Makala

DAU LA MAISHA: Changamoto kibao ila kasimama kidete

January 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

ANAKIUKA mazingira makali na hali duni ya miundomsingi kuhakikisha kwamba wakazi wa Pokot Magharibi wanafikia huduma za afya.

Kutana na Penina Titimo, mhudumu ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba afya ya uzazi ya akina mama, watoto, vijana na wanaume eneo la Pokot Magharibi inazingatiwa.

Kupitia wadhifa wake kama mhudumu wa afya na naibu mratibu wa afya ya uzazi katika Kaunti ya Pokot Magharibi, majukumu yake yanahusisha kuzuia maambukizi ya maradhi ya zinaa kama vile virusi vya HIV na kaswende kutoka kwa mama mjamzito hadi kwa mtoto.

Pia, amekuwa akipiga vita dhuluma za kijinsia katika eneo hili ambapo haki za wanawake hazizingatiwi sana kitamaduni.

Aidha, kazi yake inahusisha kufunza wahudumu wengine wa afya kuhusu umuhimu wa kuelimisha akina mama na wanandoa kufanyiwa uchunguzi wa virusi vya HIV baada ya kushika mimba na wakati wa kujifungua. “Pia, mafunzo haya yanahusisha kuwahimiza wakazi kuhusu umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi huu hata wakati wa kunyonyesha hadi mwisho wa kipindi cha kunyonyesha ili kuzuia maambukizi ya virusi hivi,” aeleza.

Kadhalika amechangia pakubwa katika jitihada za kuelimisha vijana wa eneo hili kuhusu umuhimu wa kutambua hali zao za HIV, vile vile kuwasisitizia umuhimu wa matumizi ya mipira ya kondomu.

Mbali na hayo pia amekuwa akiwashughulikia waathiriwa wa dhuluma za kijinsia kwa kuhakikisha kwamba wanapokea matibabu, na kufuatilia kesi hizi ili watekelezaji wa unyama huu wachukuliwe hatua za kisheria.

Ni shughuli ambayo imekuwa na matokeo mazuri katika eneo hili huku ikipunguza visa vya maambukizi ya maradhi ya zinaa kutoka kwa akina mama hadi kwa wanao, na hivyo kuhakikisha kwamba watoto wanazaliwa wakiwa na afya. Aidha, jitihada zake zimechangia pakubwa kuangazia suala la dhuluma za kijinsia.

Lakini licha ya ufanisi huu haijakuwa rahisi huku akikabiliana na changamoto mbalimbali.

“Tatizo kuu limekuwa utamaduni wa eneo hili ambapo jamii nyingi hapa hazikubaliani na suala la upangaji uzazi, kumaanisha kwamba ni vigumu hata kushawishi akina mama kuzalia hospitalini. Tunavyozungumza, ni asilimia 27 pekee ya akina mama wanaokuja kuzalia hospitalini, suala linalotia wasiwasi,” asema.

Aidha, anazungumzia changamoto ya unyanyapaa, suala ambalo limefanya iwe vigumu kwa watu kukubali kufanyiwa uchunguzi kubaini hali yao ya HIV.

“Asilimia 54 ya wanawake wanajifungua bila kujua hali zao za HIV na maradhi ya kaswende,” aeleza.

Lakini anasema kwamba tatizo kuu limekuwa miundomsingi duni, shida ambayo imeathiri uwezo wa kufikia watu wanaohitaji huduma hizi.

“Barabara duni za kuingia vijijini, vilevile mwendo mrefu kuelekea katika vituo vya afya, ni masuala ambayo huwavunja wakazi wengi mioyo na hivyo kuwazuia kusaka huduma za kiafya hospitalini,” asema.

Hata hivyo anasema kamwe havijasitisha jitihada zake kuhakikisha kuwa, wenyeji wa eneo la Pokot Magharibi wanapokea huduma mwafaka za afya kama wakazi wa sehemu zingine nchini.

“Ndoto yangu ni kuhakikisha idadi ya akina mama wajawazito wanaopokea huduma za kliniki inaongezeka, suala ambalo nina uhakika kwamba litapunguza vifo vya watoto na akina mama wakati wa kujifungua. Hii pia itapunguza maambukizi ya HIV na maradhi mengine ya zinaa kutoka kwa akina mama hadi kwa watoto wao,” asema.

Aidha, anazungumzia azimio lake la kukabiliana kabisa na visa vya dhuluma za kijinsia kama vile ukeketaji, ndoa za kulazimishwa na wanaume kuwapiga wake zao, kwa kuelimisha watu kupitia mikutano ya machifu na wazee wa vijijini.