Ronaldo asisimua Serie A na hat-trick ya kwanza Italia
Na MASHIRIKA
TURIN, Italia
NYOTA Christiano Ronaldo alifungia Juventus mabao matatu katika mechi moja, na kuandikisha hat-trick yake ya kwanza katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Mabao ya Ronaldo yalisaidia mabingwa hao wa Serie A kuandikisha ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Cagliari, Jumatatu usiku.
Ufanisi huo umechangia idadi ya mabao yake kufika manane, katika mechi tano za majuzi kwenye ligi hiyo ya Italia.
Raia huyo wa Ureno alifunga bao la kwanza kufuatia makosa ya safu ya ulinzi ya Cagliari, dakika nne baada ya kipindi cha mapumziko.
Aliongeza la pili kutokana na mkwaju wa penalti.
Baada ya kumuandalia Gonzalo Higuin pasi la kufunga bao la tatu dakika ya 81, Ronaldo alipachika wavuni bao lake la tatu dakika moja baadaye.
Juventus wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 45 kutokana na mechi 18.
Hii ni sawa na Inter Milan ambao wanaongoza kwa tofauti ya mabao.
Idadi ya mabao ya Ronaldo, 34, katika mashindano yote msimu huu imefika 15, yakiwemo 13 aliyofunga katika Serie A.
Yuko katika fomu nzuri ya ufungaji wa mabao tangu atue Juventus kutoka Real Madrid mnamo 2018, akicheka na wavu katika mechi tano zilizopita za Serie A.
Katika mechi nyingine ya ligi iliyochezwa baadaye, Inter Milan walitandika Napoli 3-1 ugani San Siro.
Mshambuliaji Romelu Lukaku alifunga magoli mawili kabla ya Arkaduisz Milik kuipa Napoli bao la kufutia machozi.
Juhudi za Napoli zilizimwa dakika ya 62 bao la tatu la Inter lililopofungwa na Lautaro Martinez.
Ibra arejea
Kwingineko, kurejea kwa mkongwe Zlatan Ibrahimovic, almaarufu Ibra, katika ligi hiyo hakukuwa na makali yoyote baada yake kushindwa kuisaidia AC Milan kupata ushindi dhidi ya Sampdoria katika mechi ambayo ilitamatika kwa sare tasa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38 aliingizwa dakika ya 55 na kushangiliwa na mashabiki waliofurika ugani San Siro.
Hata hivyo, Ibra hakuonyesha makali kama ilivyotarajiwa.
Raia huyo wa Uswidi aliwahi kuichezea AC Milan msimu wa 2010-11 na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Serie A msimu huo.
Aliondoka na kujiunga na Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa mwishoni mwa msimu uliofuata.
Matokeo mengine ya awali ikiwemo kutoka sare dhidi ya Sassuolo yameiacha Milan katika nafasi ya 12 kwenye jedwali la Seria A, chini ya klabu ya Verona kwa tofauti ya mabao.
Majuzi, Milan walinyukwa 5-0 na Atlanta, ambao walicharaza Parma kwa idadi kama hiyo, katika mechi ambayo Josip Ilicic alifunga mabao mawili.