• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Wanyama hajaniambia anataka kuhama – Mourihno

Wanyama hajaniambia anataka kuhama – Mourihno

Na GEOFFREY ANENE

HUKU Tottenham Hotspur ikijiandaa kualika Liverpool kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Jumamosi usiku, habari kutoka uwanjani Tottenham zinasema Victor Wanyama hajasema wazi kama anataka kuhama ama la.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya amehusishwa na klabu za AC Milan (Italia), West Ham United na Norwich (Uingereza), Celtic (Scotland), Galatasaray (Uturuki) na sasa Lyon nchini Ufaransa.

Hata hivyo, kocha wa Tottenham Jose Mourinho, ambaye aliwahi kufanya kazi na kakake Wanyama, McDonald Mariga miaka iliyoenda katika klabu ya Inter Milan nchini Italia, amekunuliwa na vyombo vya habari nchini Uingereza akisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hajatangazia klabu hiyo msimamo wake.

“Yeye (Wanyama) ni mchezaji wetu. Ikiwa anataka kuondoka ama la, hajaniambia. Hatujajadiliana chochote,” ripoti hizo zinasema.

Tottenham imekuwa ikitaka kuuza Wanyama kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa na hata kumfikisha sokoni mwezi Agosti. Wakati huo, alihusishwa na klabu kadha nchini Uingereza pamoja Galatasaray na Fenerbahce kutoka Uturuki kabla ya Club Brugge kutoka Ubelgiji kuonyesha nia ya kumsaini.

Hata hivyo, uhamisho kutoka Tottenham hadi Brugge ulifeli dakika ya mwisho na Wanyama akasalia mchezaji wa Spurs chini ya kocha Mauricio Pochettino.

Kocha huyo kutoka Argentina alimtumia katika mechi mbili pekee za ligi za msimu huu wa 2019-2020 ambazo ni dhidi ya Leicester (dakika 23 mnamo Septemba 21, 2019) na Southampton (dakika moja mnamo Septemba 28, 2019).

Baada ya Pochettino kutimuliwa, kocha mpya Mourinho amemchezesha dakika tisa pekee dhidi ya Bayern Munich kwenye Klabu Bingwa Ulaya.

Mashabiki wa Tottenham wamekuwa wakitaka Wanyama auzwe kutokana mchango wake kudidimia baada ya kusumbuliwa na majeraha. Walimsifu sana alipojiunga na Tottenham kutoka Southampton msimu 2016-2017, lakini majeraha yamefanya akose mechi nyingi na pia kuorodheshwa chini katika viungo ambao klabu hiyo kutoka jijini London inatumia katika idara hiyo.

You can share this post!

Uzembe wa Seneti huenda ukamnusuru Waititu

Tangatanga walaani serikali kufungia Ruto nje ya makazi

adminleo