Habari

Msichana jasiri ajitoa mdomoni mwa mamba

January 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na STEPHEN ODUOR

MSICHANA wa umri wa miaka 12 katika Kaunti ya Tana River amezua gumzo mtaani kutokana na kitendo chake cha ujasiri baada ya kujitoa mdomoni mwa mamba, aliyekuwa amemnyaka akiwa anachota maji kando ya mto.

Riziki Mzubaki alikuwa mtoni kuchota maji akiwa ameandamana na mamake wa kambo siku moja kabla ya Krismasi, kisa hicho kilipotokea.

Chifu wa eneo hilo, Bw Iddi Wayu alisema, kisa hicho cha kishujaa kuonyeshwa na mtoto wa umri wake ni jambo la kushangaza sana, kwa kuwa hata wanaume wazima wamewahi kuuawa na mamba.

Ingawa mama wa kambo wa mtoto huyo, Bi Asha Salim hakushuhudia lililotokea wakati huo, anasema alisikia kama kitu kizito kilikuwa kimeangushwa kwenye maji. Pia msichana alikuwa ametoweka.

“Baada ya kujitundika mtungi wangu kichwani, nilianza kumwita msichana huku nikianza kuelekea nyumbani. Ghafla, pakatokea pandikizi la mamba likiwa limemshika mwanangu mdomoni. Alikuwa akipiga kelele za kutaka msaada na kung’ang’ana mdomoni mwa mamba huyo,” akasema Bi Salim.

Kwa mshtuko, alipiga mayowe yaliyowavutia wanakijiji mtoni. Msichana huyo alijaribu kujinusuru kutoka kwenye mdomo wa mamba huyo.

Wanakijiji walibaki kuduwaa, mikono vichwani wakaanza kuomboleza kwa pamoja huku wengine wakitia dua. “Nilishuhudia akivutwa ndani zaidi, nikajua hapa yote yamekwisha, Nishampoteza mwanangu. Nikawa nashindwa nitamwelezaje babake,” akaeleza Bi Salim.

Mamba huyo alimzamisha msichana kwa mara ya pili kwa sekunde chache. Alipoinuka naye kwa mara ya pili, huku mguu mmoja ukiwa mdomoni, msichana huyo alitupa teke lililompata mamba jichoni. Alimtema mtoto huyo kwa maumivu aliyopata.

Waliokuwa wakishuhudia walipomwona msichana ameachiliwa na alikuwa akijibidiisha kufika ufuoni japo kwa unyonge, walijitosa majini wakiwa na silaha na kuogelea kwa upesi. Kwa umbali, mamba alionekana akizama na kuinuka tayari kurejelea kuchukua kitoweo chake, lakini alipoona idadi hiyo ya watu majini imeongezeka, alikata matumaini.

Mtoto huyo alikimbizwa katika hospitali ya Masalani, kaunti ya Garissa, kwa kuwa mguu wake wa kushoto ulikuwa umeng’atwa na kuchanika vibaya.