Kalonzo akataa ndoano ya Ruto kuwa naibu wake
Na PIUS MAUNDU
KINARA wa chama cha Wiper, Stephen Kalonzo Musyoka ametofautiana hadharani na Naibu Rais William Ruto, kuhusiana na urais mwaka 2022.
Wawili hao wakiwa kwenye mazishi ya Mama Rael Mbeleete Mailu, mamake aliyekuwa Waziri wa Afya Dkt Cleopha Mailu, Bw Musyoka amekemea Jumamosi jaribio la Dkt Ruto na wafuasi wake kumtaka aungane naye ili awe mgombea mwenza.
“Nimejitolea kushirikiana na Rais Kenyatta, kama nilivyomhakikishia wakati wa mazishi ya marehemu babangu mwaka 2019. Baada ya uongozi wa Rais Kenyatta, hakuna atakayenizuia kumrithi,” akasema Bw Musyoka.
Dkt Ruto alikuwa amerusha chambo kupitia Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen na Dkt Victor Munyaka (Machakos Mjini).
“Bw Musyoka anapaswa kushirikiana na Dkt Ruto sawa tu anavyofanya kazi pamoja na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Wanapaswa kubuni muungano ambao utawawezesha kubuni serikali ijayo,” akasema Bw Murkomen.
Yeye na Bw Munyaka walimrai wazi Bw Musyoka atathmini uwezekano wa kushirikiana na Dkt Ruto, ili wabuni serikali baada ya uchaguzi wa 2022.
Na aliposimama kuzungumza, Dkt Ruto alimwonya Bw Musyoka dhidi ya kuweka matumaini makubwa, kwenye malengo yake ya kisiasa.
“Bw Musyoka anapaswa kuwa na mtazamo mpana kwenye malengo yake. Anapaswa kujihadhari asipotoshwe na baadhi ya waandani wake, ambao lengo lao ni kumtumia kama jukwaa la kushinda nyadhifa za kisiasa.”
Dkt Mailu ambaye ni balozi wa Kenya nchini Uswisi, alimuomboleza mamake aliyefariki akiwa na umri wa miaka 90, kuwa mtu aliyeipenda familia yake.
“Mamangu alikuwa mwanamke mwenye nguvu, aliyeunganisha familia yake. Alitupenda sana kama familia,” akasema.
Dkt Ruto alisoma ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo alimsifu kama mwanamke aliyekuwa mfano wa kuigwa na wengi.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos Bw Johnstone Muthama na mfanyabiashara Jimmy Wanjigi.