• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
KINA CHA FIKIRA: Inawezekanaje mwalimu wa Kiswahili kuchukia lugha hii ilhali anaifundisha?

KINA CHA FIKIRA: Inawezekanaje mwalimu wa Kiswahili kuchukia lugha hii ilhali anaifundisha?

Na KEN WALIBORA

SIKU nyingi zimepita bila ya mimi kuzungumza redioni.

Sababu kuu ni kwamba baba yangu hakuwahi kumiliki kituo cha redio wala mimi mwenyewe sijawahi kumiliki kituo cha aina hiyo.

Huwa najidanganya kihambe hambe kwamba uwezo ninao na nia ninayo. Ila kama unavyojua dunia haiendi kwa nia na uwezo tu; kwa mnyonge kupata ni mwenye nguvu kupenda.

Kwa hiyo Jumamosi iliyopita, yaani Jumamosi ya mwisho ya mwaka 2019, nilifarijika aliponipigia simu mtangazaji Geoffrey Mung’ou kunihoji redioni kuhusu hali ya Kiswahili ndani na nje ya Kenya. Nikapata dakika zangu tangu za umaarufu. Hilo la umaarufu wala usilione muhimu sana-wala sikuzote sina nia ya kujizolea umaarufu ingawa mara nyingine hujiambia, kihambe hambe labda, kwamba kwa hili uwezo ninao.

Mungou alinihoji kuhusu maendeleo ya Kiswahili na nini mustakabali wake. Majibu yangu yalilenga mambo makuu nchini Kenya, hasa dalili nzuri kwamba hatimaye huenda litaundwa baraza la Kiswahili la Taifa la Kenya (BAKIKE) ili lishirikiane na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (Kakama) kusukuma mbele utanuzi wa Kiswahili.

Nilisema kwamba Tanzania bara na visiwani kuna angaa mabaraza mawili ya Kiswahili—Bakita na Bakiza. Kile ambacho sikusema ni kwamba mabaraza mawili Tanzania ni laana na baraka kadhalika. Ni jambo zuri maana Kiswahili kinaendelezwa na lakini vilevile baya kwa vile Bakita na Bakiza kila moja linavutia kwake kama mwamba ngoma.

Tanzania bara na Tanzania visiwani wanagombania fito ilhali ujenzi ni wa nyumba moja. Hilo ni kinyume na falsafa yangu kuhusu maendeleo ya Kiswahili, “tunajenga nyumba moja tusipiganie fito.”

Ni matumaini yangu hatimaye baraza litaundwa Kenya, tena moja si mawili au matatu. Likishaundwa tuache kuandikia mate, tumeandikia mate kwa muda mrefu sana. Tumesema sana bila kutenda kwa muda mrefu sana, zaidi ya miongo mitano. Imekuwa miongo mitano ya uongo kwamba Kiswahili ni lugha yetu huku dharau kukielekea ikiwa ndiyo falsafa yetu inayotuandisi.

Ili kuelewa kina cha dharau hii fikiria tamko la mhadhiri mmoja wa fasihi ya Kiswahili (sitamtaja jina wala chuo chake), alilolitamka kwenye kongomano la kimataifa la Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kyambogo, Uganda mapema Disemba mwaka jana. Bila kutetereka, mwalimu huyu wa chuo kikuu alisema kwamba anaichukia sana fasihi ya Kiswahili kwa vile alilazimishwa kusoma tafsiri tata za hayati Mwalimu Julius Nyerere za kazi za Shakespeare kwa Kiswahili. Anasema anaichukia fasihi na anaifundisha kwenye chuo kikuu!

Je, inawezekana kwamba hata kwenye nchi nyingine za Afrika Mashariki na hasa Kenya wapo walimu wa Kiswahili wanaokichukia na kukidharau? Tutarajieje mwalimu wa bayolojia kupenda Kiswahili?

Na kama walimu wakikichukia na kukidharua Kiswahili wanafunzi watakipendaje? Mwana hufuata kisogo cha nina ati.

Tutaendelea mpaka lini jamani kujipigapiga vifua kwamba Kiswahili ni lugha yetu, sijui lugha ya taifa, sijui lugha rasmi, huku twaendelea kukidharau?

You can share this post!

KUMBUKUMBU 2019: Magavana watatu waanza mwaka mpya wakiwa...

Watu 41 wauawa 29 wakijeruhiwa katika vita vya kikabila...

adminleo