WANDERI: Kibao #WashenziNyinyi chafaa kuibua mjadala wenye faida
Na WANDERI KAMAU
MOJAWAPO ya wanamuziki ambao watakumbukwa sana katika historia ni marehemu Bob Marley kutoka Jamaica.
Marley alisifika sana katika miaka ya sitini na sabini kutokana na nyimbo zake ambazo ziliyahimiza mataifa ya Ulaya kuzipa nchi za Afrika uhuru.
Nyimbo zake kwa mtindo wa reggae kama “Africa Unite”, “Zimbabwe”, “Babylon System” kati ya zingine zilijenga mwamko wa kipekee katika nchi za Kiafrika.
Mwamko huo ndio ulikuwa mojawapo ya misukumo mikuu iliyowafanya Waafrika kuzinduka na kuanza harakati za kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni bila kuogopa chochote.
Waafrika walibuni vyama mbalimbali vya kitaifa na maeneo ambavyo vilihimiza umoja na uzalendo miongoni mwao ili kuwawezesha kukabiliana na dhuluma, ukatili na unyama wa wakoloni.
Cha kushangaza ni kuwa, Marley hakuwa shujaa miongoni mwa Waafrika pekee, mbali kwa kila Mtu Mweusi. Hii ni kwa kuwa nchini mwake, mlikuwemo na Waafrika waliokuwa wametekwa na kusafirishwa katika mataifa mbalimbali Amerika Kaskazini ambako walihudumu kama watumwa.
Mwanamuziki huyo aliwazindua wanamuziki wengine kama Peter Tosh, Joseph Hill, Israel Vibrations, Lucky Dube kati ya wengine wengi ambao walikita utunzi wao katika kuzihamasisha nchi za Magharibi kuwapa Waafrika uhuru wao.
Utunzi wa Marley pia unaelezwa kuwateka baadhi ya wanaharakati miongoni mwa wazungu, ambapo wao wenyewe waliungana na Waafrika kuitisha uhuru wao.
Baadhi ya wanaharakati wazungu wanaoelezwa kutekwa na utunzi wa Marley ni Thomas Clarkson na William Wilberforce kutoka Uingereza.
Kijumla, urejeleo huu unadhihirisha kuwa sanaa, hasa muziki, una nguvu sana katika kushinikiza mageuzi ya kijamii.
Kauli hii inafuatia msisimko wa aina yake ambao umekuwepo nchini kufuatia wimbo “Wajinga Nyinyi” aliotoa mwanamuziki Kennedy Ombima, maarufu kama King Kaka.
Kwenye wimbo huo, mwanamuziki huyo anatumia kauli nzito kuwakashifu wananchi na viongozi wanaochaguliwa kutokana na changamoto zinazoikumba nchi.
Katika hatua inayoonyesha ujasiri wa kipekee, anawataja baadhi ya viongozi ambao wamehusishwa na sakata za awali za ufisadi.
Ni wimbo ambao umezua mjadala na hisia mbalimbali, lakini swali kuu ni ikiwa kibao hicho kinaweza kuzua ghadhabu kiasi cha kuwafanya wananchi kuanza harakati za kuleta mageuzi ya kiutawala bila kuogopa.
Kwa utathmini wa kina, utunzi kama huo si wa kwanza. Kuna wanamuziki, wanaharakati na waandishi wengi ambao wametunga nyimbo na kuandika vitabu kushinikiza mageuzi ya kisiasa nchini.
Baadhi ya wasanii hao ni Eric Wainaina, ambaye alitunga kibao “Nchi ya Kitu Kidogo” kuukashifu utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi.
Waandishi kama Ngugi wa Thiong’o pia walifungwa gerezani na baadaye kutoroka nchini kwa kuandika kitabu “Caitaani Mutharaba-ini” (Shetani Msalabani) kuukashifu utawala wa Mzee Jomo Kenyatta mnamo 1977.
Wimbo huu wafaa kuzua mjadala wa jinsi ya kumaliza maovu mengi nchini.