• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
DIMBA PWANI: Bandari wageuzwa windo la timu miamba Kenya wakiwemo K’Ogalo

DIMBA PWANI: Bandari wageuzwa windo la timu miamba Kenya wakiwemo K’Ogalo

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KUNA msemo kuwa mti wenye matunda mazuri ndio unaopigwa mawe.

Na msemo huo ndio unaoakisi kikamilifu hali ilivyo kwa klabu ya Bandari FC ambayo wakati huu inanyemelewa na klabu kadhaa zenye nia ya kuwasajili wachezaji wake tegemeo.

Habari ambazo hazijathibitishwa zinafahamisha ukumbi huu kuwa miamba ya soka hapa nchini, Gor Mahia FC ambayo imepania kuwasajili wanasoka watatu wa kuaminika wa Bandari.

Kulingana na uvumi ulioenea, viongozi hao wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor wamekula yamini kuhakikisha kuwa wanawasajili kiungo Abdalla Hassan na mastraika wawili William Wadri na Yema Mwana katika kipindi hiki kifupi cha usajili.

Limekuwa jambo la kawaida kwa maafisa wa Bandari kutopendelea kuongelea jambo lolote lile linalohusiana na uhamisho wa wachezaji wake. Kwa wanasoka hao watatu, inaonekana dhahiri, uvumi huo ni kweli kwani afisa wa Gor aliwahi kusema wana nia ya kuwasajili.

Kwa upande wa Bandari, maafisa wake mara nyingi huwa wanakanusha kama kuna mipango yoyote ya kuwaacha wachezaji wake kwenda klabu nyingine; mfano mkubwa ukiwa wa aliyekuwa golikipa wao Farouk Shikhalo kuhamia klabu ya Yanga ya Tanzania.

Uvumi wa Shikhalo kutakiwa kusajiliwa na Yanga ulipotokea, maafisa wa Bandari walikanusha na kusisitiza kuwa mwanasoka huyo ni mchezaji wao wala hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika na wakuu wa klabu hiyo ya Bongo juu ya uhamisho huo.

Lakini kanusho hilo halikufua dafu kwani Shikhalo alisajiliwa rasmi kulingana na kanuni na sheria za usajili.

Swali kubwa wanaloliuliza mashabiki wa timu hiyo ya pekee ya jimbo la Pwani inayoshiriki ligi kuu ni, kuna ukweli wowote wa wanasoka wake watatu kusajiliwa na Gor?

Kulingana na kocha mkuu Bernard Mwalala, wanasoka hao watatu wangali wachezaji wao wala hakuna habari juu yao kuihama timu.

Alifahamisha Dimba katikati ya wiki hii kuwa Wadri na Yema wanauguza majeraha hali Hassan yuko uwanjani akifanya mazoezi na wachezaji wenzake.

Ukumbi huu ulipofika uwanja wa Mbaraki SC mnamo Alhamisi ya wiki iliyopita, ilimkuta Hassan akiwa mazoezini.

Kuzoeana

Pia iligundua sajili ya pekee ya Bandari, Mike Mwita akifanya mazoezi na kuonekana tayari amezoeana na wenzake.

Mwita amesajiliwa kutoka Sony Sugar, timu ambayo imebanduliwa nje ya ligi kuu kutokana na kutocheza mechi tatu za ligi hiyo.

Sony imeteremshwa ngazi na msimu ujao itashiriki kwenye Supaligi ya Taifa.

Habari nyingine ambayo haijathibitishwa ni kuwa klabu moja maarufu inayoaminika kuwa Simba SC ya Dar es Salaam ya nchini Tanzania ina mpango wa kumsajili kocha wa magolikipa wa Bandari FC, Razak Siwa.

Siwa ambaye aliwahi kuwa kocha wa makipa katika klabu ya Yanga na pia kuwahi kushikilia wadhifa huo katika timu ya Harambee Stars, hakukanusha wala kukubali kama anafanya mazungumzo na wakuu wa mabingwa hao wa soka ya Tanzania, Simba SC.

Kwa vyovyote vile, habari za kuhama kwa wanasoka hao na mkufunzi huyo zinawatia hofu baadhi ya mashabiki ambao wana hamu kuu ya kuiona timu yao hiyo inabeba taji la KPL na kuwa timu ya pili baada ya Feisal FC mwaka 1965 katika historia ya soka ya Kenya kwa timu ya jimbo la Pwani kuwa mabingwa.

You can share this post!

Watatu wakamatwa kwa kujaribu kuingia kambi ya mazoezi ya...

Yaibuka Ruto ‘alimsindikiza’ Uhuru uchaguzini

adminleo