Michezo

Bao la Aguero lasaidia City kuondoka na ushindi finyu

January 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MSHAMBULAJI hodari Sergio Aguero alifunga bao lake la sita katika mechi tatu za karibuni, na kusaidia klabu yake ya Manchester City kuibuka na ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya Sheffield United, katika mechi ya Ligi Kuu (EPL) iliyochezewa Bramall Lane siku ya Jumanne.

Bao hilo liliingia wakati wenyeji Sheffield walionyesha dalili za kutoka sare na miamba hao, katika mechi ambayo kipa Dean Henderson alidhihirisha mchezo wa hali ya juu ikiwemo kupangua penalti ya Gabriel Jesus.

Aguero alifunga muda mfupi tu baada ya Sheffield kukaribia kufunga bao langoni mwa Vity, baada ya Oli McBurnie kukosea tu kidogo kumimina shuti wavuni alipobaki na lango wazi.

Ushindi wa mabingwa hao watetezi wa EPL ulitokea baada ya kocha Pep Guardiola kufanya madiliko machache kikosini.

Umewaweka katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 51, alama 13 nyuma ya vinara Liverpool.

City wako pointi sita mbele ya Leicester City wanaokamata nafasi ya tatu, lakini kabla ya mechi ya Foxes jana dhidi ya West Ham United.

Sheffield chini ya kocha Chris Wilder wamefikisha pointi 33.

Kabla ya kucheza na Sheffield, kocha Guardiola, ambaye awali kunoa vikosi vya Barcelona (Uhispania) na Bayern Munich (Ujerumani) alikuwa amebashiri mechi ngumu.

Uwanjani, hali ilikuwa ngumu kwa kikosi chake baada ya kuwekewa ukuta mgumu uliovuruga kabisa juhudi za washambuliaji kupenya.

Ni hali iliyomfanya kocha huyo kumuingiza Aguero kuokoa jahazi.

Licha ya kuwa na umri mkubwa wa miaka 31, raia huyo wa Argentina ameshangaza kwa kuendelea kusukuma matulinga wavuni mara kwa mara.

Yamchukua dakika sita

Ilimchukua dakika sita tu kufunga bao hilo baada ya kuingia kwa nafasi ya Jesus.

Kufikia sasa, mshambuliaji huyo amefunga mabao 21 katika mechi 23 kwenye mashindano yote ambayo City imeshiriki msimu huu, yakiwemo manane katika mechi tano zilizopita.

Matumaini ya timu yake kuhifadhi ubingwa wa EPL yamedidimia, lakini huenda mchango wake ukaisaidia timu hiyo katika mashindano mengine.

Cha kufurahisha zaidi kwa kocha Guardiola ni kurejea kwa beki mahiri Aymeric Laporte, ambaye amekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na jeraha.

“Tumefurahi sana kumkaribisha (Laporte) baada ya muda mrefu. Ndiye bora zaidi katika safu yetu ya ulinzi na ni miongoni mwa mabeki bomba duniani.”