• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe wa maziwa eneo la samaki

AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe wa maziwa eneo la samaki

NA SAMMY WAWERU

Maridi, ni kijiji kilichoko mashinani katika Kaunti ya Homa Bay na wakazi wengi wanajishughulisha na kilimo cha miwa na mahindi.

Kikiwa katika mazingira ya Ziwa Victoria, ukuzaji wa viazi vitamu pia umekumbatiwa na kushika kasi. Lakini katika shamba la Mhandisi Joseph O. Makolwal taswira inayokulaki ni tofauti kabisa.

Mhandisi huyo anayefanya kazi Switzerland, Barani Uropa, kama Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Novartis Pharmaceuticals, amewekeza pakubwa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Tunampata katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari 12 na karibu na Shule ya Upili ya Wasichana ya Maridi, wakati wa likizo ya hivi majuzi. Katika lango la shamba lake maarufu kama Williberg Farm, tunakaribishwa na kiunga cha miti aina ya whispering casualina na eucalyptus calmadulensis – blue gum.

Pia katika kiingilio kuna vidimbwi kadhaa vya samaki. Mita chache mbele, mradi mkuu wa ng’ombe wenye kimo cha mita 70 kwa 20 umesitiri ng’ombe 15 wa maziwa, ingawa kwa sasa 10 ndio wanazalisha kinywaji hicho.

Ana ndama saba, watano wakiwa wa kike. Isitoshe, ana fahali wanne japo anasema atawauza hivi karibuni kwa sababu Williberg Farm inalenga uzalishaji wa maziwa pekee.

“Dhana imekuwepo kaunti ya Homa Bay na Nyanza kwa jumla si maeneo bora kwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Huu ukiwa mwaka wangu wa pili, nilianza mradi huu kwa njia ya kujaribu tu na ni wazi dhana hiyo ni potovu. Eneo hili lina hali bora kufuga ng’ombe, hususan wa maziwa, mradi wangu umethibitisha hayo,” anafafanua Mhandisi Makolwal.

Mapema 2018, mkulima huyo anasema aliwekeza zaidi ya Sh4 milioni kwenye mradi huo, kutoka kwa akiba yake. Alihamia ughaibuni, Switzerland 1999.

Utengenezaji wa zizi – makao ya ng’ombe, ulimgharimu takriban laki tano, akidokeza kwa mbao na vikingi vilitoka kiunga chake cha miti.

Alianza kwa ng’ombe watano, gharama yao kuwanunua ikifikia Sh500, 000. Matumizi mengine yalikuwa lishe ya mifugo, leba na matibabu.

Hata hivyo, Bw Makolwal anasema utangulizi haukuwa rahisi kwa kile anataja kama ng’ombe wa hadhi ya chini. “Wengi walikuwa chotara ambao hawapendekezwi vile katika uzalishaji wa maziwa. Wawili pekee ndio walikuwa Friesian,” asema.

Anafafanua kwamba ng’ombe mmoja alikuwa akizalisha chini ya lita saba kwa siku, na akiondoa maziwa ya ndama alisalia na mbili pekee kupeleka sokoni.

Kulingana na wataalamu, ndama hapaswi kunyonya malapulapu ya ng’ombe mama kwa sababu mkulima hajui kiwango anachovuta, ila anapaswa kunyweshwa ili kumpimia. Aidha, anahitaji kiwango cha kati ya lita 4 – 6 kwa siku. Unyweshaji wa maziwa akiwa mdogo, husaidia katika uundaji wa tumbo zote nne za ng’ombe.

Suala la chakula cha hadhi ya chini, dairy feeds, pia lilichangia masaibu aliyopitia. “Nilitumia pesa nyingi kununua chakula cha duka ambapo kingi ni duni na hata bandia; kisichoafikia virutubisho na madini hitajika kwa ng’ombe wa maziwa,” aelezea Mhandisi.

Kwenye orodha ya changamoto zilizomkumba pia ni kupata wafanyakazi walioelewa jinsi ya kulisha mifugo, kudumisha kiwango cha usafi ikiwa ni pamoja na matibabu.

Baada ya kufanya utafiti wa kina uliohusisha kutembelea wafugaji waliobobea eneo la Kati na Bonde la Ufa, mfugaji huyu alishauriwa kuwekeza kwa ng’ombe wanaozaa kwa mara ya kwanza.

Mhandisi Makolwal 39, anasema aliwekeza kwa Friesian na Aryshire, hasa wanaojamiishwa kwa mbegu za kisasa, uhamilishaji (AI).

Awali alikuwa akinunua chakula chote, kuanzia nyasi maalum aina ya silage na hay na chakula cha mifugo cha maduka.

Alipochukua mkondo tofauti, wa kujikuzia nyasi na kujiundia chakula mwenyewe, uzalishaji wa maziwa umeongezeka mara dufu.

“Ishara ya ng’ombe kupata mlo kamilifu ilianza kudhihirika, kupitia ukakamavu na uchangamfu wao. Wanazalisha maziwa kwa wingi na hata kupata lepe la kutosha la usingizi,” anaiambia Akilimali.

Kwa sasa, ng’ombe mmoja huzalisha kati ya lita 15 – 20 kwa siku, wateja wake wakuu wakiwa wanakijiji, shule, hospitali na mikahawa kadhaa Homa Bay. Lita moja anaiuza Sh60, na kulingana na maelezo yake akiondoa gharama ya chakula na kutengeneza, leba na matibabu, hakosi kutia faida kati ya asilimia 15 – 20.

Watalamu wanasema ufugaji wa ng’ombe wa maziwa unafanikishwa na chakula bora; chenye virutubisho na madini faafu. Uchanganyishaji wa mlo, ratio ya chakula maalum cha mifugo, silage, hay na molasses, pia ni vigezo muhimu kuzingatia.

“Chakula cha ng’ombe wa maziwa kinapaswa kuwa na virutubisho na madini yanayofaa. Vyote, vichanganywe sawasawa,” ashauri John Momanyi kutoka Sigma Feeds.

Mdau huyo anaonya kuwa chakula duni huchangia kushuka kwa uzalishaji wa maziwa. Aidha, anasisitizia umuhimu wa molasses katika ratiba ya chakula, akifichua kwamba huwapa ng’ombe motisha kunywa maji kwa wingi. Maji ni kiungo muhimu katika uundaji wa maziwa.

Kwa kujikuzia nyasi, Mhandisi Makolwal anasema amepunguza gharama kwa asilimia 70. Chini ya mradi wa Williberg Farm, ekari nne ni za kukuza nyasi aina ya boma rhodes, brachiria na napier, ambazo ni muhimu katika uongezaji wa maziwa.

Pia hukuza mahindi, ambapo hutumia majani na matawi yake kutengeneza silage. Ana mashine aina ya chaff cutter, inayotumika kusaga majani.

Williberg Farm ina vidimbwi vitano vya samaki, kimoja kikiwa na ukubwa wa mita 20 kwa 25 na kati ya samaki 2, 000 – 2, 500 kila moja. Mkulima huyo hufuga samaki aina ya tilapia na kambare.

Shamba lake lina shimo la maji lenye urefu wa futi 30 alilochimba 2016. Pia husambazia wakazi maji.

Kiunga cha miti kina takriban miti 3, 000 aina ya blue gum na whispering casualina. Kulingana naye ufanisi wake haujajiri kwa njia rahisi ikizingatiwa kuwa anafanya kazi ughaibuni. Huendesha shughuli hiyo kwa njia ya simu, ambapo huzungumza na wafanyakazi wake kila siku; asubuhi kabla ya kuingia ofisini, mchana na jioni.

“Ninawafanyakazi wanne, akiwemo meneja. Nimejifunza kuwa na imani na uaminifu nao. Huhakikisha kila mmoja ameridhika na endapo ana shida au kupitia changamoto zozote zile ninamsaidia kwa hali na mali,” asema mfugaji huyo.

Huweka kumbukumbu za rekodi ya uzalishaji wa maziwa kwa kila ng’ombe, ujamiishaji, siku ya kuzaliwa, miaka, aina ya ng’ombe na rekodi ya matibabu. Ana mshauri wa masuala ya kifedha anayemsaidia katika uhasibu na uwekaji wa rekodi.

You can share this post!

AKILIMALI: Binti mfugaji hodari wa sungura

AKILIMALI: Ufugaji wa kuku faida tele Krismasi

adminleo