• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Njonjo aadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa

Njonjo aadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa

Na WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa kwanza nchini, Bw Charles Njonjo anaadhimisha miaka 100 Januari 23, 2020 ikiwa hatua kubwa miongoni mwa watu wengi wa kizazi chake.

Alizaliwa Januari 23, 1920 wakati Kenya ikiwa bado chini ya utawala wa mkoloni Mwingereza. Aidha, siku yake ya kuzaliwa ilikujia miaka miwili baada ya kukamilika kwa Vita vya Kwanza vya Duniamnamo 1918.

Charles Njonjo alihudumu kama Mwanasheria Mkuu kati ya 1963 na 1980, katika tawala za marais Mzee Jomo Kenyatta na Daniel Moi.

Anakumbukwa kuwa mmoja wa viongozi wachache walio hai, wenye kumbukumbu pevu kuhusu harakati za kuundwa kwa serikali ya kwanza na Mzee Kenyatta mnamo 1963.

Hii ikizingatiwa kwamba alikuwa miongoni mwa maafisa waliohudumu katika serikali hiyo, yeye kama Mwanasheria Mkuu.

Bw Njonjo pia atakumbukwa sana kwa mchango mkubwa aliotoa kuhakikisha Bw Moi ametwaa urais, baada ya kifo cha Mzee Kenyatta mnamo 1978.

Hii ni baada ya kuibuka kwa kundi la “Change the Constitution Movement” lililoshirikisha wanasiasa kutoka eneo la Kati ambao walitaka kumzuia Bw Moi asimrithi hayati Mzee Kenyatta, kwa kushinikiza mageuzi ya kikatiba.

Kundi hilo lilijumuisha wanasiasa Kihika Kimani, Dkt Munyua Waiyaki, Njenga Karume kati ya wengine.

Hata hivyo, licha ya juhudi zao Bw Njonjo alisimama kidete na kusema kuwa atahakikisha Bw Moi amemrithi Mzee Kenyatta kulingana na taratibu za kisheria.

Kando na hayo, Bw Njonjo atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa watu maarufu waliochunguzwa na serikali ya Bw Moi kwa tuhuma za kuhusika kwenye jaribio la mapinduzi mnamo 1982.

Haya yalijiri baada ya Mzee Moi kubuni tume maalum ya kumchunguza kutokana kwamba alikuwa Waziri wa Masuala ya Kikatiba wakati wa jaribio hilo hilo la mapinduzi.

Kama sehemu ya maadhimisho yake ya kutinga miaka 100 tangu kuzaliwa, Bw Njonjo alifanya matembezi Jumapili iliyopita katika Mbuga ya Wanyama ya Mgahinga nchini Uganda kuwatega sokwe. Huu umekuwa uraibu wake kwa muda mrefu.

Matembezi hayo ni mojawapo ya shughuli mbalimbali ambazo zimeandaliwa na familia yake kuadhimisha umri huo wa karne nzima.

Kwenye video fupi iliyotolewa na Mamlaka ya Kusimamia Wanyamapori ya Uganda (AWU) wiki iliyopita, Bw Njonjo alisema kuwa anapenda kutembelea nchi hiyo ikizingatiwa alisomea huko.

“Nilijawa na furaha sana kuwaona sokwe; watoto wawili na ndume wakubwa,” akasema Bw Njonjo.

Baadaye, wasimamizi wa mbuga hiyo walimpa cheti maalum pamoja na ujumbe wa heri njema (picha ndogo).

“Ahsante Bw Njonjo kwa kutembelea mbuga hii. Tutakukumbuka daima,” ilisema mbuga hiyo kwenye taarifa.

Wakenya mbalimbali pia wametoa jumbe za kumtakia heri njema anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Akiwa na miaka 100, Bw Njonjo ndiye kiongozi wa pekee ambaye yuko hai aliyehudumu katika Baraza la Kwanza la Mawaziri alilobuni Mzee Kenyatta mnamo 1963.

Charles Njonjo ni mwanawe Bw Josiah Njonjo, aliyekuwa Chifu Mkuu katika enzi ya ukoloni. Alizaliwa katika eneo la Kibichuku mjini Kabete, Kaunti ya Kiambu (wakati huo ikiwa wilaya).

Mwanasiasa huyo ana ndugu wanane; kaka wanne na dada wanne. Kufikia wakati huu, watatu kati yao wangali hai.

Hakuteseka hata kidogo utotoni mwake. Inadaiwa alikuwa akipelekwa shuleni kwa farasi iliyoendeshwa na mmoja wa wafanyakazi walioajiriwa na babake. Babake ni miongoni mwa watu walioshirikiana na Waingereza walipowasili nchini Kenya.

Bw Njonjo alisomea katika shule ya msingi ya Gwa Gateru. Shule hiyo ilihusishwa na Kasisi Canon Leakey, aliyesimamia Kanisa la Kianglikana (ACK) katika eneo la Kabete. Baadaye, alijiunga na shule ya upili ya Alliance karibu na eneo la Kikuyu. Alisoma pamoja na watu maarufu kama vile mwanasiasa Jeremiah Nyagah, ambaye baadaye walihudumu pamoja katika baraza la mawaziri.

Kwa kuwa alizoea chakula maalum na maisha ya juu akiwa nyumbani kwao, alilalama kwamba maisha ya Alliance “yalikuwa magumu.” Anakumbuka: “Wanafunzi hawakuwa wakivaa viatu na walioga maji baridi. Ni katika shule hii ambapo nilikula ugali kwa mara ya kwanza.”

Mnamo 1939, Bw Njonjo alijiunga na Taasisi ya King’s nchini Uganda ambako alisoma kwa miaka miwili. Alikuwa katika darasa moja na Bw Frederick Mutesa, ambaye baadaye alifanywa kuwa Mfalme (Kabaka) wa jamii ya Wabaganda ya Uganda.

Baada ya kumaliza masomo katika taasisi hiyo, babake alimtaka kuelekea nchini Uingereza kwa masomo zaidi. Hata hivyo, hakuwa na fedha za kutosha kumfadhili kimasomo. Badala yake alienda Chuo cha Fort Hare nchini Afrika Kusini kwa miaka mitatu alikosomea masuala ya Utawala, Soshiolojia, na Sheria ya Kilatino.

You can share this post!

Uingereza itakoma kutoa tahadhari za usafiri Kenya –...

Kesi za waliouawa na polisi bado zinajikokota -IPOA

adminleo