Habari

Serikali yakanyagia Miguna breki tena

January 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MATUMAINI ya wakili mbishi Miguna Miguna kurudi nchini Jumanne yaligonga mwamba baada ya Serikali kumzuia kusafiri kutoka Ujerumani.

Bw Miguna alitarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi saa tatu usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Lufthansa kutoka Ujerumani.

Hata hivyo shirika hilo lilimzuia kuabiri ndege kutoka mjini Frankfurt, Ujerumani kuelekea Nairobi baada ya kupewa tahadhari na Serikali ya Kenya.

Bw Miguna alikuwa amefanikiwa kuwasili Ujerumani kutoka Canada anakoishi na familia yake na alitarajia kuabiri ndege ya kumleta Nairobi kutoka hapo.

Lakini hakuweza kusafiri baada ya serikali kutahadharisha shirika la Lufthansa dhidi ya kumsafirisha nchini ama nchi yoyote katika Bara la Afrika.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, Bw Miguna alidai Serikali ililiagiza shirika hilo kumrudishia nauli ya ndege aliyokuwa amelipa kusafiri nchini Kenya.

“Serikali ya Kenya imeliagiza Shirika la Lufthansa kurudisha nauli yangu. Imeliagiza kutonisafirisha nchini ama nchi yoyote barani Afrika. Meneja wa Kusimamia Safari za Ndege anasema kuwa lazima serikali itume taarifa rasmi kabla niruhusiwe kusafiri Kenya ama nchi nyingine yoyote barani Afrika,” akasema.

Shirika hilo kwa upande wake lilisema huwa linahitajika kutuma kwa serikali ya Kenya orodha ya wasafiri wote wanaotumia ndege zake kuja Kenya kabla ya kuanza safari, na lilipofanya hivyo jana serikali ilishauri lisimsafirishe Bw Miguna kuja Kenya.

Hii ni licha ya kuwa mnamo Jumatatu Serikali ilisema haingemzuia wakili huyo kurudi nyumbani.

Msemaji wa Serikali Kanali Cyrus Oguna alisema suala hiyo lingeweza kutatuliwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Juhudi za Bw Miguna kurudi nchini zimekuwa zikigonga mwamba tangu 2018 serikali ya Jubilee ilipomtimua nchini kwa visingizio kuwa si raia wa Kenya.

Anasema kuwa serikali imekuwa ikimhangaisha kimakusudi kwani paspoti yake ya Kenya inashikiliwa na Idara ya Uhamiaji.

Mahangaiko ya Miguna yaliendelea hadi usiku ambapo aliondolewa katika ndege ya Air France kabla ya kuondoka jijini Paris na ambayo alisema ilitarajiwa kutua jijini Nairobi ikikaribia saa kumi na mbili za asubuhi leo Jumatano.