Serikali kutumia ndege kunyunyiza kemikali kukabiliana na kero ya nzige – Oguna
BRUHAN MAKONG na MARY WANGARI
SERIKALI inatarajia kuanza shughuli ya kutumia ndege kunyunyiza takribani lita 3,000 za kemikali kuangamiza mamilioni ya nzige waliovamia eneo la Kaskazini mwa Kenya huku wingu jingine kubwa la wadudu hao likionekana ambapo wamevamia Kaunti ya Wajir na kuibua hofu miongoni mwa Wakenya.
Akizungumza na vyombo vya habari, Msemaji wa serikali Kanali Cyrus Oguna amesema Jumamosi kwamba Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amearifiwa kikamilifu kuhusu suala hilo na kwamba mikakati ya dharura imeanza kutekelezwa ili kukabiliana na suala hilo haraka iwezekanavyo.
“Serikali imetuma makundi ya kutathmini katika kaunti zilizoathiriwa. Timu hizo zitaelekeza unyunyuziaji kutoka angani wa lita 3000 za kemikali iliyofanyiwa majaribio na kuidhinishwa kuanzia leo,”
Afisa huyo pia aliwahakikishia Wakenya kwamba serikali ilikuwa imedhibiti kikamilifu tatizo hilo la nzige huku akiwahimiza Wakenya kurejelea shughuli zao kama kawaida.
“Hili ni suala ambalo serikali imedhibiti kikamilifu. Hali hiyo imedhibitiwa. Wakulima wote na Wakenya na wakazi kwa jumla wanapaswa kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa kama kawaida,” amesema Bw Oguna.
Haya yamejiri siku moja tu baada ya mamilioni ya nzige wa jangwani kutoka ama Ethiopia au Somalia kuvamia eneo la Kutulo, Kaunti ya Wajir baina ya Jumatano na Ijumaa katika hali iliyoibua taharuki eneo hilo.
Wingu la nzige hao waliovamia eneo hilo kwa mara ya pili, lilikuwa kubwa mara tatu zaidi kwa idadi ya nzige kushinda kundi la kwanza lililoshambulia eneo hilo siku nne zilizopita, kwa mujibu wa afisa kutoka Idara ya Kilimo katika Kaunti ya Wajir, Hassan Gure.
Kulingana na Bw Gure, idadi ya nzige hao ilikuwa kubwa kupindukia kiasi kwamba Polisi wa Akiba Nchini (NPRs), walipatiwa idhini ya kuwatawanya kwa kufyatua risasi za mipira hewani ili kuwasaida wakazi kuwafukuza nzige hao kutoka eneo hilo.
Alisema kuwa kundi la nne la nzige hao lilikuwa pia limeingia Wajir kupitia upande wa Mashariki mnamo Alhamisi, na kuvamia eneo la Dadajabula, lililo kwenye mpaka kati ya Wajir na Garissa.
Afisa huyo alisimulia jinsi wakazi mnamo Ijumaa walivyolazimika kurejelea kibarua cha kuwafukuza nzige hao ambao awali, walishambulia eneo hilo na kutafuna mimea yote kutoka chini hadi kwenye miti.
“Nyasi yote, vichaka na matawi na majani ya miti yametafunwa na nzige,” alieleza Bw Gure.
Bw Gure alielezea wasiwasi wake kwamba wadudu hao huenda wakasambaa katika maeneo mengine nchini ikiwa mikakati ya dharura haitabuniwa.
“Suala hili sasa linazidi kuwa la kutisha zaidi na tunahofia kuwa nzige hao huenda wakaendelea kusambaa katika maeneo mengine ya kaunti,” alisema.
Ripoti za awali ziliashiria kwamba baadhi ya wakazi walikuwa wamehamishwa eneo hilo ili kutoa nafasi ya kuwaangamiza wadudu hao kwa kutumia mbinu zinazotumika eneo hilo kama vile: kupaaza sauti, kupiga honi za magari na kugonga vifaa vya vyuma ili kuwafukuza nzige hao kwa kuwashtua.