• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Uvamizi wa nzige nchini hatari kwa mazingira na afya

MAZINGIRA NA SAYANSI: Uvamizi wa nzige nchini hatari kwa mazingira na afya

Na LEONARD ONYANGO

NZIGE waliovamia baadhi ya sehemu nchini waweka Kenya katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa, magonjwa na uharibifu mazingira.

Wataalamu sasa wanaonya kuwa kemikali zinazotumiwa kiholela na wakazi wa kaunti zilizoathiriwa na nzige huenda zikageuka kuwa chanzo cha maradhi hatari kama vile kansa.

Wanasema nzige pia watasababisha uhaba wa chakula humu nchini hivyo kutoa mwanya kwa mkurupuko wa maradhi yanayohusiana na lishe duni.

Kulingana na mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Wadudu (ESK) Dkt Muo Kasina, wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa wamekuwa wakinunua kemikali na kuzitumia kufukuza nzige bila kufuata maelekezo.

Dkt Kasina anasema kuwa huenda wakazi wakatumia kemikali nyingi kupita kiasi na kusababisha uharibifu wa mazingira na kuhatarisha afya zao.

Miongoni mwa Kaunti ambazo zimevamiwa na nzige ni Mandera, Wajir, Marsabit, Isiolo, Garissa, Meru na Laikipia.

Hata hivyo, anasema kuwa kemikali zanazonyunyizwa na serikali kwa kutumia ndege ni salama.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula (FAO) limeidhinisha mchanganyiko huo maalumu unaofahamika kama Ultra-Low Volume (ULV) na ndio njia ya pekee ya kukabiliana na wadudu wa kuhamahama kama vile nzige.

“Mchanganyiko wa kemikali hizo hunyunyizwa hewani. Nzige hupumua hewa hiyo na kufa papo hapo. Kiasi cha kemikali inayofika ardhini ni kidogo mno na hukauka ndani ya wiki moja. Mchanganyiko huo ni salama kwa afya ya binadamu na mazingira,” anasema Dkt Kasina.

“Kemikali inayonyunyizwa na ndege haina shida. Tatizo ni kemikali zinazonyunyizwa na watu kiholela. Kunyunyiza kemikali kwenye mimea hakuwezi kufukuza nzige,” anasema Dkt Kasina.

Kutokana na ukosefu wa mbinu mwafaka ya kuwafukuza nzige hao, wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa wamekuwa wakijaribu kila aina ya njia.

Katika baadhi ya maeneo, wakazi wanapiga kelele, kugonga masufuria au mabati na hata kupiga firimbi.

Polisi wamekuwa wakifyatua risasi hewani na hata kutumia vitoa machozi kuwafukuza nzige hao.

Baadhi ya wakazi pia wamelazimika kusoma Koran kama njia mojawapo ya kuwafukuza wadudu hao wanaosababisha uharibifu mkubwa.

Wengine wanafukuza wadudu hao kwa kuwanyunyizia kemikali.

Shirika la Kudhibiti Nzige Afrika Mashariki linasema kuwa nzige waliovamia Kenya hawajakomaa. Linasema nzige waliokomaa wako katika eneo la Garbahare karibu na Mandera.

Wataalamu wanasema kuwa huenda Kenya ikawa na kibarua kigumu kukabiliana na nzige hao iwapo wataachwa wakomae. “Nzige hao wanafaa kuangamizwa na kufukuzwa wangali wachanga. Wakikomaa watasababisha uharibifu mkubwa zaidi,” anasema Dkt Kasina.

Kulingana na shirika la Afya Duniani (WHO), baadhi ya kemikali za kunyunyizia mazao ni hatari kwa afya na mazingira iwapo zitatumiwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa mfano, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa kemikali za kunyunyizia mazao zilizo na viungo vya dichlorodiphenyltrichloroethane (DDT) zinaweza kusalia ardhini na ndani ya vyanzo vya maji kwa zaidi ya miaka 20.

Kemikali zilizo na DDT tayari zimepigwa marufuku katika mataifa mbalimbali ambayo yalitia saini Mkataba wa Stockholm mnamo 2001. Mkataba huo unalenga kumaliza kemikali ambazo ni hatari.

Kemikali za DDT zinapoingia mwilini husababisha matatizo ya ini na mfumo wa uzazi.

Kulingana na Bodi ya Kudhibiti Matumizi ya Kemikali za Kunyunyizia Wadudu (PCPB), kemikali zilizo na kiasi kidogo cha DDT zilizoruhusiwa humu nchini ni ACARIN T 285 EC na APCOTHION EC. Kemikali hizo hutumiwa kuua wadudu kwenye pamba.

Wataalamu wanaonya kuwa iwapo wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa watatumia kemikali hizo hatari kufukuza nzige watahatarisha afya zao kwani mvua inaponyesha huingia kwenye vyanzo vya maji.

Eneo la kilomita moja linaweza kushambuliwa na nzige 50 milioni ambao hula tani 100 za mimea. Nzige wanaweza kuathiri eneo kubwa ndani ya muda mfupi.

Shirika la FAO linasema kuwa nzige wanaweza kusafiri kilomita 130 kwa siku.

Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), linasema kuwa kundi moja linaweza kuwa na nzige milioni 80.

Mbali na Kenya, nzige hao pia wamevamia Ethiopia, Somalia, Djibouti, Eritrea na Sudan.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la masuala ya hali ya anga la Pan-African Climate Justice Alliance (PACJA), Mithika Mwenda analaumu serikali kwa kuzembea katika maandalizi ya kukabiliana na nzige.

“Shirika la FAO lilionya mnamo Juni 2019 kuhusu uwezekano wa nzige kuvamia Kenya na mataifa mengine jirani. Lakini serikali haikuweka mikakati yoyote ya kukabiliana na nzige hao,” anasema Bw Mwenda.

Shirika la FAO lilitoa onyo hilo baada ya wadudu hao kuvamia Saudi Arabia, Yemen na India mwaka jana.

Shirika hilo lilisema kuwa nzige walikuwa wamezaana kwa wingi kati ya Juni 2018 na Machi 2019 katika baadhi ya maeneo ya Saudi Arabia.

“Nzige wameisababishia Kenya masaibu zaidi kwani tungali tunauguza majeraha yaliyosababishwa na mafuriko, ukame ulioshuhudiwa mwanzoni mwa mwaka jana, maporomoko ya ardhi, kati ya athari nyinginezo zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi,” anasema.

You can share this post!

TEKNOHAMA: Uraibu unaduwaza wauguzi kazini

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nahisi uchungu mwingi baada ya...

adminleo