Pep awamiminia sifa tele vijana wake

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Pep Guardiola alivulia kofia vijana wake wa Manchester City kwa kuonyesha ujasiri mkubwa, walipoilaza Everton 2-1 siku ya Jumatano dhidi ya Everton yaliyofungwa na Gabriel Jesus siku ya Jumatano.

Straika Gabriel Jesus ndiye alifunga mabao yote mawili na kuipa City ushindi muhimu katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kufungua mwaka Januari 1, 2020.

Jesus alianzishwa katika mchuano huo kocha Guardiola akiamua kumpumzisha sogora Sergio Aguero.

Kwa hakika uamuzi wa kumuacha nje mfungaji huyo bora wa City haukumfanya ajute, baada ya Jesus kuadhibu safu ya ulinzi ya Everton.

Mshambuliaji huyo Mbrazil sasa amefunga mabao saba katika mechi tano dhidi ya Everton.

“Tulicheza vyema sana na hivyo nafurahia kazi yao. Kipindi hiki ni kigumu; tulifanya vyema. Pointi zingine tatu kibindoni na sasa tunakaribia Leicester,” alisema Guardiola.

City inasalia katika nafasi ya tatu baada ya ushindi huo wake wa pili mfululizo, ambao umepunguza mwanya kati yao na viongozi Liverpool hadi alama 11.

Liverpool, hata hivyo, imesakata mechi chache kuliko mabingwa hao watetezi.

“Wakati mwingine unapokuwa mbali na kilele cha jedwali watu hufa moyo, lakini hatukufanya hivyo,” alisema kocha huyo Mhispania.

“Tunafaa kuendelea na mtindo huu. Bado tuko na mashindano ya FA na League Cup mbele yetu. Timu kadha zilipoteza alama katika vita hivi vya kumaliza msimu ndani ya nafasi nne za kwanza (ili kufuzu kombe la UEFA), kwa hivyo ushindi huu ulikuwa muhimu sana kwetu.”

Richarlison alifungia Everton bao la kujifariji kwenye kichapo hicho cha kwanza kabisa cha kocha mpya Carlo Ancelotti, ambaye alijaze nafasi ya Marco Silva aliyetemwa Desemba 2019.

Ancelotti alikuwa ameongoza vijana wake kupepeta Burnley na Newcastle katika mechi zake mbili za kwanza.

City ilinyakua mataji 10 yakiwemo manne ya EPL katika mwongo ambao umepita, lakini fomu ya kutisha ya Liverpool katika kipindi cha miezi 18 iliyopita ndio tishio kubwa katika utawala wake.

Katika mechi zingine zilizosakatwa Jumatano, Jose Mourinho na vijana wake wa Tottenham walikubali kuchapwa 1-0 na Southampton, Brighton ikakaba Chelsea 1-1 nayo Wolves ikapoteza 2-1 dhidi ya Watford. Norwich ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Crystal Palace huku Aston Villa ikilemea Burnley 2-1.

Habari zinazohusiana na hii