Habari

Kundi jipya laibuka kutaka Pwani ijitenge na Kenya

December 31st, 2019 2 min read

Na BRIAN OCHARO

KUNDI jipya limejitokeza Pwani na kuwatia wasiwasi wakazi kwa kurejesha mwito wa eneo hilo kujitenga.

‘Singwaya Government’ limefufua jitihada za Mombasa Republican Council (MRC), kusema ukosefu wa ajira, ubaguzi na ukatili wa polisi kuwa baadhi ya mambo yanayoifanya Pwani kutostahili kuwa sehemu ya Kenya.

Kundi la MRC ambalo baadaye mahakama ilisema si haramu, lilikuwa likiendeleza mwito wa kujiondoa kwa Pwani likitumia kauli mbiu ya “Pwani Si Kenya”.

Sasa kundi la ‘Singwaya Government’ chini ya uongozi wa mzee Paul Mwaro Petro, 87, limeiambia mahakama ya Mombasa kwamba, wamekuwa wakifanya maandamano ya amani ili kilio chao cha kutaka mabadiliko na mapinduzi dhidi ya serikali ya Kenya kisikike.

“Watoto wetu wanakosa kazi na wanaonewa katika maeneo yao ya kazi. Kidogo wanachopata kutokana na vibarua wanazofanya kinachukuliwa na polisi,” akasema Mzee Petro.

Mzee huyo alisema kuwa vijana wametengwa na wamekuwa wakikamatwa na kupokonywa pesa na polisi.

“Polisi huwafuata na kuwanyang’anya fedha walizozifanyia kazi siku hiyo. Vijana wamekuja kwangu mara nyingi wakilalamikia wanayoyapitia mikononi mwa maafisa wa polisi, “Bw Mwaro alimwambia Hakimu Mkuu Mkazi wa Mombasa, Martin Rabera.

Mzee huyo ni kati ya watu 16 ambao Jumatatu walifikishwa mahakamani kwa kutaka jimbo la Pwani lijitenge.

Alifikishwa kortini pamoja na Bw Denis Mui, Simon Katana, Emmanuel Katana, John Mwalimu na watu wengine kumi.

Washukiwa hao walikamatwa walipokuwa wanaandamana na kuwahamasisha wakazi wa Mombasa kuunga mkono wito wao wa pwani kujitenga kutokana na kile walichodai kama ubaguzi na ukosefu wa ajira miongoni mwa wapwani.

Washukiwa hao walikiri mashtaka ya kutaka kuunda serikali mpya, lakini baadaye walibadilisha mawazo yao baada ya korti kuwaonya kuhusu matokeo ya hatua yao ya kukubali mashtaka.

Washukiwa hao wanashtakiwa kwa kuchochea vurugu, ambapo serikali inadai kwamba kikundi hicho kilitaka pwani ijitenge na tayari walikuwa wamechapisha bendera mpya ya “serikali” yao tofauti.

Karatasi ya mashtaka inasema washtakiwa hawa, pamoja na wengine, walichapisha bendera nne yenye maneno ‘Singwaya Government’ bila ruhusa.

Serikali inasema maneno yaliyomo kwenye bendera hizo yalionyesha au kuashiria kuwa washtakiwa walikuwa wameunda serikali yao haramu mbali na ile halali ya Kenya.

Serikali inasema kuwa hatua hiyo, imeifanya jamii katika jimbo hilo kuhofia kwamba kitendo hicho kinaweza kuzuia utekelezaji wa sheria.

Wakijibu mashtaka, washukiwa hawa walisema walikuwa katika harakati za ‘kurejesha tena hali bora ya nchi yao’.

Walipewa dhamana ya Sh100,000 kila mmoja na kesi hiyo itasikilizwa tena Januari 13.