LANGAT: Kiswahili chazidi kupanua mbawa zake barani Afrika
Na PATRICK LANGAT
KUANZIA mwaka ujao, Kiswahili kitaanza kufunzwa rasmi kama somo lisilo la lazima katika shule 90 nchini Afrika Kusini.
Kitakuwa lugha ya kwanza nje ya Afrika Kusini kufunzwa katika nchi ambako Kifaransa, Kijerumani na Kichina ni masomo yasiyo la lazima.
Tayari, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeanza kutumia Kiswahili kama lugha yake rasmi ya nne ya mawasiliano.
Lugha rasmi za mawasiliano ambazo hutumika katika jumuiya hiyo ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.
Lugha hiyo pia itakuwa ya kwanza asili kutoka Afrika kutumika katika shughuli rasmi za jumuiya hiyo.
Kiswahili ndiyo lugha ya Afrika yenye wazungumzaji wengi zaidi, ambapo kwa sasa, watu 100 milioni wanakisiwa kukitumia. Hatua hii inakikweza nje ya Afrika Mashariki, ambako ndiko kitovu chake.
Kwa mfano, mwanamuziki Sho Madjozi, 27, ameiteka tasnia ya burudani nchini Afrika Kusini kwa kishindo kutokana na nyimbo zake ambazo huzitunga kwa Kiswahili.
Mojawapo ya nyimbo hizo ni ‘John Cena’ ambao kufikia sasa umetazamwa mara 7.6 milioni kwenye mtandao ya YouTube huku wimbo ‘Huku’ ukitazamwa mara 6.3 milioni kwenye mtandao huo. Hilo lilimwezesha kuibuka mshindi kwenye kitengo cha Mwanamuziki Mpya Bora Zaidi wa Kitaifa kwenye tuzo za muziki za B.E.T mwaka huu nchini Amerika.
Kwa hatua hiyo, ndiye mwanamuziki wa kwanza mwanamke kushinda katika kitengo hicho nchini Afrika Kusini na mwanamuziki wa nne kutoka taifa hilo.
Mwanamuziki huyo alisomea nchini Tanzania, ambako babake alikuwa akifanya kazi.
Kando na hayo, mwanamuziki maarufu Miriam Makeba alitumia Kiswahili kwenye nyimbo zake ‘Hapo Zamani’ na ‘Malaika.’
Tanzania na Kenya zilipitisha Kiswahili kuwa somo la lazima katika shule za upili mnamo 1986.
Baadhi ya watu katika nchi za Rwanda, Burundi, DR Kongo, Msumbiji, Somalia, Visiwa vya Komoro, Zambia na Malawi wanaizungumza lugha hii.
Mnamo Februari 2017, Bunge la Rwanda liliidhinisha Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha rasmi nchini humo.
Lugha zingine rasmi katika taifa hilo ni Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza.
Mnamo Septemba, Baraza la Mawaziri nchini Uganda liliidhinisha kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili kusaidia kukifanya Kiswahili kama lugha ya pili rasmi kwa ushirikiano na Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC).