Kiini cha ufanisi wa Vihiga Queens
Na JOHN KIMWERE
HAKIKA Vihiga Queens kamwe hawana mzaha kwenye kampeni za Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL).
Warembo hao sasa watahifadhi kombe la ubingwa huo milele baada ya kushinda taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.
Mara ya kwanza vipusa hao waliposhiriki kampeni za msimu wa 2016 walifanikiwa kumaliza nafasi ya pili kwenye jedwali baada ya kulimwa mabao 2-0 na Thika Queens.
Licha ya Thika kutoshinda taji hilo tangia mwaka 2017 inajivunia kuwa kati ya kikosi cha kwanza katika soka ya Kenya kuliweka kombe hilo kabatini ilipolishinda mara tatu mfululizo.
Vihiga ya kocha, Alex Alumira ilitawazwa mabingwa wa kipute cha muhula uliokunja jamvi mapema mwezi huu baada ya kuibuka kileleni kwa kuzoa pointi 79, tisa mbele ya Gaspo Women FC.
Nayo Thika ya kocha, Benta Achieng ilikubali yaishe na kumaliza tatu bora kwa kuzoa alama 66, mbili mbele Trans-Nzoia Falcons. Nao kina dada wa Kisumu All Starlets kwa kutia kapuni alama 46 walimaliza tano bora.
”Licha ya kukabili ushindani mkali mbele ya wapinzani wetu hatimaye tulitimiza azma yetu ya kuhifadhi taji hilo kwa mara ya pili,” alisema kocha wa Vihiga na kuwamiminia sifa vigoli wake kwa ufanisi huo.
Baada ya kushiriki mechi zote 28 Vihiga ilishinda 26, kutoka nguvu sawa mara moja na kudondosha patashika moja.
VITA VYA MABAO
Kwenye kampeni hizo, Vihiga, Gaspo, Thika, Trans-Nzoia Falcons, Kisumu All Starlets na Oserian Ladies zilishusha ushindani wa kufa mtu kwa kufunga mabao mengi.
Malkia hao chini ya nahodha, Mango Enez walicheka na nyavu mara 101 na kunyukwa 9mabao 14. Nazo Gaspo ilifunga (62), Thika (84), Trans-Nzoia (80), Kisumu (66) na Oserian (54).
TEREZA ENGESHA
Kando na Vihiga kutazwa malkia wa kinyang’anyiro hicho inajivunia wachezaji wake watatu kuibuka kati ya wafungaji tano bora.
Tereza Engesha aliibuka kinara wa kutikisa nyavu alipotupia kambani jumla ya magoli 36, manne mbele ya Mercy Airo sawa na Topistar Situma wa Kisumu na Vihiga mtawalia.
Wengine walikuwa Mwanahalima Adams (Thika) na Tumaini Waliaula (Trans-Nzoia) waliofunga mabao 31 na 30 mtawalia.
MUHULA UJAO
Mechi za kipute hicho msimu ujao zinatazamiwa kuteremsha upinzani mkali zitakapojumuisha timu tatu mpya zilizopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza ambazo ni Kahawa Queens, Nakuru West Queens na SEP Oyugis FC.
”Ninaandaa kikosi cha chipukizi tayari kushirki mitifuano ya muhula ujao,” ofisa mkuu wa Thika, Fredrick Chege alisema kabla mechi za kipute hicho kufikia tamati.
Katika mpango mzima hatua ya FKF kuizawadia Vihiga kombe pekee bila tuzo ya pesa haijkupokelewa vizuri na wafuasi wa mchezo huo nchini.