Polo auza mali kuhama kijiji cha warogi
Na JOHN MUSYOKI
ISINYA, KAJIADO
JAMAA wa hapa alizua kioja alipoamua kuuza mali yake ili ahamie mjini, akisema anahofia kurogwa na watu wasiomtakia mazuri.
Hata hivyo mke wa jamaa alikataa katakata uamuzi wa mumewe.
Juhudi za jamaa huyo za kutaka kuuza mali yake zilizimwa mama watoto alipotisha kumshtaki kwa wazazi na wazee wa kijiji.
Siku ya kioja mke alimkaripia jamaa huyo alipogundua njama yake ya kuuza mali yao, na kumuonya vikali.
“Wewe una sarakasi chungu nzima. Huu mpango wako wa kutaka kuuza mali yetu kamwe hautafua dafu,” akasisitiza mwanadada.
“Unadai watu wanataka kukuroga, lakini kumbe ni wewe umejiroga mwenyewe,” mrembo akaongeza kwa hasira.
Inasemekana licha ya jamaa kuonywa na mke wake, alisimama kidete kutetea uamuzi huo.
“Ukikataa kwenda na mimi mjini utabaki hapa kijijini peke yako. Ukitaka kuolewa tena uko huru. Mimi sitakusaidia kwa chochote kama umeamua kunipuuza,” kalameni akatisha.
Siku iliyofuata mkewe aliita kikao cha wazee kuwapasha mpango wa mumewe kutaka kumtelekeza na kunadi mali yao.
“Ako na vituko vinavyonitisha. Anataka kuuza mali yote na kuhamia mjini. Pia anasema hanipendi. Naomba mnisaidie kwa sababu akijaribu kufanya kitu atakiona cha mtema kuni,” mwanadada aliapa.
Wazee hao walimtafuta polo wakamketisha chini na kumpa kisomo kikali.
Aidha, walitisha kwamba watamfurusha kijijini humo kabla hajauza mali yake.
“Unataka kuuza mali yako uende wapi. Mke wako pia ana haki ya kumiliki mali na haufai kumpuuza wala kudai utamuacha.
“Una mpango gani ama unataka kwenda kujivinjari na vipusa mjini msimu huu wa Krismasi. Hutafaulu hata kidogo katika hiyo njama yako,” mzee mmoja alimkabili jamaa.