Masaibu ya Weta ni mwiba wa kujidunga – Raila
Na VALENTINE OBARA
KIONGOZI wa Chama cha Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula, ametakiwa akome kumlaumu mwenzake wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kwa masaibu ya kisiasa anayopitia.
Maseneta wa Muungano wa NASA na Bw Dennis Onyango, ambaye ni msemaji wa Bw Odinga, Jumanne walipuuzilia mbali madai ya Seneta huyo wa Bungoma kwamba Bw Odinga ndiye alipanga njama na maseneta hao kumpokonya mamlaka ya kiongozi wa wachache katika seneti.
Kulingana na Bw Onyango, uamuzi wa kumg’oa Bw Wetang’ula ulifanywa na maseneta ambao hawakupendezwa na mitindo yake ya uongozi kwa hivyo anapaswa kujilaumu mwenyewe.
“Kufikia leo, hakuna seneta wa NASA ambaye amejitokeza kumtetea Bw Wetang’ula. Hatujawahi kushuhudia kiongozi akikataliwa jinsi hii kwa hivyo ni ishara inayoonyesha kulikuwa na tatizo kubwa kati yake na wenzake,” akasema kwenye taarifa kwa vyumba vya habari.
Seneta wa Siaya, Bw James Orengo wa ODM, alichaguliwa kuchukua nafasi ya Bw Wetang’ula.
Bw Wetang’ula amekuwa akidai kuwa kinara mwenzake, Bw Odinga, alifahamu kuhusu mipango ya kung’olewa kwake kwani anaamini wanachama wa ODM hawawezi kuchukua hatua kubwa kama hiyo bila kiongozi wao kujua.
Suala la kikabila
Lakini Bw Orengo alisema inasikitisha jinsi suala hilo limegeuzwa kuwa la kikabila ilhali uamuzi ulifanywa kidemokrasia.
“Raila Amolo Odinga hafai kuhusishwa kwa suala hilo kwa kuwa hakuna seneta yeyote kutoka kwa vyama tanzu ambaye alipinga mabadiliko ya uongozi katika seneti,” akasema.
Bw Onyango alifichua kuwa wakati wa mkutano ulioitishwa na Bw Odinga kumpatanisha seneta huyo na wenzake, maseneta walimlaumu kwa “kutofahamu mambo, kuwa mbinafsi, mjeuri na mwenye uzoefu wa kuwalazimishia maamuzi kwa kudai yalikuwa maagizo ya wakuu wa NASA ilhali wakati mwingi huo ulikuwa ni uongo”.
Bw Wetang’ula jana alinukuliwa kusema Bw Odinga alikutana kisiri na maseneta wa ODM ambapo mpango wa kumng’atua ulifanywa.