• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:40 AM
NGILA: Blockchain itumiwe kuokoa taaluma ya uanahabari 2020

NGILA: Blockchain itumiwe kuokoa taaluma ya uanahabari 2020

Na FAUSTINE NGILA

TEKNOLOJIA za kisasa zilitawala katika majukwaa ya teknolojia katika mwaka wa 2019, wanadamu wakisaka mbinu mpya za kutatua changamoto mbalimbali.

Mojawapo ya teknolojia hizo ni Blockchain, ambayo huwezesha watumizi kufuatilia kila data katika mtandao wake, huku ikiwafungia nje wadukuzi.

Hivyo, inakuza imani katika sekta au kazi yoyote ile inapotumika.

Sekta ya uanahabari, kwa mfano, imekumbwa na visiki vingi katika mwongo uliopita, kama vile kudidimia kwa mapato, kuchipuka kwa habari feki, mfumo duni wa kulipisha matangazo, wanahabari kukosa malipo kwa baadhi ya makala wanayoandika, miradi ya kuripoti masuala muhimu kukosa ufadhili, wasomaji kukwepa kulipia habari na baadhi ya habari kukosekana kwenye tovuti.

Tunapoingia katika mwaka wa 2020, vyombo vya habari nchini na kimataifa havina budi kuanza kufanyia majaribio teknolojia hii, la sivyo, changamoto hizi zitaongezeka hata maradufu, na kuua maana ya uanahabari katika jamii.

Ili kuzima habari feki, teknolojia hii ina uwezo wa kufuatilia chanzo cha habari, picha au video kwa usahihi, na kuthibitisha iwapo ni kweli au feki, jinsi lifanyavyo gazeti la kimitandao la New York Times.

Nimeshuhudia wanahabari wakikosa kulipwa kwa habari na makala wanayoandika kwa asilimia 100, na hili hutokana na kusahaulika kwa baadhi ya habari, na mwanahabri kuishia kupoteza hela.

Pia, katika vyombo vikubwa vya habari ambapo kuna wanahabari wengi, baadhi yao huwa na majina sawa na wakati mwingi idara ya malipo huishia kumpa mwanahabari mshahara usio wake.

Kusuluhisha haya, blockchain inaweza kutumiwa kumpa kila mfanyakazi utambulisho wa kipekee wa kidijitali ambao utaambatanishwa na kila habari, makala, picha au video inayochapishwa, na kulipwa jasho lake mwishoni mwa mwezi bila kukosea hesabu.

Kupitia sarafu za kidijitali, blockchain ina uwezo wa kusaidia wanahabri kuomba ufadhili wa kuripoti makala na masuala ya kijamii yaliyokosa hela za kusafiri na kuhoji watu katika maeneo ya mbali.

Ili kuongeza mapato ya magazeti, kupitia blockchain, kampuni na mashirika ya kiserikali yanafaa kupewa nafasi kugeuza matangazo yao kuwa makala, na kuyachapisha kwa ada fulani, kwani wasomaji wa kisasa hawapendi kutazama matangazo ya magazetini wala mitandaoni.

Kupandisha imani ya habari, wasomaji wanafaa kupewa uhuru wa kuandika habari zinazowahusu kisha kutoa mchango wao wa kifedha kufadhili magazeti mitandaoni.

Pia, kuwazawidi wasomaji wanaotoa maoni kuhusu habari fulani kutachochea tovuti kusomwa na watu wengi, na kuongeza kipato.

Kwa kuwa mbinu za kale zimepitwa na wakati, blockchain itawafaa wasomaji na wanahabari pakubwa. Hivyo, inafaa kuanza kutumiwa mapema ili kuokoa jahazi la uanahabari ambalo huenda likazama zaidi 2020, tusipochukua hatua.

You can share this post!

WASONGA: Rais Kenyatta, naibu wake waonyeshe maafikiano

TSC kufunza walimu kuhusu CBC, kiwango cha Gredi 4

adminleo