Shughuli za usafiri zarejelewa kama kawaida Lamu siku moja baada ya shambulio
Na KALUME KAZUNGU
SHUGHULI za usafiri wa umma zimerejelewa kama kawaida kwenye barabara kuu ya Lamu-Mombasa ikiwa ni siku moja baada ya wapiganaji wa al-Shabaab kushambulia basi la Mombasa Raha na kuua utingo na abiria wengine wawili wa basi hilo.
Uvamizi huo ulitekelezwa Alhamisi saa sita na nusu mchana ambapo wapiganaji waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari walisimamisha msafara wa mabasi yaliyokuwa yametoka Mombasa kuelekea Lamu kabla ya kuwaamuru abiria wote kushuka na kulala chini.
Baadaye waliwaua kwa kuwapiga risasi watu watatu kabla ya kutorokea kwenye msitu wa karibu.
Kufuatia uvamizi huo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, aliamuru shughuli zote za usafiri wa umma kusitishwa kwa muda ili kupisha walinda usalama kuwasaka na kuwamaliza magaidi waliotekeleza shambulizi hilo.
Katika mahojiano na ‘Taifa Leo‘, Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata, amesema Ijumaa usalama umeimarishwa vilivyo kote Lamu, ikiwemo kwenye barabara kuu ya Lamu-Mombasa na kwamba shughuli za kawaida eneo hilo zimerejelewa.
Bw Elungata amewataka wakazi na watumiaji wa barabara hiyo kuondoa shaka kwani maafisa wa kutosha wa polisi na jeshi (KDF) wamesambazwa eneo hilo ili kuendeleza msako dhidi ya watu wasiojali thamani ya maisha ya binadamu asiye na hatia.
Mshirikishi huyo wa usalama aidha ameamuru kampuni zote ya mabasi ya usafiri wa umma yanayohudumu kwenye barabara ya Lamu kuelekea Mombasa kutii sheria zilizoko za barabarani, ikiwemo kuhakikisha wanasafiri kwenye msafara mmoja unaosindikizwa na maafisa wa polisi.
Alionya wale watakaokaidi amri hiyo kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Tumedhibiti vilivyo usalama kote Lamu, ikiwemo barabarani na tayari shughuli za uchukuzi wa umma zimerejelewa kama kawaida. Cha msingi ni makampuni ya mabasi na magari mengine ya usafiri wa umma kutii mpangilio uliopo barabarani. Lazima gari sisafiri katika msafara mmoja unaosindikizwa na maafisa wetu wa usalama,” akasema Bw Elungata.
Alisema doria za jeshi na polisi pia zimeongezwa maradufu kwenye barabara hiyo ya Lamu kuelekea Mombasa hasa kwenye maeneo ambayo yameshuhudia uvamizi wa awali wa al-Shabaab.
Maeneo hayo ni pamoja na Nyongoro, Lango la Simba, Mambo Sasa, na Milihoi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia anawataka wakazi kote Lamu kuwa macho na kuwaripoti watu wanaowashuku kuwa kero kwa usalama wa nchi ili hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana nao.
“Ninawasihi wakazi, ikiwemo abiria wanaotumia barabara zetu kuwa macho. Mshirikiane nasi na mtoe habari zitakazosaidia walinda usalama wetu kuwakamata washukiwa wa uhalifu na ugaidi eneo hili. Tunataka Lamu yenye amani ili maendeleo yaafikiwe hapa,” akasema Bw Macharia.