KSG Ogopa wabanwa na South C United

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya WYSA United ilibamiza Kemri FC kwa mabao 2-0 na kurukia usukani wa kipute cha kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.

Nao vijana wa KSG Ogopa FC waliopigiwa chapuo kupiga mtu na kutwaa uongozi wa kipte hicho waliteleza na kutoa nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya South C United katika uwanja wa KSG jijini Nairobi.

KSG ilitupia kambani mabao hayo kupitia Kelvin Ndung’u na Seby Kivairo.

WYSA iliteremka dimbani kwa kusudi moja kutesa wapinzani wao na kutia kapuni alama tatu muhimu. Kemri imeshiriki kipute hicho kwa misimu kadhaa lakini inahitaji kujitathimini ili kufanya kweli.

WYSA ilizoa mafanikio hayo baada ya Denis Atsenge na Kelvin Etemesi kila mmoja kucheka na wavu mara moja. Nayo Parklands Sports iliichapa Uthiru Vision mabao 2-1 yaliyojaza kimiani na Caleb Cisco huku Collins Alphonse akifungia Uthiru bao la kufuta machozi.

Nao Nelson Mandela na Henry Api kila mmoja alipiga kombora moja safi na kubeba Silver Bullets kucharaza KYSA Karengata mabao 2-0.

Katika matokeo hayo, KFS ilizabwa 2-1 na South B United, Maafande wa Nairobi Prisons walipiga Kibera Soccer goli 1-0 lililofumwa kimiani na Gabriel Gabu.

MAA FC ilichapawa mabao 2-0 na Kibera Lexus nayo Dagoretti Lions iliagana sare ya bao 1-1 na Riruta United (Makarios 111 FC). WAYSA inaongoza kwa alama 15, moja mbele ya KSG Ogopa sawa na Kibera Saints tofauti ikiwa idadi ya mabao.