HabariSiasa

Miguna akunja mkia na kurudi Canada

January 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI Miguna Miguna Jumanne alikunja mkia na kuamua kurudi Canada baada ya kukwama Ujerumani kwa siku 16, kufuatia hatua ya serikali kumzuia kurejea nchini.

Bw Miguna alitangaza uamuzi huo huku Mwanasheria Mkuu, Paul Kihara Kariuki akieleza Mahakama Kuu kwamba Serikali haijamkataza kurejea nchini.

Wakili huyo alifukuzwa nchini na Serikali mnamo 2018 kutokana na msimamo wake wa kisiasa ikidai hakuwa raia wa Kenya mbali wa Canada.

Maafisa wa Serikali walimfukuza Bw Miguna nchini kwa mabavu licha ya mahakama kuagiza akubaliwe kukaa Kenya.

Kupitia mtandao wa Twitter, Dkt Miguna alisema: “Nimechoka kusubiri maafisa wakuu serikalini watii maagizo ya mahakama ndipo nirudi Kenya bila vikwazo. Sina budi ila kurudi Canada ninakoishi. Sitachoka kupigania haki yangu. Mapambano yanaendelea!”

Bw Kariuki alisema katika ripoti iliyowasilisha kortini kwamba muda wa pasipoti ya Dkt Miguna kutumika uliisha Machi 23, 2019 na hivyo alitakiwa kuomba pasipoti mpya ama atumie kitambulisho chake cha kitaifa kuingia nchini.

Alipowasili Berlin mnamo Januari 7, 2020 alipata serikali ya Kenya ilikuwa imetoa onyo kwa mashirika ya ndege kutomsafirisha hadi Nairobi.

Bw Kariuki aliwatetea maafisa wa serikali na kumlaumu Dkt Miguna kwa masaibu yaliyompata.

“Naomba mahakama itilie maanani mfumo wa kisheria unaopaswa kufuatwa katika utoaji wa pasipoti. Dkt Miguna hajaomba pasipoti mpya baada ya ile yake kuisha muda wake Machi 23, 2019,” akasema Bw Kariuki.

Wakili wa Serikali, Bw Emmanuel Mbita, jana aliwapiga chenga mawakili wa Dkt Miguna, Dkt John Khaminwa na Harun Ndubi kwa kuwasilisha ripoti ya Bw Kariuki mbele ya Jaji Weldon Korir bila kuwaarifu. Kitendo hicho kiliwaudhi mawakili hao na wale wa Tume ya Haki za Binadamu nchini (KHRC).

Mawakili hao walilalamikia Jaji Korir wakisema kesi hiyo ilikuwa imeorodheshwa kutajwa saa tano jana lakini Bw Mbita akajificha na kuomba korti itenge sik mpya ya kusikizwa.

Wakili Khaminwa alisema atawasilisha ombi leo kuhusu tabia hiyo ya afisi ya mwanasheria mkuu.

Bw Mbita aliomba mahakama itenge kesi hiyo kusikizwa Machi 23, 2020.