• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
KAMAU: Magufuli adhibitiwe na EAC, amevuka mipaka!

KAMAU: Magufuli adhibitiwe na EAC, amevuka mipaka!

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Novemba 5, 1984, kinara wa ODM Raila Odinga alifahamishwa kuhusu kifo cha mamake, Bi Mary Juma ikiwa imepita muda wa miezi miwili tangu afariki.

Mary alifariki mnamo Septemba 1984, lakini Bw Odinga hakuwa na ufahamu wowote kuhusu tukio hilo kwa kuwa alikuwa akitumikia kifungo katika Gereza la Shimo la Tewa, jijini Mombasa.

Alikuwa na mfungwa mwenzake, Bw George Anyona alipopata habari hizo za kuhuzunisha.

Kwa jumla, ilikuwa vigumu kwa wafungwa kuwasiliana na jamaa zao wakati huo kutokana na ulinzi mkali waliowekewa na serikali ya Rais Mstaafu Daniel Moi.

Kwa mujibu wa simulizi nyingi za watu waliojipata kama wafungwa wa kisiasa katika utawala wa Mzee Jomo Kenyatta na Bw Moi, walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao kwa kuandika kwenye shashi ndipo wasijulikane na serikali.

Katika maisha, hilo ndilo mojawapo ya pigo kubwa zaidi mwanadamu yeyote anaweza kukumbana nalo; kutopata nafasi ya kumuaga mzazi, hasa mama.

Hali hiyo hiyo ndiyo imemkumba mwanahabari Eric Kabendera kutoka Tanzania, anayeendelea kuzuiliwa na serikali ya Rais John Magufuli, kwa tuhuma za kuandika habari za “uongo na kuwapotosha” wananchi.

Bw Kabendera amekuwa akizuiliwa kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, huku juhudi zake zote kuomba msamaha Rais Magufuli zikigonga mwamba.

Serikali pia imepuuzilia mbali rai za mawakili wake kumwachilia kwa dhamana ili kuendelea na kesi yake akiwa huru.

Majuma mawili kabla ya kifo chake, Bi Verdiana Mjwahuzi alikuwa amemwomba Rais Magufuli kumsamehe mwanawe, hasa baada ya Bw Kabendera kumwandikia barua akimwomba msamaha.

Licha ya juhudi hizo zote, Bw Magufuli alifumbia macho kilio hicho cha mama kwa niaba ya mwanawe.

Taswira hii bila shaka inaondoa dhana ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kwamba, Bw Magufuli ni “ufufuo na msisimko” wa aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa hilo, Bw Julius Kabarage Nyerere.

Badala yake, ameibuka kuwa kiongozi wa kiimla anayeendesha taifa hilo kwa mfumo wa kidikteta.

Chini ya utawala wa Bw Magufuli, uhuru wa wanahabari umedidimia pakubwa, huku baadhi yao wakitoweka wasijulikane waliko.

Mfano dhahiri ni mwanahabari Azory Gwanda, aliyetoweka Novemba 2017 katika hali ya kutatanisha. Hadi sasa, haijulikani aliko mwanahabari huyo.

Kando na wanahabari, Tanzania pia imekuwa ikiwahangaisha viongozi wa upinzani, mmoja wao akiwa aliyekuwa mbunge wa Singinda Mashariki, Bw Tundu Lissu.

Mnamo Oktoba 2017 gari la Bw Lissu lilimiminiwa risasi zaidi ya 30 baada ya kuondoka kwenye kikao cha Bunge jijini Dodoma.

Bw Lissu, ambaye ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Magufuli na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alipoteza kiti chake akitafuta matibabu katika nchi mbalimbali barani Ulaya.

Bila shaka, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wafaa kusimama kidete kupinga dhuluma anazoendeleza Bw Magufuli dhidi ya wapinzani wake. Kwa sasa anairejesha kanda hii katika enzi ya giza.

 

[email protected]

You can share this post!

OBARA: Mwaka huu kuwe na mageuzi mwafaka sekta ya elimu

Msitu wa Mau kuzungushiwa ua kuanzia Aprili –...

adminleo