RIZIKI: Wanjiru sasa afurahia bidii yake katika uwekezaji
Na SAMMY WAWERU
BI Monicah Wanjiru anakumbuka barabara kana kwamba ilikuwa jana tu, miaka 15 iliyopita, ndoa yake ilipoanza kuingia doa.
Kilichoanza kama mzaha kilitunga usaha, “mume wangu wa miaka kadha kuanza kufika akiwa amechelewa usiku”.
Akivuta mawazo nyuma, kati ya mwaka wa 2005 – 2007, Wanjiru alitetea kwa hali na mali kunusuru ndoa hiyo iliyokuwa ingali changa. Wakati huo, walikuwa wamejaaliwa mtoto mmoja, mwanambee – yaani kifungua mimba.
Hata hivyo, juhudi zake zikawa mithili ya kuchezea mbuzi gitaa, akieleza aliona ni sawa na kujaribu kujaza gunia maji. “Nilitamani niwe na familia, tujaaliwe watoto na tuwalee kwa msingi wa kidini, kumuogopa Mwenyezi Mungu,” Wanjiru asimulia.
Usililojua ni kama kumtafuta paka mweuzi gizani bila kurunzi, hakujua kilichobadilisha mume wake ghafla, mapema aliyozoea kujiunga na familia yake kula chajio, ikawa saa nne, ikaenda saa sita, saa nane, saa tisa na hatimaye kuingia alfajiri na mapema.
Wanjiru anasema alikuwa akija kukoga na kubadilisha mavazi pekee, hata kiamsha kinywa asile.
Kinachouma mke, ni kuandalia mume wake chakula kisha anakosa kula. “Ni mojawapo ya visababishi vya ndoa kusambaratika. Mume anayejali mke wake, anapaswa kula alichomuandalia,” Leah Wairimu, daktari na mshauri wa masuala ya ndoa na kifamilia anasema.
Hayo ndiyo masaibu yaliyozingira Monicah Wanjiru, kilele kikawa kutemwa nje. Katika pilka pilka za kujaribu kuteka hisia na mawazo ya mume, tayari alikuwa na ujauzito, wakawa na watoto wawili kwenye kapu la ndoa.
Hakuwa na budi ila kuondoka, kwa minajili ya kujitafutia amani yake yeye pamoja na malaika wake, aliojaaliwa.
“Maisha yalikuwa magumu, hasa kutalakiwa bila chochote mfukoni,” akumbuka Wanjiru.
Anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba alianza biashara ya uchuuzi wa nguo ambapo alikuwa akiziendea katika soko la Gikomba lililoko jijini Nairobi.
“Nilikuwa ‘mama na baba’ ya watoto wangu, na lazima ningetafuta cha kutia kinywani na hatimaye kiingie tumboni. Kwa neema za Mungu, mama mzazi hakuniachilia bali alinishika mkono kwa kupokea watoto wangu,” aelezea.
Ulikuwa uchuuzi kutoka boma moja hadi jingine, soko moja hadi jingine. Biashara ilinoga, na ni katika harakati hizo mnamo 2010 alikutana na rafikiye aliyefanya kazi ughaibuni, akamfungua macho.
Alikuwa akisukumia gurudumu la maisha, katika mojawapo ya falme za Kiarabu, Dubai iliyoko UAE. Dubai ni mji tajika katika shughuli za biashara na kivutio cha utalii.
Wanjiru anasema kwamba rafikiye alimtafutia gange humo, ikawa nyota ya jaha, hatua anayosimulia kuwa ilibadilisha maisha yake.
“Nilibahatika kupata kazi katika duka moja ambapo nililipwa zaidi ya Sh70,000 ambapo malipo yaliongezeka kila mwaka,” afichua.
Anaeleza kuwa nina yake alishirikiana naye sako kwa bako, kumtunzia watoto na wazo lake katika uwekezaji wa nyumba za kukodi.
Miaka mitano baadaye, Wanjiru katika mojawapo ya likizo humu nchini, alifanya ziara eneo la Zimmerman, Nairobi ambapo alikutana na mmoja wa mwekezaji nyumba za wapangaji kuishi kwa kulipia kodi.
Ni hapo ndipo alipata fursa ya kuonyeshwa mradi wa mwekezaji huyo na anaosema ulimpa mapato ya kuridhisha.
Alirejea nyumbani akiwa na wazo lililomkuna kichwa, “uwekezaji ambao unahitaji maelfu ya pesa na nikiufanikisha nitafurahia matunda yake siku za usoni”.
Baada ya mazungumzo ya kina na mama yake, Wanjiru anasema waliafikiana kuchukua hatua nyingine; kutafuta ploti. Hatimaye waliipata, eneo la Zimmerman, akainunua kupitia akiba aliyoweka kibindoni na shughuli za ujenzi zikaanza.
“Mama ndiye alisimamia mradi huo, hata ingawa ulitugharimu hatujutii kamwe,” anasema. Wanjiru, anasema alijinyima mengi, ikiwamo starehe ili kufanikisha mradi wa nyumba hizo za kupangisha.
Mchumia juani hulia kivulini, baada ya kukamilisha, Wanjiru alirejea nchini 2018 ili kuendeleza azma yake, akifichua kwamba anapania kununua ploti maeneo mengine, kwa kuwa biashara ya nyumba za kupangisha inalipa.