Habari

Uhuru ataingia orodha gani?

January 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amepata fursa ya kuamua iwapo ataingia kwenye orodha ya aibu ya marais wa Afrika waliokatalia madarakani, ama ile ya viongozi wa kuheshimika walioondoka madarakani baada ya kukamilisha muda wa kikatiba wa utawala wao.

Hii ni baada ya kuzuka kwa mjadala kufuatia miito ya baadhi ya wanaomuunga mkono kuwa Katiba inapasa kubadilishwa ili kumwezesha kuendela kuhudumu katika cheo cha juu hasa cha Waziri Mkuu baada ya kukamilisha kipindi chake cha urais hapo 2022.

Wanaopiga kampeni hii wakiongozwa na David Murathe na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyikazi (COTU), Francis Atwoli wanasema Ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) inapasa kutumika kuwezesha mabadiliko ya kikatiba ambayo yatamwezesha Rais Kenyatta kupewa wadhifa wa Waziri Mkuu.

Lakini naibu wake William Ruto ametilia shaka kuwa Rais anataka kuendelea kutawala baada ya 2022: “Sidhani kama Rais ana mpango wowote wa kubadilisha katiba kuongeza muda wake wa kuhudumu. Ninasema hivi kwa vile ninamjua vyema na anaheshimu demokrasia.”

Ripoti ya BBI imependekeza kubuniwa kwa cheo cha Waziri Mkuu na tayari wanasiasa wanashinikiza kufanyika kwa kura ya maamuzi hivi karibuni kuipitisha.

Ingawa hajakanusha matamshi ya wandani wake kwamba kuna mpango wa kubadilisha Katiba ili aendelee kuhudumu, Rais Kenyatta alinukuliwa mwaka 2019 akiwa katika Ikulu ya Sagana, Kaunti ya Nyeri akisema hatajali kuendelea uongozini iwapo Wakenya wangependa hivyo.

Wanaopinga pendekezo lake wanasema kwa kukubali kuundiwa cheo cha Waziri Mkuu, Rais Kenyatta ataingia katika orodha ya viongozi ambao wamehujumu demokrasia ya nchi zao kwa kubadilisha katiba ili waendelee kutawala.

Nchini Ivory Coast, Rais Alassane Ouattara pia ameripotiwa kuwa ana mpango wa kubadilisha Katiba ili aweze kugombea urais kwa kipindi cha tatu.

Wakosoaji wanasema Rais Kenyatta anapaswa kujiunga na orodha ya viongozi mashuhuri barani Afrika badala ya kuwa katika orodha ya wanaobadilisha katiba ili wakwamilie mamlakani.

Kati ya marais walioondoka madarakani kwa uungwana ni pamoja na Mwai Kibaki (Kenya), Jakaya Kikwete (Tanzania), Ian Khama (Botswana) na Olusegun Obasanjo (Nigeria).

Katika orodha ya aibu kuna Yoweri Museveni (Uganda), Pierre Nkurunziza (Burundi), Paul Biya (Cameroon), Denis Sassou Nguesso (Congo Brazaville), Omar al-Bashir (Sudan), Robert Mugabe (Zimbabwe), Hosni Mubarak (Misri) miongoni mwa wengine.

Tawala za marais wanaokwamilia mamlakani kwa kawaida hugeuka kuwa kero kwani wengi hubadilika na kuwa madikteta katika juhudi zao za kubakia madarakani.

Pia nyingi za nchi hizo hukumbwa na misukosuko ya kisiasa, kuporomoka kwa uchumi, ukiukaji wa haki za binadamu na utawala mbaya

Katika taifa jirani la Uganda, bunge linalothibitiwa na vibaraka wa Rais Museveni lilibadilisha katiba kuondoa hitaji la umri wa wagombeaji wa urais. Hii ilimfungulia milango kiongozi huyo kuendelea kugombea urais mara nyingi atakavyo.

Utawala wake umelaumiwa kwa kukiuka haki za raia na kutumia vyombo vya usalama na mahakama kuhangaisha wapinzani.

Mnamo 2018, serikali ya Rais Nkurunziza iliandaa kura ya maamuzi iliyomruhusu aendelee kugombea urais wa Burundi hadi 2034.

Hii ilikuwa mara ya pili katiba kubadilishwa ili rais huyo aendelee kugombea urais.

Burundi imekumbwa na misukosuko ya kisiasa, ukosefu usalama na kudorora wa uchumi tangu 2015 Nkurunziza alipogombea urais kwa kipindi cha tatu.

Alipoanza kutawala Zimbabwe mnamo 1980, marehemu Mugabe alikuwa mmoja wa viongozi walioheshimika sana kwa sera zake bora.

Zimbabwe ilipigiwa upatu kuwa moja ya nchi za kuigwa barani Afrika. Hata hivyo, Mugabe alikataa kuondoka mamlakani na akaanza kutumia mbinu za kukadamiza haki za binadamu, kuwakamata, kushtaki na kudhulumu wapinzani na watetezi wa haki za binadamu ili kuendelea kutawala.

Alikataa wito wa kustaafu na aliondolewa mamlakani 2018 kwa aibu baada ya kutawala Zimbabwe kwa miaka 38.

Katika nchi ya Sudan, Bashir alikatalia madarakani kwa miaka 30 hadi alipooondolewa kwa aibu na raia waliosaidiwa na wanajeshi na akashtakiwa. Bashir alikuwa akikadamiza wapinzani wake na kuwatupa kizuizini katika juhudi za kubakia uongozini.

Katika nchi ya Rwanda, Rais Paul Kagame amekuwa mamlakani kwa miaka 20 na amefaulu kuunganisha nchi hiyo, kudumisha uthabiti wa kisiasa na kupata ufanisi wa kiuchumi. Hata hivyo, amelaumiwa kwa kukadamiza wapinzani wake.