahili katika hotuba yake!

Ukweli ni kwamba asilimia kubwa ya wananchi wa Kenya hukitumia Kiswahili iwe yawe tu kwa kutoona lugha hii ikitiliwa maanani na viongozi wao.

Wanapokosa kuwaona viongozi wao wakiitilia maanani na kuizungumza kwa mapenzi sawa na wanavyofanya viongozi wenzao kutoka Tanzania, wananchi hawa wanakata tamaa kuihusu lugha hii hivyo basi hawaipi thamani na uzito unaostahili kwa amali hii muhimu ya kitaifa.

Hapa ndipo panapostahili kushonwa kwa sababu pameraruka na pakaurarua utaifa wetu. Na pengine hii ni sehemu ya ujinga wetu wananchi msanii King Kaka alisahau kututajia katika shairi lake la kikariri maarufu kama ‘Wajinga Nyinyi’.

Rais angeitoa hotuba yake katika Kiswahili kisha aifikie kauli aliyoisisitiza sana ya mgongano wa maslahi na kutuuliza kuhusu ‘conflict of interest’ inavyoitwa katika Kiswahili wanataaluma wa Kiswahili wangehamasika kuipata tafsiri yake papo hapo.

Pengine atakapoanza kutoa hotuba zake katika Kiswahili, walezi, wataalamu na wanataaluma wa Kiswahili watakuwa sehemu ya kikosi anachoambatana nacho katika safari na hafla za mara kwa mara.

Tafsiri ambayo angepewa na aitangaze hapo, hatimaye ndiyo ambayo ingeishia kuwa maarufu kuwakilisha maneno haya ya Kiingereza. Lakini hilo halikufanyika kwa hivyo sisi shibe yetu ibaki ile ya matumaini.

Tutaendelea kuwa na matumaini kwamba siku moja atatuonesha mfano bora wa kuiga kuhusu amali hii muhimu ya kitaifa. Kwa kuwa tayari Rais alikwishaonesha nia ya kuthamini Kiswahili kwa kuwateua wasemaji wa serikali wanaoonea fahari uzungumzaji wa Kiswahili bora kama Ndg. Oguna na Bi Kanze Dena, hatua iliyobaki ni ya kuanza kutoa hotuba zake katika Kiswahili.

You can share this post!

NGILA: Data itumike kwa pamoja kufaidi kila mshikadau

MATUNDURA: Athari za sera ya udhibiti kwa waandishi wa...

adminleo