• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
KAMAU: Mwongo wa mageuzi duniani waanza 2020

KAMAU: Mwongo wa mageuzi duniani waanza 2020

Na WANDERI KAMAU

IMEBAKI siku moja tu kabla ya mwaka 2019 kukamilika.

Mnamo Jumatano, dunia nzima itakuwa ikisherehekea mwanzo wa mwongo mpya wa 2020 hadi 2030.

Hili ni tukio ambalo litakuwa lenye uzito mkubwa kote duniani. Mwongo huo utakuwa mojawapo ya nyakati zenye umuhimu mkubwa sana katika kizazi cha sasa.

Ni mwongo ambao dunia inatarajia kushuhudia mageuzi makubwa zaidi ya kiteknolojia tangu uumba wake. Ni wakati huu ambapo mfumo wa mawasiliano pia utabadilika pakubwa kutokana na ukuaji wa teknolojia.

Ni dhahiri kuwa uhalisia wa athari za teknolojia katika maisha ya mwanadamu umedhihirika sana hasa mwaka 2019.

Hii ni kwa kuwa kampuni kadhaa zimewafuta watu kazi kutokana na mageuzi ya kiteknolojia.

Kimsingi, uwepo wa teknolojia unamaanisha kuwa baadhi ya majukumu ambayo watu walikuwa wakifanya yaliisha baada ya mashirika hayo kukumbatia matumizi ya teknolojia.

Kwa mujibu wa wadadisi wa masuala ya teknolojia, miongoni mwa mageuzi yatakayoshuhudiwa ni kushuka kwa bei za simu za mkononi, hasa zilizo na uwezo wa kufikia mtandao wa Intaneti.

Mageuzi ya pili yatakayoshuhudiwa ni kushuka kwa ada za mitandao, kwani watu wengi watakaokuwa wakitumia huduma hizo ni vijana, kutoka umri wa miaka 18 na zaidi.

Kimsingi, idadi ya vijana wenye ufahamu wa kisasa kuhusu teknolojia itaongezeka ikilinganishwa na kizazi cha watu wenye umri wa miaka zaidi ya 50. Hili bila shaka litaathiri mwelekeo wa kijamii, kiuchumi na kisiasa kote duniani.

Tumeshuhudia teknolojia ikichangia mageuzi makubwa kiutawala katika nchi kama Hong Kong, Sudan, Lebanon na kwingineko, ambako raia wameandamana kushinikiza mageuzi ya kisiasa kwa kuwasiliana kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, Twitter na Instagram.

Mitandao iyo hiyo ndiyo iliyotajwa kuchangia maasi yaliyotokea katika nchi za Arabuni kama Tunisia, Libya, Misri na Yemen, ambako marais kadhaa waliokuwa wamekwamilia mamlakani walilazimika kung’atuka uongozini kutokana na shinikizo ya waandamanaji.

Shinikizo zizo hizo zimeshuhudiwa katika nchi kama Amerika na Uingereza, ambapo Rais Donald Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wamejipata kwenye njiapanda kuhusu uongozi wao, hilo likichangiwa pakubwa na mitandao ya kijamii.

Katika masuala ya kiuchumi, mashirika mengi yameanza kuelekeza matangazo yao ya kibiashara katika mitandao. Hii ni kwa kuwa mbali na kuwafikia watu wengi, majukwaa kama tovuti yanawatoza bei rahisi ikilinganishwa na njia za kawaida.

Kijamii, asilimia kubwa ya watu wanatumia mitandao hiyo kwa mawasiliano au hata kuendeshea shughuli zao za kila siku.

Uhalisia huu unahitaji kwamba lazima viongozi nchini waanze kubadilisha mielekeo yao ya kisiasa. Hii ni kwa kuwa kizazi na nyakati zilizopo ni tofauti sana na ilivyokuwa katika miaka ya sabini, themanini na tisini.

Serikali pia lazima ipanue na kuwekeza pakubwa katika majukwaa yatakayotoa nafasi kwa upanuzi wa matumizi ya mitandao kwa ustawi wa nchi.

 

[email protected]

You can share this post!

ONYANGO: Wakenya wote washirikishwe katika upanzi wa miti

UDAKU: Ni wazi Neymar anakula bata na Paola

adminleo