Michezo

Umbro yazuru kambi ya Gor na kupokeza wachezaji jezi

January 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

USIMAMIZI wa kampuni ya kutengeneza mavazi ya michezo ikiwemo soka, Umbro, umeahidi kuheshimu na kutimiza malengo yote yaliyoko kwenye mkataba wa miaka mitatu.

Kampuni hiyo ilitia saini mkataba huo unaokisiwa kuwa na thamani ya Sh45 milioni na Gor Mahia wiki iliyopita.

Maafisa wa Umbro, Jumanne walizuru kambi ya mazoezi ya K’Ogalo uwanjani Camp Toyoyo ambapo walimiminia timu hiyo sifa tele, wakiitaja kama moja wapo ya klabu ambazo wamekuwa wakiazimia kushirikiana nayo kibiashara na kwenye ulingo wa soka.

Mwenyekiti wa Umbro tawi la Afrika Kusini, Brian Katzen aliwaongoza wenzake kuwapa wachezaji jezi na vifaa vingine huku wakiahidi kwamba wanalenga kuleta jezi 10,000 wiki ijayo kwa mashabiki wa K’Ogalo.

“Sisi tumefikia hapa kuona namna ambavyo tunaweza kufanikisha udhamini huu kwa kuhakikisha wachezaji, benchi ya kiufundi na mashabiki wa timu wanatimiziwa mahitaji yote ya mchezo wa soka,” akasema Katzen.

“Jezi 10,000 zitaletwa nchini kutoka Afrika Kusini wiki ijayo, na tunalenga kuhakikisha kwamba makubaliano haya ya miaka mitatu yanainufaisha Gor Mahia na kuisadia kupiga hatua kwenye mchezo wa soka,” akaongeza.

Naibu Mwenyekiti wa K’Ogalo, Francis Wasuna ambaye alihudhuria hafla hiyo, naye alihakikishia Umbro kwamba mashabiki wa Gor watavumisha nembo yao kote nchini na akichangamkia ufadhili huo na kusema umefanyika wakati unaostahili.

“Umbro ni kampuni ya soka inayotambuliwa kote duniani na tuna furaha kwamba walikubali kufadhili timu yetu. Ufadhili huu umekuja kwa wakati ikizingatiwa klabu imepitia hali ngumu tangu kujiondoa kwa SportPesa mwaka 2019,”

“Tumewaleta hapa ili wajionee uga wetu wa mazoezi ndipo pia wawe na nia ya kuwekeza kwenye miundomsingi ya kuifaa timu yetu,” akasema Wasuna.

Kocha wa Gor Mahia, Steven Polack naye aliwaongoza wachezaji na benchi ya kiufundi kukaribisha udhamini wa Umbro, akiahidi kwamba watavuma uwanjani na kushinda mataji mbalimbali kwa kuwa wachezaji watakuwa na motisha mishahara yao ikilipwa kwa wakati.

“Umbro ni kampuni kubwa na mimi binafsi nimewahi kufundisha timu ambazo zinadhaminiwa na kampuni hii. Kazi sasa ni kuwajibika uwanjani na kushinda mataji. Tumepitia uchechefu wa kifedha na ufadhili huu ni afueni kwetu,” akaongeza.