MAKALA MAALUM: Mto uliogeuka msambazaji maiti vijijini badala ya kuwafaa wakazi
Na SAMUEL BAYA
KUISHI kando ya mto kwa kawaida huwa baraka kwa wanaofurahia mazingira kama hayo.
Hii ni kwa sababu maji yake hutumika kunyunyiza mashamba, kufua nguo, kupika na kufanya kazi zingine muhimu za kila siku.
Lakini taswira hii ni tofuati kwa wakazi wa kijiji cha Baraka, kinachopakana na Mto Molo, hatua chache tu kutoka kituo cha biashara cha Salgaa, Nakuru.
Badala ya mto huu kuwa baraka kwao, umegeuka kero kubwa. Kuna sababu mbili muhimu; kwanza ni agizo la serikali kwamba wasitumie maji ya mto huo kunyunyizia mashamba yao na pili ni hatua ya maiti zinazobebwa na maji kuletwa kijijini.
Kwa sababu hawawezi kutumia maji hayo kunyunyizia mashamba yao, sasa wamebakia tu na hatua ya kuzoa maiti kila zinapoletwa katika kijiji chao.
Tulipouzuru kijiji hicho majuzi, kando tu na barabara kuu inayoelekea Eldoret kutoka mjini Nakuru, tulikumbana na masaibu ya wakazi hao.
Sauti ya maji makali yakipitia mtoni lakini bila hata tone la uhai kwa mimea katika mashamba jirani ilidhihirisha changamoto hiyo wanayopitia.
Bw Thomas Ledamaa, ambaye ni balozi wa nyumba kumi aliambia ukumbi huu kwamba miezi sita iliyopita, mwanafunzi wa chuo kikuu alifariki alipokuwa akipiga picha aina ya ‘selfie’ kando ya mto huo.
“Nimeishi hapa kwa miaka 10 sasa lakini tuliambiwa na serikali tusitumie maji haya mashambani ila tu kwa matumizi ya nyumbani. Miezi sita iliyopita, kijana mmoja wa mkazi jirani alizama majini alipoanguka akipijiga picha ya selfie.
“Aliangamia baada ya kutumbukia katika maji haya,” akasema Bw Ledamaa.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na visa kadhaa ambapo wakazi wamelazimika kuokota miili ya watu mingine ikiwa imeoza ndani ya mto huo.
“Mara nyengine unaamka asubuhi na kukutana na mwili ukielea majini. Mara nyingi huwa hatujui kama maiti hizi zinatokea maeneo gani ila tunaamini kwamba ni watu ambao labda walifariki katika upande wa juu wa mto Molo kisha baadaye wanaletwa na kasi ya maji katika eneo hili,” akasema Bw Ledamaa.
Kulingana na Bw Peter Gathugo ambaye ni mzee wa kijiji hicho cha Baraka, wao wamejaribu sana kutaka serikali iwaruhusu kutumia maji ya mto huo kuendeleza kilimo ila bila mafanikio yoyote.
“Mimi nilikuja katika kijiji hiki miaka kumi na mmoja iliyopita na hapa tuko na idadi ya watu 300. Shida ya hapa ni kuwa mto huu huleta taka nyingi sana kutoka kwa kampuni zinazomwaga uchafu wao ndani ya mto huu. Mara nyengine unaamka asubuhi na kukumbana na mto wenye harufu kuu,” akasema Bw Gathugo.
Alisisitiza kwamba maelezo pekee ambayo walipewa na serikali wakati wakifika hapo yalikuwa kutumia maji hayo labda kwa kufua tu na shughuli nyingine wala sio kunyunyizia mashamba maji.
“Tunajua kwamba kuna visa vyengine ambapo walevi mara nyengine wanaanguka ndani ya mto, lakini hilo halijafanyika hapa. Ila kile ambacho tunajua ni kuwa kuna maiti ambazo huletwa na maji hadi katika eneo hili. Baadhi huwa hata zimeoza na kubakia mifupa,” akasema.
Mkazi mwengine wa kijiji hicho Bw Joseph Ochieng alisema kuwa jamii imekuwa na kibarua kigumu cha kuopoa miili kutoka mtoni licha ya kutojua imetoka wapi.
“Hivi majuzi mwili wa mwanamume ambao ulikuwa umeanza kuoza uliletwa na maji na kuolea hapa kijijini. Tulishtuka na tunahofia kwamba haya yote yanaweza kutuletea magonjwa endapo hatua mathubuti hazitachukuliwa.
Alisema kuwa mara nyengine wanapojaribu kuweka papipu za kupiga maji kutoka mashambani, mitambo yao huchukuliwa na kuwekwa kando.
“Jambo hili linasikitisha sana na linahitaji kuangaliwa kwa kina. Sasa hatuwezi kutumia mto huu ila umegeuka sasa na kuwa egesho la maiti,” akasema.
Hata hivyo kulingana na Bw Kibet Komen ambaye aliwania ubunge wa eneobunge la Rongai, serikali ilikuwa na sababu ya kuzuia wakazi kutumia mto huo katika shughuli za kilimo.
Hii alisema ni kwa sababu mto huo unatumiwa na wakazi wengi na hivyo basi endapo kila mmoja akianza kuutumia kwa kilimo, maji yake hayatatosha.
“Huo mto husambaza maji kuanzia maeneo ya juu ya Molo hadi kaunti jirani ya Baringo. Kwa hivyo serikali iliwakataza wakazi wote wanaoishi kando ya mto huo dhidi ya kutumia maji yake mashambani. Hata hivyo kwa sababu kunanyesha sana kwa sasa, serikali inafaa kuruhusu wakazi hao kutumia maji hayo bila matatizo yoyote,” akasema Bw Komen.
Naye Bw Stanley Kiptanui ambaye ni mzee wa kueneza amani katika kijiji hicho alisema kuwa wakati wakiletwa kijijini, serikali iliwaambia wasitumia maji hayo kunyunyizia mashamba yao maji.
“Licha ya serikali kutuzuia sisi kutumia maji haya mashambani, hata miti ambayo tunapanda hapa haifai kuwa ile inayotumia maji mengi. Sasa haya yote yakitimia hivi sisi hatuna usemi ila kusubiri maiti ziendelee kuletwa hapa nasi tuendelee kuwambia poplisi waje wakichukua. Moto huu kimsingi unatakikana uwe msaada kwetu badala ya dhiki,” akasema Bw Kiptanui.