Makala

Matapeli 'mapepo' wanavyohangaisha wakazi Limuru

January 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 5

NA MARY WANGARI

Huku gharama ya maisha ikizidi kupanda na changamoto za kupata riziki zikigeuka kitendawili kigumu, baadhi ya Wakenya wako radhi kufanya chochote kile ilmradi tu wajikimu kimaisha.

Wahalifu pia hawajaachwa nyuma katika msafara huu huku wakibuni mbinu anuai za kutekeleza uhalifu wao kuanzia matumizi ya dijitali na mbinu nyinginezo ambazo zinafanana tu na ngano za mizimwi.

Utapeli si jambo geni. Lakini utapeli huo unapofanywa kwa kutumia hirizi, mapepo au njia za kishetani, basi hapo linakuwa suala la kuhofisha mno.

Huu ndio uhalisia ambao wakazi mjini Limuru, Kaunti ya Kiambu, wanakumbana nao.

Ninapokutana na Kagendo, 24, taswira ya kwanza inayonijia kumhusu ni kwamba ni msichana mpole, mwenye heshima na mnyamavu.

Bila shaka, angali ametishika kutokana na tukio lililomsibu majuzi, jambo linalojidhihirisha wazi kutokana na jinsi machozi yanavyomlengalenga, mara tu anapoanza kunisumulia masaibu yaliyompata.

Anakumbuka kana kwamba ni jana tu Jumamosi hiyo alipotumwa na mwajiri wake kununua bidhaa za chakula sokoni.

Haikuwa mara ya kwanza kutumwa sokoni, hivyo basi Kagendo anayefanya kazi kama mjakazi Limuru, hakuwa na wasiwasi wowote maadamu alijua alichohitajika kufanya.

Mwajiri wake alimkabidhi Sh3000 pamoja na orodha ya vitu viliyohitajika na hapo akafululiza moja kwa moja hadi sokoni, akiwa na nia moja tu. Kununua bidhaa na kurejea nyumbani na kuendelea na majukumu mengine.

Hata hivyo, hakuwa tayari kwa tukio lililomsubiri ambalo bila shaka atalikumbuka kwa muda mrefu.

Zilisalia tu siku chache kabla ya Sikukuu ya Krismasi hivyo soko lilifurika watu katika pilkapilka za kununua vyakula na mavazi katika maandalizi ya sherehe.

Katika pitapita zake akielekea sokoni kabla ya kuanza kununua bidhaa, wanawake wawili waliojifunga kanga walimjia.

Walimsalimia Kagendo kwa upole huku wakimwomba awaelekeze katika jumba fulani mjini humo, lakini akawafahamisha hakufahamu eneo hilo vyema.

“Walinisalimia kwa mkono kisha wakaniomba niwaelekeze kwa jumba linaloitwa Metropolitan Sacco. Niliwaeleza kwamba pia mimi nilikuwa mgeni hivyo sikufahamu sehemu nyingi mjini humo,” anaeleza.

Baada ya kila mmoja kushika hamsini zake, binti huyo ghafla, kama aliyepagawa, alikumbuka kuna hela alizokuwa ameacha nyumbani na akashikwa na hamu isiyo ya kawaida kwenda kuzichukua, hata pasipo kujua ni kwa nini hasa alizihitaji.

“Nilimwita mwendeshaji pikipiki aliyekuwa karibu na nikarejea nyumbani kwa haraka. Nilipofika nilichukua pesa zangu zote nilizokuwa nimeweka kama akiba kwa takriban mwaka mmoja nilipokuwa nikifanya kazi zilikuwa karibu Sh30,000.

“Nilidhamiria kuwatumia wazazi wangu na kuwanunulia ndugu zangu zawadi nitakaporejea nyumbani,” anasimulia huku akisita kwa muda kufuta machozi huku akishindwa kujizuia.

Kisha aliabiri pikipiki iliyomleta maadamu mwendeshaji bodaboda huyo alimsubiri kwenye lango na kurejea sokoni akidhamiria kukamilisha shughuli iliyomsubiri.

Aliwasili sokoni tena na kwa njia ya kimiujiza ambayo Kagendo hajawahi kuelewa hadi hii leo, walikutana kwa mara nyingine na wanawake hao wawili.

“Kutoka hapo sikumbuki kilichotokea. Ninachokumbuka tu ni kwamba waliniitisha hela na nikawapa zote nilizokuwa nazo ikiwemo nilizotumwa kununulia bidhaa.

“Kisha waliniitisha simu na nikawapa hata bila kuwauliza chochote. Mwishowe nilijipata tu nikiwa nimeketi chini ya daraja nikiangalia tu hewani. Nilipotanabahi nilikuta wapita njia kadha wamenizingira,” alieleza.

Kulingana na Kagendo, juhudi za wasamaria wema kumsaidia ziliambulia patupu maadamu alikuwa hajijui hajitambui, hakuwa na simu na ilichukua muda kabla ya fahamu zake kumrudia.

“Nilianza kulia nikishangaa ni vipi nilivyoishia hapo. Nilimwomba mtu mmoja simu nimpigie mwajiri wangu aliyekuwa kazini na kumfahamisha kuhusu mashaka yaliyonipata. Kwa bahati nzuri alikuja na akanipeleka nyumbani,” alieleza Kagendo.

Kisa cha Kagendo ni mojawapo wa misururu ya visa vya utapeli usio wa kawaida, na ambao umewahangaisha wakazi wa Limuru.

Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba kwa sasa baadhi ya wakazi wanahofia kuwasalimu au kuwasaidia watu wasiowafahamu.

Siku chache tu baada ya Kagendo kutapeliwa Joel mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu mojawapo nchini kutoka eneo la Tigoni, Limuru, alitapeliwa kiasi cha Sh8,000 alizodhamiria kulipa nazo karo.

Sawa na Kagendo, Joel alikuwa akielekea chuoni anamosoma alipokutana na mwanamke mmoja aliyemsalimia kwa unyenyekevu na kumwomba amwelekeze katika duka mojawapo eneo hilo.

Kama mwenyeji eneo hilo na bila kushuku chochote, Joel alijitolea kumsaidia mwanamke huyo na kisha aende zake.

“Mambo yalitendeka haraka sana hadi sasa mimi huona kama ni ndoto. Baada ya kunisalimia na tukaandamana pamoja, nakumbuka tu akiniitisha pesa nami nikampa zote nilizokuwa nazo bila pingamizi lolote,”anasimulia huku akicheka kwa kutoamini.

Kwa Maryam ambaye ni mkazi wa Limuru vilevile, nyota ya jaha ilikuwa upande wake maadamu alinusurika kwa tundu ya sindano kutapeliwa kiasi cha zaidi ya Sh40,000 alipokutana na washukiwa hao.

“Ilikuwa siku ya Jumapili ambapo niliamua kupitia sokoni baada ya kuhudhuria ibada kanisani. Mshahara ulikuwa umeingia hivyo nilienda kwanza kwenye mtambo wa hela kisha nikaelekea sokoni,” anaeleza.

Mama huyo wa watoto watatu hakuwa na habari kuhusu hatari iliyokuwa ikimkondolea macho.

“Nilipokuwa nikielekea kwenye kibanda mojawapo kununua mboga, nyanya na vitunguu, wanawake wawili walinijia ghafla. Sikuwa nimewaona mbele yangu, ni kama walichipuka tu. Kwanza nilimwona mmoja aliyenisalimia na kuniomba niwaelekeze mahali ambapo wanaweza kupata viatu aina ya ‘boots’,”

“Baadaye nilimwona mwenzake kando yake. Sijui ni vipi lakini niligutuka na nikakumbuka ghafla nilikuwa nimebeba kiasi kikubwa cha hela. Pia nilijisaili kimoyomoyo, iweje katika soko lote ni mimi tu walikuwa wameona wa kuuliza. Iweje walitoka mwendo wote huo na kunijia mimi huku kukiwa kumejaa wateja na wauzaji kwenye vibanda sokoni?

“Niliwaeleza sijui na kuwaondokea haraka. Ni kama hata hao waligundua kuna jambo lilikuwa limetendeka. Waliondoka na kutoweka ghafla sawa tu na walivyoibuka,” anasimulia Maryam huku akimshukuru Maulana kwa kumnusuru siku hiyo.

Hata hivyo kuna baadhi ya wakazi wanaoamini kwamba matapeli hao si wa kawaida na kwamba wanatumia nguvu za kishetani kuwalenga na kuwapumbaza wahasiriwa wao na kisha kuwaibia mchana peupe.

“Ni kama wanatumia nguvu za mapepo kuwaongoza kwa wahasiriwa wao. Mara tu unapowagusa ama kuzungumza nao unajisahau na kufanya chochote wanachokuagiza kufanya,” anaeleza Mama Ian ambaye ni muuzaji katika soko la Limuru.

Siku za wahalifu hao hata hivyo zimehesabiwa huku wakazi wenye ghadhabu wakililia damu yao na kuapa kumpa kichapo cha mbwa yeyote atakayepatikana na bahati mbaya ya kukamatwa.

“Lakini kwa sababu kuna siku tutawakamata, hiyo ndiyo siku watajutia kwa dhati vitendo vyao. Tunaomba na tunajua Mungu halali kuna siku watafumaniwa hadharani,” anaeleza mfanyabiashara mmoja huku akiwa amejawa na machungu.

Visa vya matapeli si vipya mjini Limuru huku wahalifu hao wakitumia mbinu za kila aina ikiwemo watoto huku baadhi ya visa vikiweza hata kuwafanya watengenezaji tajika wa filamu duniani kuwaonea gere kwa ustadi wao.

Mnamo Julai 2019, wasichana wawili mmoja aliyejifanya kuugua kifafa na mwingine akisingizia kuwa dadake walikuwa wakiwalenga waendeshaji magari kwenye barabara kati ya Limuru hadi Nairobi.

“Mmoja wao alikuwa akijifanya amezirai na kulala barabarani ili kuvutia wasamaria wema. Karibu wanitapeli eti niwape hela za matibabu kabla ya dereva aliyekuwa amewaona hapo awali wakiwatapeli watu kwenye barabara ya Kiambu aliponitahadharisha kuondoa upesi kabla sijanaswa mtegoni,” anasimulia Nicholas Kareu.

“Wanawake hao huchanganya mtu. Unajipata wametumia kifaa cha kusaidia kupumua (inhaler) unajisahau unawapatia kila kitu,” anaonya Magecha.

Ikiwa hilo halijakushtusha basi hujasikia kisa mojawapo 2018 ambapo mwanamme mmoja aliyekuwa akijifanya kuwa kasisi kutoka Benedictine Monastery, alikuwa akiwatapeli wafanyabiashara Limuru.

Kasisi huyo feki kwa jina Kasisi Edward alikuwa vilevile akisingizia kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Katoliki ili kuwarushia chambo wahasiriwa wake ambapo alimtapeli muuzaji dawa mmoja kiasi cha Sh500,000.

Mwaka uo huo kuliripotiwa visa vya wasichana matapeli waliokuwa wakisingizia kusaka kazi za ujakazi na kisha kufagia vitu vya nyumbani na kutoweka baada ya siku chahe.

Ni hali hii ya kuongezeka kwa matapeli mjini Limuru ambayo imefanya baadhi ya watu kushangaa nini hasa kiini chake.

Jinsi wanavyotania baadhi ya watu, huenda ni hali ya anga yenye baridi shadidi, ukungu na barafu ambayo eneo hilo linalosifika kwake, ndiyo inayochangia pakubwa kwa kuwapa maficho mwafaka wahalifu hao.

[email protected]