• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Kituo cha mafunzo ya soka Nakuru chalenga makuu

Kituo cha mafunzo ya soka Nakuru chalenga makuu

NA RICHARD MAOSI

Watoto kutoka mashinani na mijini wakipatiwa nafasi kuonyesha weledi wao wangali wahanga,wanaweza kuwa watu wa kutegemewa katika nyanja mbalimbali za kimaisha siku za usoni.

Hali ni kama hiyo katika uchezaji soka,mchezo maarufu unaotumika kama chombo cha kuwaunganisha watu kutoka matabaka mbalimbali ulimwenguni bila kujali jinsia,rangi wala dini.

Huu ndio wosia wa Ken Seda mkufunzi wa kikosi cha Nakuru Sports Association (NSA),U-9,U-11,U-13,U-15 na U-17, ambacho ni mwasisi wa chuo cha soka kinacholea vipaji vya watoto wakati wa likizo na baada ya kuhitimisha masomo yao.

Wengi wao wakiwa ni watoto kutoka familia maskini katika mitaa ya mabanda ya Bondeni, Freearea, Rhonda, Pondamali na Shabbab viungani mwa mji wa Nakuru.

Seda anasema alianzisha kikosi hiki mnamo Octoba 2018, ili kuwapatia watoto jukwaa la kutumia talanta zao,badala ya kutumia muda wao mwingi wakitazama filamu wakati wa likizo.

Anasema wazo hili limewasaidia wazazi ,kupata njia mwafaka ya kuwalea watoto wao ili wajiepushe na mihadarati ama uhalifu wangali na umri mdogo,katika hatua ya kujitengenezea maisha.

Aidha alitaka kuhakikisha kuwa watoto kutoka jamii zenye uwezo mdogo, wanatangamana na wale wenye hadhi katika jamii,akiamini kuwa masogora kama vile Victor Wanyama walianzia  kwenye mitaa ya mabanda Muthurwa Nairobi.

Mkufunzi Seda anasema ameridhika na mchango wa wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata mabuti,jezi,nyavu na kushiriki mechi nyingi za kirafiki na za ligi ili kujiweka pazuri wakati wa mapambano.

“Mwenyewe nilipata malezi yangu mitaani wala singependa kizazi cha kesho kupitia chanagamoto kama zetu ndio maana ninashirikiana na wazazi kutoka Rhonda,Kivumbini,Bondeni,Freearea na Shauri yako,”akasema.

Akisema kuwa juhudi zake zimeelekea kutambisha jina la timu ya Nakuru Soccer Academy ndani na nje ya kaunti ya Nakuru, ambapo walipata mafanikio makubwa kwenye mashindano ya Rausha kipaji walipoibukia kuwa bora.

Rausha kipaji ni michuano iliyowaleta watoto kutoka kwenye timu mbalimbali,wenye uwezo tofauti na kutengeneza timu ya pamoja kuwakilisha Bonde la Ufa kwa michuano ya FKF nchini.

Seda anaamini kuwa watoto hupata motisha kila wanapoandikisha matokeo mazuri au kupongezwa wakati wakifanya vizuri, baada ya michuano.

Ni wepesi kuelekezwa kwani wao hujifundisha kwa kuyarekebisha makosa madogo wanayofanya, ili waweze kuwa wabobevu katika ulingo wa kusakata kabumbu safi ya kulipwa.

Anawahimiza wanafunzi na wazazi kutambua kuwa soka inaweza kuwa kazi kama nyinginezo, kwa sababu wengi wamefanikiwa kujikimu kimaisha,kujijengea nyumba za kifahari na kununua magari.

Anaona kuwa kasumba ya wazazi kuwazuia watoto kusakata mpira imepitwa na wakati kwa sababu,nafasi nyingi za ajira siku hizi zimebakia katika ulingo wa kutumia vipaji kama vile kandanda na wakimbiaji.

“Kipaji kinalipa vyema sana muradi mtu akitambue,akipalilie na kukitumia vyema bila shaka ataona matunda yake,” aliongezea.

Nahodha wa Timu ya NSA Marvin Macharia anasema soka imempatia nafasi ya kutumia likizo yake vyema na amekuwa mchezaji bora tangu alipokuwa mdogo.

Aliongezea kuwa soka imemfanya kuwa mchangamfu na anawashauri wachezaji chipukizi kujitenga na mihadarati na badala yake kufanya jambo lenye manufaa litakaloweza kubadilisha maisha yao.

Shabiki huyu wa Manchester City anaamini kuwa siku moja atakuja kucheza soka ya kulipwa katika kiwango cha kimataifa kwani amekuwa miongoni mwa nguzo muhimu kwa timu yake.

Nchini timu ya NSA inashiriki michuano ya ligi ya divisheni ya pili, ambapo vijana hawa chipukizi wamekuwa wakiumiza nyasi kila wanapokumbana na vigogo katika uwanja wa Nakuru Athletics Club kila wikendi.

NSA  ilicharaza Ligi Ndogo FC ya kutoka Nairobi 3-1 katika pambano la awali, ikizingatiwa kuwa weledi wao ligini kani ni timu iliyobuniwa yapata mwaka mmoja uliopita.

Pili walijizatiti na kuilabua timu ya Soccer Talent 1-0,hatimaye walishinda The Walk kabla ya kupepetana na kikosi cha Community 08 ya Nakuru, walipoponyoka na ushindi finyu wa 3-2 katika ngarambe hiyo kali ya kukata na shoka.

 

Marvin anawashauri wachezaji wenzake kujiamini na kujitia motisha kila mara wanapoingia uwanjani kushindana na waelewe kuwa asiyekubali kushindwa sio mshindani.

Hivi sasa NSA wanajiandaa kuboresha miundo msingi ili kufadhili vijana zaidi kutoka mitaani wanaopania kuja kucheza soka siku za mbeleni na kufanya iwe kazi.

Mkufunzi Seda analenga kuwatengenezea wachezaji wake mazingira bora na kuwawekea mikataba itakayowafanya kuwajibikia timu kwa asilimia mia moja, katika hatua ya kuinua ligi ya soka kaunti ya Nakuru,

Anasema kuwa mbali na kucheza mpira timu imekuwa ikijizatiti kuhakikisha vijana wanapata ushauri kutoka kwa wachezaji nguli kupitia mfumo wa Skype.

Wa punde zaidi akiwa ni Victor wanayama ambaye aliwahimiza umuhimu wa kutumia vipaji vyao mbali na kuzingatia masomo yao.

Malengo yao makuu hivi sasa ikiwa ni kusuka kikosi kitakachowakilisha taifa katika mashindano ya ligi ya Supa ama KPL.

You can share this post!

AKILIMALI: Ubunifu wa vyandarua vyeupe unavyoimarisha...

Masaibu ya timu ya Taekwondo kutoka Maai Mahiu

adminleo