Uhuru aiga Moi kuzima wakosoaji
Na MWANDISHI WETU
RAIS Uhuru Kenyatta ameiga mbinu za mlezi wake wa kisiasa, Rais Mstaafu Daniel Arap Moi kuwazima wanaokosoa utawala wake hasa wanasiasa.
Kati ya mbinu hizo ni kulemaza upinzani, kuwafuta kazi wanaoonekana kwenda kinyume na matakwa yake, kuvunjwa kwa mikutano ya kisiasa, kutumia polisi kuwanyanyasa na kuwatisha wakosoaji pamoja na kuanzisha uchunguzi wa madai ya uhalifu dhidi yao mara wanapoanza kukosoa utawala wake.
Rais Kenyatta sawa na Mzee Moi amefanikiwa kuhakikisha upinzani umekuwa dhaifu kwa kuwavuta wabunge wa upinzani upande wake alivyofanya Rais Kenyatta aliporidhiana na viongozi wa upinzani Raila Odinga na Kalonzo Musyoka.
Wakati wa utawala wake wa miaka 24, Mzee Moi alikuwa akiwafuta maafisa wa serikali kiholela kila alipohisi walikuwa wakikosoa utawala wake, sawa na alivyofanya Rais Kenyatta wiki iliyopita alipomfuta kazi aliyekuwa waziri wa kilimo, Mwangi Kiunjuri.
Ingawa awali alikuwa amemuonya Bw Kiunjuri kuhusu usimamizi wa sekta ya kilimo pamoja na sakata katika wizara, Rais hakumchukulia hatua hadi alipoanza kukosoa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na kutangaza wazi anaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.
Mnamo Jumatatu wiki hii Bw Kiunjuri alihojiwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu baadhi ya sakata hizo ambazo zilisahaulika alipokuwa ndani ya serikali.
Chini ya utawala wa Mzee Moi, waliokosoa maamuzi yake walichukuliwa kuwa maadui wa serikali, walihangaishwa na maafisa wa polisi na hata kufunguliwa mashtaka na kutupwa jela ili kuwafunga midomo.
Kwa wale walioonyesha uaminifu kwake, Mzee Moi aliwatunuku vyeo na fursa zingine, lakini mara walipoanza kukosoa maamuzi ama sera zake waliona cha mtema kuni. Rais Kenyatta ameiga mbinu hii kwa wandani wake wanaomkosoa kama vile mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.
Mbali na kukamatwa na kulala seli kwa siku mbili kwa madai ya kupiga mwanamke, Bw Kuria, ambaye amekuwa akikosoa sera za Rais Kenyatta, ameanza kuchunguzwa kwa madai ya kutoa zabuni za miradi ya hazina ya eneobunge lake (CDF) kwa watu wa familia yake katika kipindi chake cha kwanza akiwa mbunge.
Madai hayo hayakuibuka wakati ambao Bw Kuria alikuwa mtetezi mkuu wa utawala wa Jubilee.
Sawa na ilivyokuwa chini ya utawala wa Moi, utawala wa Rais Kenyatta umekuwa ukivunja mikutano ya kisiasa ya wanaopinga na kukosoa serikali kufuatia “amri kutoka juu”.
Katika kisa cha hivi punde, polisi walifuta mkutano mjini Mumias wa wabunge na wanasiasa wa eneo la Magharibi waliopinga mkutano wa BBI katika uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega.
Ingawa walikuwa wamewapa wabunge hao kibali cha kuandaa mkutano huo, duru zilisema baadaye waliamrishwa kuupiga marufuku na kuhakikisha haujafanyika.
Wanaharakati wanasema kutumia polisi kuvunja mikutano ya amani na kukandamiza uhuru wa kukutana, kujieleza na kushirikana ni ukiukaji wa Katiba.
Hali ilikuwa hivyo chini ya utawala wa Mzee Moi ambapo alikuwa akitumia maafisa wa usalama kutisha na kuwaandama waliomkosoa.
Mzee Moi pia alikuwa akiwapokonya walinzi maafisa wa serikali wakiwemo wabunge na mawaziri walitofautiana naye kama njia moja ya kuwatisha.
Wiki hii wabunge kadhaa akiwemo Bw Kuria na Kimani Ngunjiri (Bahati), ambao ni wakosoaji wakubwa wa Rais Kenyatta, walipokonywa walinzi na leseni zao za kumiliki silaha zikafutiliwa mbali.
Rais Kenyatta pia ameiga mlezi wake kisiasa katika vita dhidi ya ufisadi, ambapo anaapa kujitolea kukabili uovu huo na wakati huo huo utawala wake unachukua hatua za kulemaza Idara ya Mahakama, ambayo ina jukumu kubwa katika kupiga vita wizi wa mali ya umma.
Jubilee imelaumiwa kwa kulemaza vita dhidi ya ufisadi kwa kupunguzia mahakama pesa na kukosa kuidhinisha uteteuzi wa majaji licha ya kusisitiza kuwa serikali imejitolea kupambana na uovu huo.
Mbinu nyingine ni kutengwa kwa wakosoaji wa serikali kama ilivyofanyika wiki jana Mbunge wa Bahati David Gikaria na Seneta Susan Kihika wa Kaunti ya Nakuru walipozuiwa kuhudhuria mkutano wa Rais uliofanyika Nakuru.