OBARA: Agizo la Rais kuhusu wabunge mawakili lilijaa unafiki

Na VALENTINE OBARA

AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta kwamba sheria zipitishwe kuzuia wabunge na maseneta kufanya kazi za uwakili si la uaminifu kwa umma.

Agizo hilo lilitokana na jinsi maseneta walivyoamua kumwakilisha Gavana wa Nairobi Mike Sonko katika kesi yake ya madai ya ufujaji wa pesa za umma.

Singependa kujadili zaidi hatua hiyo ya maseneta bali msimamo uliotolewa na Rais ulivyojaa unafiki.Sina imani kwamba Rais alipojitokeza wazi kulaani wabunge na maseneta akidai si haki wanapowakilisha washukiwa kortini ilhali wanapaswa kuwa watetezi wa umma, alikuwa akifanya hivyo kwa kujali maslahi ya wananchi.

Ikiwa kweli Rais angekuwa anajali maisha ya umma, hili ni suala ambalo lingeibuka zamani, na hata si kuhusu wabunge na maseneta ambao ni mawakili. Haki za umma zimekandamizwa sana katika sekta muhimu wanazotegemea maishani kila siku.

Watu wanaobuni sera ndio wale wale wanaoshikilia usukani kupitia kwa mashirika ya kibinafsi katika uendeshaji wa sekta hizo kitaifa.

Ukitazama sekta ya kilimo, utakuta wawekezaji wakubwa wa kibinafsi ni wanasiasa na wandani wao walio na ushawishi kuhusu namna ambavyo sekta hii inastahili kuendeshwa.

Bila shaka, kumekuwa na matatizo chungu nzima katika kilimo kama vile cha miwa na mahindi kwa sababu ya sera duni ambazo zinafaidi sana wafanyabiashara wanaoagiza sukari na mahindi kutoka mataifa ya kigeni kwa bei ya chini na kumwacha mkulima akiwa fukara.

Zaidi ya hayo, hawajali kuhusu jinsi bidhaa kama vile maziwa na mayai ambazo ubora wao ni wa kutiliwa shaka, huletwa kutoka nchi za nje kwa bei rahisi na kuumiza wafugaji wetu.Katika sekta ya uchukuzi wa umma, juhudi za serikali kuweka magari au treni za usafiri mijini hugonga mwamba mara kwa mara.

Sababu si kuwa serikali haina uwezo, bali watu wanaotegemewa kubuni na kupitisha sera zitakazohitajika kwa mipango hii wana ushawishi wa kutosha kukwamisha juhudi hizo.

Hii ni kwa kuwa, serikali ikileta magari ya uchukuzi yatanyima faida watu hao ambao hudhulumu wananchi kwa kulipisha nauli za juu kupita kiasi.Masaibu ya raia hayaishii hapo.

Katika sekta ya afya, huwa tunapokea malalamishi mara kwa mara kutoka kwa wananchi ambao hulazimishwa kuendea huduma zaidi za matibabu au kununua dawa kutoka kwa hospitali za kibinafsi.

Ingawa serikali kuu na za kaunti zimejitahidi kuweka vifaa vya kisasa na dawa katika hospitali na zahanati za umma, kuna madaktari katika hospitali hizo ambao hutaka wagonjwa wapeleke pesa kwa hospitali zao za kibinafsi.

Ikiwa kweli Rais anamjali mwananchi wa kawaida, ajitokeze wazi sio kuagiza tu bali kuhakikisha kuna sheria zitakazopitishwa na kutekelezwa kuokoa raia dhidi ya dhuluma katika sekta hizo muhimu zaidi.