• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
MWANAMKE MWELEDI: Alijizolea heshima tele katika mapishi

MWANAMKE MWELEDI: Alijizolea heshima tele katika mapishi

Na KEYB

KWA zaidi ya miongo miwili, alituletea kipindi cha mapishi cha ‘Mke Nyumbani’ kilichopeperushwa na Shirika la Habari la Kenya; KBC.

Alice Taabu aidha aliandika kitabu cha mapishi kwa jina hilo hilo, kilichomshindia nafasi ya kwanza katika tuzo za Gourmand World Cookbook.

Licha ya ustadi wake wa mapishi uliojitokeza kwenye kipindi hiki, upishi haukuwa penzi lake la kwanza kwani kabla ya hapa, alifanya kazi kama mhudumu wa afya katika hospitali kuu ya Pwani, Coast General, kwa miezi minane.

Mzawa wa eneo la Pwani, Bi Taabu alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Ribe na kufika darasa la saba tu.

“Kwetu tulikuwa watoto wanane na wazazi wangu walihisi kwamba ingekuwa vyema ikiwa sote tungeonja kisomo pasipo kuzingitia kiwango ambacho tungefika,” aeleza.

Tangu jadi alifurahia kumtazama nyanyake akiandaa chakula.

“Nyanyangu na mamangu walikuwa wapishi katika familia yetu. Nilitumia wakati mwingi nikiwa na nyanyangu na hatimaye nikajifunza kupika kutoka kwake,” asema.

Baada ya shule ya msingi, alijiunga na Ribe Intermediate, ambapo alisomea kuwa mhudumu wa kiafya, taaluma ambayo hata hivyo alihudumu chini ya mwaka mmoja. “Pengine sikunuiwa kuwa mhudumu wa kiafya, na hivyo nililazimika kurejelea penzi langu la kwanza ambalo lilikuwa upishi,” asema.

Alijiunga na chama cha Young Women’s Christian Association, Nairobi (YWCA) ambapo alijifunza sayansi ya nyumbani kwa miaka miwili. Mwaka wa 1967, Kampuni ya Kenya Power, wakati huo ikijulikana kama East African Power and Lighting, ilimwendea na kumpa fursa ya nafasi ya ajira.

Walikuwa wakimsaka mtu ambaye angeweza kupika, vile vile kuzungumza Kiingereza na Kiswahili. Mhusika alihitajika kutoa mafunzo ya mapishi, vile vile kufunza jinsi ya kutumia umeme na vifaa vya kieletroniki kwa njia nzuri.

Bi Taabu alianza kazi hiyo na kujifunza kwa miezi minne, kabla ya baadaye kuhamia mjini Mombasa ambapo alitoa mafunzo kwa umma. Ni kazi ambayo aliendelea kuifanya kwa miaka 37.

Lakini licha ya ustadi wake katika masuala ya mapishi, anakiri kwamba haukuwa mteremko. Anakumbuka matatizo aliyopitia wakati wa kwanza alipojaribu kuoka mkate, baada ya kuruka hatua muhimu.

“Sikuongeza hamira, suala lililomfanya mkufunzi kunilazimisha kurudia utaratibu huo mara nane, hadi hatimaye nilipofanya ilivyohitajika,” aeleza.

Wakufunzi wake wangemhimiza kuwa na subira na mtulivu, mawaidha aliyoyafuata na hatimaye kumsaidia kufanikiwa.

Nyota yake iling’aa mwaka wa 1976 alipopata mwaliko wa shirika la habari la kitaifa, Sauti ya Kenya (VoK) kuchukua nafasi yake Maggie Gona ambaye alikuwa akikaribia kustaafu kama mtangazaji wa kipindi cha ‘Mke Nyumbani’.

Mwanzoni, Bi Taabu alikuwa na wasiwasi wa kuendesha kipindi hiki kwani hakuwa na mazoea ya kupika mbele ya hadhara kubwa. “Mwanzoni, mwangaza mkali kutoka kwa taa kubwa za studioni ulitisha,” akiri.

Wakati huu alikuwa akishiriki kwenye kipindi hiki, na wakati huo huo alikuwa akifanyia Kenya Power maonyesho, shirika ambalo lilikuwa likidhamini kipindi chake hicho.

Umaarufu wa kipindi hicho ulitokana na usahili wake hasa kuhusu mapishi ya vyakula rahisi kwa mbinu sahili na wazi. “Pia, niliweza kusawazisha baina ya kuwashughulikia watoto wangu na kufanya kazi mbili,” asema.

Pia, alijifunza mengi kutokana na kipindi cha Mke Nyumbani. “Kwanza, ili kufanikiwa kwa chochote lazima uwe na subira, nidhamu na uzingatie muda. Pia, lazima ujipange vyema. Usipozingatia haya, basi hautaenda mbali,” asema Bi Taabu, ambaye anamtaja mamake kama kigezo chake kikubwa.

Ufanisi wake mkubwa hata hivyo umetokana na uandishi wa kitabu chake cha mapishi. “Ari yangu ya kuandika kitabu hiki ilinijia baada ya watu kuanza kuulizia resipe zangu. Nilikuwa nachapisha resipe zangu kwenye magazeti ambapo watu wangeuliza mbona nisichapishe kitabu?” Na hivyo kwa usaidizi wa familia na marafiki zake, alikusanya resipe 500 na hatimaye kuchapisha kitabu.

Japo alistaafu kutoka kipindi cha ‘Mke Nyumbani’ mwaka wa 1999, bado anapotembea barabarani, hutambulika na watu ambao mara nyingi humuuliza kwa nini hakurejea kwenye televisheni.

“Watu huniambia kwamba niliwafunza mengi ambapo wengine hunisimamisha barabarani na kuniitisha resipe zangu au vidokezi vya mapishi,” asema.

Licha ya kwamba kwa sasa amestaafu, bado yeye hutoa mafunzo ya mapishi katika Kanisa la Mombasa Methodist Church of Kenya ambapo yeye ni muumini.

Aidha, yeye ni mwanachama wa bodi ya shule ya upili ya wasichana ya Ribe Girls’, eneo la Kilifi.

Ushauri wake kwa wapishi ni: “Fahamu unachotaka kupika na ujiandae vilivyo. Nunua viungo unavyohitaji mapema ili usipoteze muda ukivitafuta. Kisha, fuata resipe,” aongeza.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Amehatarisha maisha yake mara nyingi kutetea...

SHANGAZI AKUJIBU: Ukatili wa mpenzi kunitema na kuhama...

adminleo