Habari

Mahakama yaamuru serikali ijibu kesi ya Miguna

January 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAWAKILI wa mwanaharakati na wakili mwenye tajiriba ya juu Dkt Miguna Miguna anayekumbwa na matatizo ya usafiri Jumatano wameomba Mahakama Kuu ishurutishe Serikali kufanikisha kurudi kwake nchini Kenya.

Dkt Miguna aliyetarajiwa kuingia nchini Jumatano angali jijini Paris, Ufaransa akisubiri Serikali ya Kenya itoe agizo la kumruhusu kuabiri ndege arudi nyumbani.

Dkt Miguna ambaye pia ni raia wa Canada alitarajiwa kurudi nchini Januari 7/8, 2020, lakini angali anakumbwa na matatizo ya usafiri.

Baada ya Dkt Miguna kuwafahamisha mawakili Dkt John Khaminwa na Nelson Havi matatizo yanayomkabili, waliwasilisha kesi chini ya sheria za dharura wakiomba Serikali ishurutishwe kumruhusu aingie nchini.

Alipofika mbele ya Jaji Weldon Korir , Dkt John Khaminwa aliomba mahakama iamuru Serikali imruhusu Dkt Miguna arudi nchini.

“Licha ya agizo lako la Ijumaa wiki iliyopita ukiamuru serikali ifanikishe kurudi kwa Dkt Miguna bado anakumbwa na matitizo ya kurudi nchini baada ya Serikali kutotoa ilani yake kwa mashirika ya ndege ya kimataifa,” alisema Dkt Khaminwa.

Wakili huyo aliambia mahakama Dkt Miguna angali Ufaranza na mashirika ya ndege ya kimataifa hayataki aabiri ndege zao kurudi Kenya.

“Licha ya hakikisho la serikali kwamba haipingi Dkt Miguna akirudi nchini bado anakabiliwa na matatizo ya usafiri,” Dkt Khaminwa alieleza korti.

Jaji Korir alimwamuru Dkt Khaminwa aikabidhi idara husika nakala za kesi ndipo iwasilishe ushahidi na kufika kortini kesho kusikiza hiyo.

Dkt Khaminwa aliambia Mahakama alizugumza na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i aliyemweleza Serikali haipingi Dkt Miguna akirudi.

Mahakama Jumatatu ilitoa agizo la kuishurutisha serikali kufanikisha Dkt Miguna kurejea nchini Jumanne.

Jaji Korir aliwaamuru; Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji, Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Inspekta Jenerali wa Polisi wasimtatize mwanaharakati huyo.

Dkt Miguna alifurushwa nchini mwaka 2018 baada ya kumwapisha kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga kuwa ‘Rais wa wananchi’.

Jaji Korir amemwamuru Msajili wa Mahakama Kuu amrudishie Dkt Miguna pasipoti yake kupitia kwa wakili wake ama afisa wa tume ya kutetea haki za binadamu nchini (KNCHR).

Punde tu Mahakama Kuu ilipotoa agizo hilo Jumatatu, serikali ilitangaza itafanikisha kurudi kwake mradi awe na hati zilizo sahihi.

Msemaji wa Serikali Kanali (mstaafu) Cyrus Oguna alisema ushauri wa Rais Uhuru Kenyatta kuhusu kurudi kwa Dkt Miguna unazingatiwa.

Lakini Kanali Oguna alibainisha Dkt Miguna atakaguliwa kama wananchi na wasafiri wale wengine na lazima awe na hati halisi za usafiri.