Habari

Miguna anavyojikaanga mwenyewe

January 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MSIMAMO mkali wa wakili mbishi Miguna Miguna ndicho chanzo cha masaibu yanayomwandama, wamesema wadadisi.

Dkt Miguna alizuiwa kurudi Kenya mnamo Jumanne baada ya Shirika la Ndege la Ufaransa kudai kupokea agizo kutoka kwa serikali ya Kenya kutomsafirisha nchini.

Masaibu yake yamezua hisia mseto, huku baadhi ya viogozi wakiilaumu serikali kwa kumhangaisha kimakusudi.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’ Jumatano, Maprofesa Peter Kagwanja na Macharia Munene wanasema kuwa Dkt Miguna ni mwanasheria mwenye uwezo mkubwa, hasa kimasomo, ingawa anautumia vibaya.

“Nimefanya kazi na Bw Miguna kwa muda, na ni mwanasheria mwenye uwezo mkubwa kiakili. Vile vile, ni mwandishi mwenye mawazo mapevu ambayo yangekuwa yenye manufaa makubwa kwa nchi, ikiwa angeyaelekeza katika juhudi za kuifaa jamii,” akasema Prof Kagwaja.

Mdadisi huyo anasema kuwa ni sababu hiyo ambapo kinara wa ODM Raila Odinga alimchukua kuwa mshauri wake mkuu alipohudumu kama Waziri Mkuu kati ya 2007 na 2013 kwenye Serikali ya Muungano kati yake na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Bw Miguna alihudumu katika wadhifa huo kati ya mwaka 2009 na 2011.

“Kimsingi, Bw Odinga alimdhamini sana Bw Miguna kutokana na uelewa wake mpevu wa masuala ya sheria na siasa. Hata hivyo, mojawapo ya udhaifu wake mkubwa ni hasira na kutokubali kukosolewa,” asema Prof Kagwanja.

Naye Prof Munene anasema kuwa lazima wakili huyo atii sheria.

Mvutano kati yake na serikali ulizidi kutokota jana, baada ya Msemaji wa Serikali Kanali Cyrus Oguna kudai kwamba wakili huyo atakubaliwa nchini tu ikiwa atakuwa na stakabadhi zifaazo, ikiwemo paspoti.

Vilevile, alisema kuwa sababu kuu ya mashirika ya ndege ya Lufthansa (Ujerumani) na Ufaransa kumkataza kusafiri ilitokana na mienendo yake ambayo inakiuka kanuni za kimataifa kuhusu usafiri wa ndege.

“Lazima abiria anayesafiri kwa ndege azingatie sheria na kanuni zote zilizowekwa. Tatizo lake [Dkt Miguna] ni kukiuka sheria hizo,” akasema kwenye taarifa.

Hata hivyo, Chama cha Wakenya Wanaoishi Ughaibuni (KDA) kiliikosoa vikali serikali, kikitaja sababu hiyo kama kisingizio tu cha kumzuia kurejea nchini.

“Tunafahamu kuhusu sheria mpya za usafiri wa ndege ambazo zimeanza kutekelezwa. Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote kwamba Dkt Miguna amekiuka sheria hizo kutokana na mienendo yake,” akasema Dkt Shem Ochuodho ambaye ndiye mwenyekiti wa chama hicho.

Dkt Miguna alifutwa kazi na Bw Odinga mnamo Septemba 2011 kwa tuhuma za “kiburi na kutowaheshimu wafanyakazi wenzake.” Alirejeshwa kazini baada ya miezi miwili lakini akakataa.

Tangu kurudishwa kwa lazima na serikali nchini Canada mnamo 2018, amekuwa akitoa jumbe zake kali kupitia mitandao ya Twitter na Facebook, huku akifuatwa na mamilioni ya watu.

Amekuwa akitumia mitandao hiyo kama majukwaa ya kuwasiliana na wafuasi wake nchini.

Masaibu yake pia yalivuta hisia za baadhi ya viongozi, huku mbunge wa Kandara Alice Wahome akimlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kwa masaibu yanayomwandama wakili huyo.