• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Re-Union yahifadhi taji kwa mara ya tatu mfululizo

Re-Union yahifadhi taji kwa mara ya tatu mfululizo

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Re-Union FC ilihifadhi taji la NewFire for Christ (NFC) baada ya kubugiza Lucky Stars magoli 4-0 kwenye mechi iliyopigiwa uwanja wa Goan Institute Pangani, Nairobi.

Re-Union ya kocha, Joseph Milimo iliweka kombe hilo kabatini milele baada ya kutawazwa mabingwa wa kinyang’anyiro hicho mara tatu mfululizo.

Mashindano ya mwaka huu yaliyoshirikisha timu nne yalikuwa makala ya nne ambayo huandaliwa na kufadhiliwa na Kundi la NewFire for Christ (NFC) lenye makazi yake mjini Kitale Kaunti ya Trans-Nzoia.

Bosi wa NFC, Evans Ulwami (kushoto), akiwatuza kocha wa Re-Union, Joseph Milimo (kulia) na nahodha wake, Dickson Gitau Gitahi baada ya kuhifadhi taji la NFC makala ya 2019. Picha/ John Kimwere

Katika mchezo huo, Re-Union ilitandaza soka safi na kufanya wapinzani wao kukosa ujanja. Ilivuna ushindi huo kupitia Dickson Gitau Gitahi (nahodha), Mark Amboka, sajili mpya Felix Ochieng na David Timbe waliotupia kambani bao moja kila mmoja.

”Tunapongeza wachana nyavu wa Re-Union kwa kutandaza soka safi kwenye kampeni za mwaka huu na kufanikiwa kuhifadhi taji hilo,” alisema bosi wa kundi hilo Kenya, Evans Ulwami. Naye mshirikishi wa kundi hilo, David Mugaya alishukuru vijana walioshiriki mechi za mwaka huu na kudokeza kuwa wanatarajia ngarambe ya mwaka ujao itakuwa bora.

Wachezaji wa Terakoya baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye shindano la NFC makala ya 2019. Picha/ John Kimwere

Kadhalika alitoa mwito kwa wahisani wajitokeza kushirikiana na kundi kwenye juhudi za kuhubiri neno la Mungu mashuleni pia kuandaa mashindano ya soka kwa wachezaji chipukizi katika maeneo tofauti nchini.

Re-Union ilitawazwa mabingwa wa ngarambe hiyo baada ya kumaliza kidedea kwa alama alama sita sawa na Terakoya FC tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kwenye utangulizi wa kipute hicho, Re-Union ilikomoa Terakoya mabao 2-1 kabla ya kuzimwa na Ngara United kwa mabao 2-0. Nayo Terakoya United ya nahodha, Edwin Nase na Meshack Godia ilishinda mechi mbili kwa kunasa magoli 3-2 na 2-0 dhidi ya Lucky Stars na Ngara United mtawalia.

Wachezaji wa Re-Union baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye shindano la NFC makala ya 2019. Picha/ John Kimwere

Nayo Ngara United ilimaliza ya tatu kwa alama alama nne, tatu mbele ya Lucky Stars baada ya kulaza Re-Union mabao 2-0 na kutoka sare ya bao 1-1 na Lucky Stars.

Re-Union na Terakoya FC kila moja ilituzwa kombe, jezi na mipira miwili. Ngara United ilipokea kombe na mipira mwili nayo Lucky Stars ilipata mipira miwili. Kadhalika wachezaji wa timu zote kila mmoja alipata cheti cha kushiriki mashindano hayo.

You can share this post!

SHAKA ZULU KIUMBE: Mwanamuziki, mwigizaji na mpishi hodari

Gavana ataka mahari sawa kwa mabinti waliosoma na wasiosoma

adminleo