Habari

Mhubiri ajiua baada ya kumsababishia mke majeraha yaliyomuua

January 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

DIANA MUTHEU na ANTHONY KITIMO

MHUBIRI mmoja eneo la Bamburi, Kaunti ya Mombasa alijitoa roho Jumapili katika madhabahu ya kanisa lake, baada ya jaribio la kumuua mkewe ndani ya kanisa hilo katikati ya ibada, kutibuka japo pia alifariki baadaye akitibiwa.

Mhubiri huyo, Bw Elisha Misiko wa kanisa la Ground for God’s Gospel Ministries lililoko Chembani, Bamburi, alimdunga mkewe, Ann Mghoi mgongoni kwa kutumia kisu kisha akajitoa uhai kwa kujikata shingo akitumia kifaa hicho.

Mwanamke huyo aliyenusurika na majeraha ya kisu mgongoni, mkononi na tumboni baadaye aliaga dunia mwendo wa saa saba mchana, alipokuwa akiendelea kupata matibabu katika hospitali kuu ya eneo la Pwani (CGPH).

Bi Mghoi aliokolewa na washirika wa kanisa hilo na kukimbizwa hospitalini.

Polisi walithibitisha kuwa kiini cha mauaji hayo ni mgogoro kati ya wanandoa hao baada ya kupata waraka wenye zaidi ya kurasa 10, ulioelezea sababu za mhubiri huyo kuchukua hatua hiyo ya kutisha.

Miongoni mwa masuala yaliyonukuliwa katika karatasi hizo ni pamoja na mke wake kumvunjia heshima na pia kumdharau licha ya kujitolea kwake kulijenga kanisa hilo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti-ndogo ya Kisauni, Bw Julius Kiragu alisema mhubiri huyo alifariki katika kanisa hilo na mwili wake ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya CGPH.

“Watu kadhaa wameandikisha taarifa na tumethibitisha tukio hilo lilitokea baada ya mke wa mhubiri huyo kujaribu kumtoa mchungaji huyo katika kanisa ambalo alijitahidi kulijenga,” alisema Bw Kiragu.

Mzee wa kijiji, Bw Mtengo Amuri, alisema kuwa mhubiri huyo alitenda unyama huo kufuatia ugomvi uliokuwa unaendelea kati yake na mkewe.

“Wawili hawa wamekuwa wakiliendesha kanisa hili kwa zaidi ya miaka minane. Miezi michache iliyopita, kumekuwa na tofauti baina yao kuhusu usimamizi wa kanisa hilo. Tunashuku kuwa hiyo ndiyo sababu kuu ya tukio hilo,” alisema Bw Amuri.

“Mchungaji huyo alitembea polepole hadi kwenye altari ambapo mkewe alikuwa ameketi. Alimdunga mgongoni kwa kutumia kisu na alipojaribu kumkata koo, mke wake alijizuia kutumia mkono kabla ya waumini kumuokoa.”

Muumini mmoja wa kanisa hilo ambaye alizungumza na ‘Taifa Leo‘, alisema kuwa wawili hao walikuwa na ugomvi nyumbani hata kabla ya kuhudhuria ibada.

“Leo ni Jumapili ya kwanza ya mwaka 2020. Tunasikitika kuwa tumekuwa tukijitahidi kusuluhisha mgogoro kati ya wawili hawa bila ya kufanikiwa,” alisema mmoja wa waumini.

Alidokeza kuwa vita kati ya mhubiri huyo na mkewe vilianza kutokana na usimamizi wa kanisa hilo pamoja na fedha.

Marehemu hao wamewaacha watoto wanne wenye umri wa chini ya miaka 18.