RIZIKI: Mitandao ya kijamii inavyomfaa kufanya mauzo ya bidhaa
Na SAMMY WAWERU
FACEBOOK, Twitter, Skype, Instagram na WhatsApp, ni miongoni mwa mitandao yenye wachangiaji wengi si tu hapa nchini bali katika mataifa mengine mengi.
Ni mkusanyiko wa mitandao inayoleta watu karibu, ingawa si ana kwa ana. Kwa mfano, aliye Amerika anaweza kuwasiliana moja kwa moja na aliye hapa nchini Kenya.
Kimsingi, mitandao ya kijamii imerahisisha mawasliano, ambapo wengi wameikumbatia. Vyombo vya habari pia vinaitumia kuchapisha habari chipuka ikiwa ni pamoja na kuhoji wahusika wa matukio kupitia mawimbi.
Mfano, ni mtandao wa Skype, ambao huonesha picha kupitia video na kuandamana na sauti. Kijumla tuseme ni kuimarika kwa teknolojia na utandawazi unaoleta watu pamoja.
Mbali na kupasha ujumbe na kuelimisha, baadhi ya wachangiaji wamejihusisha kwa shughuli mbalimbali, maarufu ikiwa kupakia picha kuonesha wanachofanya, waliko na hata kuzua mitandaoni.
Aidha, kuna wanaojuana kwa njia iyo hiyo, wanachumbiana na hata kuishia kuwa mume na mke. Katika mitandao iyo hiyo, kuna matapeli.
Hata hivyo, kwa Regina Wanjiku mitandao ni sawa na ‘duka’. Mwanadada Wanjiku huitumia kufanya matangazo na mauzo ya bidhaa ja nguo, vifaa vya kielektroniki na vyombo vya mapishi na jikoni.
“Mitandao ndiyo ofisi yake, huitumia kujiendeleza kimaisha na kimapato,” adokeza, akieleza kwamba amefungua kundi kwenye Facebook na WhatsApp kwa shughuli hiyo.
Kulingana na mjasirimali huyo, anachohitaji chipukizi ni kuwa na simu ya kisasa ‘Smartphone’.
Pia, mtangulizi anapaswa kuwa na mtaji kidogo tu, kung’oa nanga kwa shughuli hiyo.
“Mtaji huo ni wa kununua bidhaa na kuweka krediti ya data,” aelezea Wanjiku ambaye ni mama wa watoto wawili. Aliingilia biashara hiyo miaka mitatu iliyopita, baada ya kujaribu biashara mbalimbali.
“Kukodi na kulipa chumba cha duka ni jambo lililonihangaisha kwani wakati mwingine ningekadiria hasara. Uchumi unaendelea kuwa ghali, utozaji ushuru, baadhi ya changamoto zinazolemaza sekta ya biashara,” afafanua Wanjiku.
Anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba utangulizi haukuwa rahisi, kwani ilimchukua muda kutumia wachangiaji ombi la kujiunga na makundi aliyofungua pamoja na kuwashawishi kuwa wateja wake. “Biashara ya mitandao inahitaji uaminifu wa hali ya juu. Matapeli wapo mitandaoni, na wateja wako makini, hivyo basi ni muhimu mfanyabiashara awe wa kuaminika,” ashauri.
Uaminifu, anamaanisha muuzaji akiagiza bidhaa mfanyabiashara awe radhi kumfikishia alizoagiza. Kuna matapeli wanaouza bidhaa hewa, Wanjiku akieleza ni miongoni mwa changamoto anazopitia wateja wakihofia kuhadaiwa. “Ninaowauzia hufahamisha wateja wenza,” asema.
Kwenye makundi, mfanyabiashara huyo huchapisha picha za mavazi na bidhaa zingine anazouza, zikiandamana na bei na nambari za simu ili kumfikia upesi. “Kuna wateja ninaowapelekea, kwa ada fulani kando na bei ya kununua. Wanaonijua hujia niliko,” asema. “Ni kazi inayohitaji uvumilivu, kwa sababu baadhi ya wachangiaji huagiza bidhaa na wanakosa kuonekana mahali tunapoagana kukutana,” asema Wanjiku.
Bw Samuel Karanja, msusi wa nywele anasema mitandao imemsaidia kuimarisha kazi yake. Alianza kama msusi tamba na baada ya kukumbatia matumizi ya mitandao kufanya matangazo, idadi ya wateja wake imeongezeka.
“Niliweza kufungua duka la kusuka, kupaka hina na rangi wanawake, baada ya mitandao kunizolea wateja,” afichua Karanja.
Kwenye ukurasa na kundi la ususi la Facebook alilofungua, Bw Karanja ameweka nambari ya simu katika ukurasa wa maelezo binafsi.
Anapochapisha picha za miundo na staili mbalimbali za ususi na huduma anazotoa, huandamabisha chapisho na nambari za simu. Kauli yake kuhusu uaminifu inawiana na ya Regina Wanjiku.
Mwaka uliopita, Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini, KRA, ilikuwa imetangaza kwamba itaanza kutoza ushuru wachangiaji wanaotumia mitandao kufanya matangazo, mauzo na bishara.
Ni hatua iliyowatia wengi kiwewe, ikizingatiwa kuwa wafanyabiashara, kampuni, viwanda na mashirika mengi hutumia mitandao kufanya matangazo na kuvutia wateja. “Ninashangaa ni ushuru upi ilhali kununua krediti tunatozwa ushuru, bila kusahau tunaotozwa kununua bidhaa,” aeleza Wanjiku.
Isitoshe, mapema mwaka huu wa 2020, serikali ilitangaza kuanza kutoza ushuru wafanyabiashara wadogo na wale wa kadri, SMEs.
Wanjiku huendea bidhaa zake katika soko maarufu la Gikomba na Kamukunji, masoko yaliyoko jijini Nairobi. Aidha, masoko hayo yanafahamika katika uuzaji wa bidhaa kwa bei nafuu.