Makala

DINI: Uwe baraka kwa wengine msimu huu jinsi Mungu alivyomtoa Yesu

December 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Tunapojiandaa kusherehekea Krismasi, ni muhimu kutosahau maana kamili ya siku hii.

Hii ni siku inayotukumbusha zawadi kuu zaidi iliyowahi kutolewa duniani. Zawadi hii ilitolewa na Mungu mwenyewe. Mungu alipotaka wana, alimtoa mwana.

Huu ni wakati mwafaka wa kujiuliza ni nini unachoweza kutoa ili kuwa baraka kwa mtu mwingine.

Jiulize kama umeishi maisha ya ukarimu au maisha ya ubinafsi? Katika kutoa kwako, umekuwa wa baraka ama umetoa machukizo.

Kila mtu duniani hutoa, lakini wengine hutoa mazuri huku wengine wakitoa mabaya. Kila toleo huwa na matokeo. Ukitoa mabaya, hatimaye utapokea mabaya.

Mungu alitoa kilicho kizuri zaidi -Wokovu kupitia kwa Kristo. Wokovu umepatikana kwetu kwa sababu Mungu alikubali kumpoteza mwanawe.

Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa. Tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa Ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. (Isaya 9:6).

Yesu kwetu ni rafiki. Wakati watu wengine wanapokudharau na kukuacha kwa sababu ya yale unayopitia, Yesu anafungua mikono yake tayari kukukumbatia kwa upendo.

Aliacha utukufu wake kwa ajili yetu. Wafilipi 2:2-8 yasema hivi, “Ijalizeni furaha yangu, ili muwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja na nia moja. Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

Kuweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Yesu kwetu ni mshauri wa ajabu, ni Mungu anayewaongoza watu wake. Wakati huu wa Krismasi kumbuka Mungu anataka kuhusika katika maamuzi unayofanya maishani mwako.

Ukiwa na Mungu utafika salama. Mtumainie Mungu kukuelekeza katika mambo yote unayofanya na utafanikiwa sana. Katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako (Mithali 3:6).

Yesu kwetu ni Mungu mkuu. Ana uwezo wa kutulinda kutokana na silaha za yule mwovu.

Tukimtumainia Yesu, hatustahili kuogopa chochote maana atatutetea.

Hata kwa mambo magumu unayopitia, yuko pamoja nawe. Hatakupungukia wala kukuacha. Nawe usimwache Bwana. Usijaribu kutembea peke yako.

Mawazo ya wanadamu hupotosha, lakini ukimtumainia Mungu atakusaidia hata katika kuepuka mawazo mabaya yanayoweza kukuweka pabaya. Hata kama tayari kitumbua chako kikiwa kimeingia mchanga, Mungu ana uwezo wa kukunusuru. Yanayoonekana hayawezekani, kwake yanawezekana.

Anaweza kukuinua. Yuaja kutuchukua maana hii dunia sisi tu wapita njia. Je, umejiandaa?

Yesu kwetu ni baba wa milele. Anatupenda kwa upendo usio na kikomo.

Licha ya maovu tunayoyatenda, yuko tayari kutusamehe na kutupa tumaini. Yeye si kama mababa wa duniani ambao wengine ni wema na wengine ni waovu. Yeye habadiliki milele. Yuko pamoja nasi kila wakati.

Yesu kwetu ni mfalme wa Amani. Maisha haya, kuna mambo mengi yanayotutia hofu. Lakini tukiwa na Yesu tunapata Amani. Hatuogopi mabaya maana yu pamoja nasi. Hatuogopi kifo maana alishinda kifo, nasi tuna uhakika wa uzima wa milele.

Si kwa matendo yetu, bali kwa neema kwa kuamini kazi iliyomleta hapa duniani. Akaenda msalabani na siku ya tatu akafufuka ili aaminiye awe na uzima wa milele.

Krismasi hii, itumie kwa kutoa mema popote uendapoa. Kuna zawadi nyingi unayoweza kuwapa wanadamu.

Wape sababu ya kufurahi, wape sababu ya kuwa na matumaini, wasio na vyakula walishe, wasio na mavazi wavishe.

Usiwe mbinafsi. Na ukumbuke zawadi kuu unayoweza kumpa Mungu, ni kumpokea mwanawe Yesu Kristo.